Benfica Yampa Mourinho Kibarua cha Kuiongoza kwa Miaka Miwili
Klabu ya Benfica imemtangaza rasmi José Mourinho (62) kuwa kocha wao mpya kwa kandarasi ya miaka miwili, akichukua nafasi ya Bruno Lage aliyefutwa kazi kufuatia kichapo dhidi ya Qarabag kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ujio huu wa “The Special One” unafungua ukurasa mpya katika safari yake ya ukocha, zaidi ya miongo miwili tangu alipokalia benchi la klabu hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2000. Mourinho, ambaye hajakuwa na timu tangu kuachana na Fenerbahce, anarudi Lisbon akiwa na kumbukumbu kubwa na uzoefu mpana ndani ya soka la Ureno na Ulaya.
Mkataba Mpya na Malengo ya Mourinho
Mourinho amesaini mkataba wa miaka miwili unaotarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2026/27. Hii inakuja baada ya kuachana na klabu ya Fenerbahce mwezi uliopita kufuatia kushindwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akiwa kwenye hafla ya utambulisho, Mourinho alieleza dhamira yake kwa maneno mazito:
“Nilikosea kwenda Fenerbahce, lakini sikujutia. Nilitoa kila kitu hadi siku ya mwisho. Kuinoa Benfica ni kurudi kwenye kiwango changu.”
Maneno haya yanaashiria ari na ujasiri wa kocha huyu mkongwe, anayelenga kuirejesha Benfica kileleni mwa mashindano ya ndani na barani Ulaya.
Tamko la Uongozi wa Benfica
Rais wa klabu, Rui Costa, hakuficha furaha yake kwa kumpata Mourinho:
“Mourinho hahitaji utambulisho. Ni fahari na heshima kubwa kumpata tena hapa Benfica. Tunataka kocha mwenye rekodi ya ushindi, na ni vigumu kumpata mtu aliye na historia ndefu kuliko yeye.”
Tamko hili linaonyesha jinsi Benfica inavyoamini uwezo wa Mourinho kurejesha hadhi ya klabu hiyo na kuleta matokeo ya haraka.
Historia Fupi ya Mourinho Benfica na Mafanikio Yake
Mourinho alianza safari yake ya ukocha Benfica mwaka 2000, lakini aliondoka baada ya mechi 10 pekee. Hata hivyo, jina lake liliendelea kung’ara akiwa na timu nyingine kubwa duniani. Aliwahi kushinda makombe muhimu na Porto, Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Manchester United na Roma, na mara mbili kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kurudi kwake Benfica kunazua msisimko mkubwa, hasa kwa mashabiki wanaokumbuka historia yake na klabu hiyo. Uwepo wake pia unaleta hamasa kuelekea mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi huu dhidi ya Chelsea, timu ambayo aliwahi kushinda nayo mataji matatu ya Ligi Kuu England.
Hali ya Benfica na Ratiba ya Kwanza kwa Mourinho
Kwa sasa Benfica ipo nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu ya Ureno ikiwa na pointi tano nyuma ya vinara Porto. Mourinho anatarajiwa kuanza rasmi majukumu yake mwishoni mwa wiki hii dhidi ya Vila das Aves, timu ambayo pia aliwahi kuinoa katika siku za awali za taaluma yake. Mashabiki wa klabu hiyo wanatarajia kuona mabadiliko ya haraka, hasa kwa kuzingatia rekodi ya Mourinho ya kuleta matokeo mara moja anapoanza kazi mpya.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo Wiliete Sc vs Yanga Leo 19/09/2025
- Kikosi cha Yanga vs Wiliete Sc Leo 19/09/2025
- Wiliete Sc Vs Yanga Leo 19/09/2025 Saa Ngapi?
- Ratiba ya Mechi za CAF Leo 19 September 2025
- Gamondi Atamba na Singida BS Baada ya Kutwaa Ubingwa wa Haraka
- Ratiba ya Mechi za Leo 18 September 2025
- Simba SC Yaondoka na Kikosi cha Wachezaji 23 kuelekea Botswana Leo 17/09/2025
Leave a Reply