Tanzania Yashinda Ubingwa wa CECAFA Wanawake 2025 Kupitia Twiga Stars

Tanzania Yashinda Ubingwa wa CECAFA Wanawake 2025 Kupitia Twiga Stars

Timu ya taifa ya soka ya Wanawake ya Tanzania, maarufu kama Twiga Stars, imeandika historia kwa kutwaa ubingwa wa Mashindano ya CECAFA Wanawake 2025 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kenya.

Mechi hiyo ya mwisho ilichezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kuanzia saa 10:00 jioni, na imemaliza kampeni ya Twiga Stars kwa ushindi wa asilimia 100 katika michuano hiyo ya Afrika Mashariki na Kati.

Katika mafanikio haya ya kihistoria, Twiga Stars imeonesha uimara wa safu ya ulinzi kwa kutoruhusu bao lolote katika mechi zote nne ilizocheza. Wakiwa mbele ya mashabiki wa nyumbani, wachezaji wa Tanzania walifanikisha ushindi kwa kufunga jumla ya mabao 13 bila kuruhusu hata moja, hatua ambayo inaonesha maandalizi madhubuti kuelekea mashindano makubwa yajayo barani Afrika.

Tanzania Yashinda Ubingwa wa CECAFA Wanawake 2025 Kupitia Twiga Stars

Bao la Ushindi na Mbinu ya Mchezo

Bao pekee la ushindi dhidi ya Kenya lilitokea dakika ya 49, baada ya mpira kujaa wavuni kufuatia kutokuelewana kati ya beki wa Harambee Starlets, Enez Mango, na kipa wake Lilian Onyango Awuor. Awali katika kipindi cha kwanza, mshambuliaji Clara Luvanga na Opa Clement Tukumbuke walitengeneza nafasi za wazi ambazo zilielekezwa langoni mwa wapinzani lakini hazikuzaa matunda.

Kenya ilijitahidi kujibu mashambulizi kupitia mchezaji wao Violet Nanjala Wanyonyi, lakini safu ya ulinzi ya Tanzania ilibaki imara. Katika kipindi cha pili, Twiga Stars ilitawala mchezo kwa kasi na shinikizo kubwa, hali iliyowaweka Wakenya katika mashaka makubwa hadi kufungwa bao hilo la kujifunga.

Rekodi ya Twiga Stars Katika Michuano ya CECAFA

Twiga Stars ilianza michuano kwa kishindo kwa kuichapa Sudan Kusini mabao 4-0, kisha ikaifunga Burundi 6-0. Katika mechi ya tatu, waliichapa Uganda 2-0 kabla ya kufunga pazia kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Kenya. Kwa ushindi huo, Tanzania ilikusanya pointi 12 katika mechi zote nne, na hivyo kutawazwa mabingwa wa CECAFA 2025.

Kenya ilimaliza katika nafasi ya pili na kujinyakulia medali ya fedha, huku Uganda ikichukua nafasi ya tatu na kupewa medali ya shaba.

Kauli za Makocha Baada ya Mchezo

Kocha mkuu wa Kenya, Bi. Berdine Odemba, aliwapongeza Twiga Stars kwa ushindi wao na kusema kuwa Tanzania imekuwa kipimo kizuri cha maandalizi yao kuelekea mechi za kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (WAFCON).

Nawapongeza Tanzania kwa ushindi. Wameweza kutupa ushindani mzuri na wanaonekana wako tayari kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bw. Bakari Shime, alieleza kuwa mashindano haya yamekuwa ya manufaa makubwa kwa timu yake, hasa kwa kuonyesha kiwango bora na maandalizi mazuri kuelekea mashindano ya CAF Women’s Africa Cup of Nations nchini Morocco.

Tumeweza kuonyesha kiwango kizuri na tumeonyesha utayari. Niwapongeze Kenya wamekuwa kipimo kizuri kwetu.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Klabu ya Liverpool Yamwaga Mamilioni Kumnasa Florian Wirtz
  2. Viingilio Simba SC vs Kagera Sugar 22/06/2025
  3. Viingilio Yanga VS Dodoma Jiji 22/06/2025
  4. Tetesi Za Usajili Simba Leo 2025/2026
  5. Tetesi Za Usajili Yanga Leo 2025/2026
  6. Kaizer Chiefs Wavamia Dili la Yanga SC Kunasa Saini ya Percy Tau
  7. Mashujaa FC Yaanza Harakati za Kumsajili Beki wa Simba SC
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo