Asante Kotoko Yachukua Nafasi ya Yanga Kombe la Toyota Afrika Kusini
Mabingwa wa Kombe la FA, klabu ya Asante Kotoko kutoka Ghana, wamepata heshima kubwa ya kuwa wageni waalikwa kwenye Kombe la Toyota linalotarajiwa kufanyika nchini Afrika Kusini, huku wenyeji wakiwa ni klabu maarufu ya Kaizer Chiefs. Hii inakuja wakati ambapo bingwa mtetezi wa taji hilo, Young Africans (Yanga SC) kutoka Tanzania, ameenguliwa rasmi katika toleo la mwaka huu.
Kwa mara ya pili mfululizo, Kombe la Toyota litaandaliwa nchini Afrika Kusini huku likiwa na lengo la kuimarisha mshikamano wa bara la Afrika kupitia kandanda. Tofauti na msimu uliopita ambapo Yanga SC ilialikwa kama timu pekee kutoka nje ya Afrika Kusini na kutwaa taji hilo kwa kishindo kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs, mwaka huu nafasi hiyo imechukuliwa na Asante Kotoko kutoka Ghana.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Masoko na Biashara wa Kaizer Chiefs, Bi Jessica Motaung, waandaaji wameamua kualika klabu ya Asante Kotoko kwa toleo la 2025 badala ya Yanga. Motaung ameeleza kuwa mchezo huo utapigwa Julai 26, 2025 katika Uwanja wa Moses Mabhida uliopo jiji la Durban – eneo linalotambulika kama kitovu cha uzalishaji wa magari ya Toyota nchini Afrika Kusini.
“Tunayo heshima kuwakaribisha marafiki zetu kutoka Ghana katika ardhi ya Afrika Kusini. Asante Kotoko ni sehemu ya historia yetu. Kombe la Toyota linaruhusu Waafrika kuungana na kusherehekea kumbukumbu zetu,” alisema Motaung.
Aidha, amesisitiza kuwa Durban si tu ni kiini cha Toyota, bali pia ni sehemu bora ya kuandika ukurasa mpya wa historia ya soka barani Afrika.
Asante Kotoko Yapongeza Mwaliko wa Kihistoria
Mwenyekiti wa klabu ya Asante Kotoko, Apinkra Akwasi Awuah, hakuficha furaha yake baada ya timu yake kupokea mualiko huo wa heshima.
“Ni kwa furaha na matarajio makubwa kwamba tunakuja Afrika Kusini kwa toleo la 2025 la Kombe la Toyota. Kandanda daima limekuwa daraja la nguvu kati ya watu na mataifa,” alisema Awuah.
Aliongeza kuwa tukio hilo ni jukwaa la kuonyesha uwezo wa michezo kama chombo cha kuleta mshikamano, na alizipongeza Kaizer Chiefs na Toyota kwa kuendelea kuinua soka la Afrika.
Yanga SC: Bingwa Mtetezi Lakini Hatoshiriki Msimu wa 2025
Mwaka 2024, Yanga iliandika historia kwa kutwaa ubingwa wa kwanza wa Kombe la Toyota baada ya kuilaza Kaizer Chiefs kwa mabao 4-0. Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, haikupata mwaliko kwa mara ya pili mfululizo. Hili linaashiria kuwa mashindano haya huenda hayana mfumo wa moja kwa moja wa bingwa mtetezi kushiriki tena, bali uteuzi unategemea vigezo maalum vya waandaaji.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Milos Kerkez Ajiunga Rasmi na Liverpool kwa Ada ya Pauni Milioni 40
- Christian Eriksen Aondoka Man United Baada ya Utumishi wa Miaka Mitatu
- Kikosi cha Tanzania CHAN 2024: Wachezaji Kuingia Kambini Julai 7, 2025
- Yanga Yailaza Simba 2-0 na Kutwaa Kombe la Ligi Kuu Kwa Mara ya 31
- Vituo Vya Tiketi Mechi ya Yanga Vs Simba 25/06/2025
- Mechi ya Yanga vs Simba Kupigwa Chini ya Uangalizi wa Waamuzi Kutoka Misri
Leave a Reply