Simba Yamtambulisha Hemed Suleiman Kama Kocha wa Mpito

Simba Yamtambulisha Hemed Suleiman Kama Kocha wa Mpito

Simba imemtambulisha Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania, Hemed Suleiman “Morocco”, kama kocha wa mpito wa klabu hiyo wakati ikikamilisha taratibu za kumpata kocha mpya wa kudumu. Hatua hii imekuja baada ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids, kusitisha mkataba wake na kujiunga na Raja Casablanca ya Morocco, akifuatana na wasaidizi wake wanne.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya klabu, Hemed Morocco ataiongoza Simba katika michezo ya kimataifa, ikiwemo mchezo muhimu wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United utakaochezwa Septemba 28, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Simba Yamtambulisha Hemed Suleiman Kama Kocha wa Mpito

Sababu za Uteuzi wa Hemed Morocco

Simba imefafanua kuwa uamuzi wa kumteua Morocco unatokana na changamoto za kiufundi zilizopo kwa sasa. Kocha msaidizi Selemani Matola hataruhusiwa kuongoza benchi la ufundi kwenye mchezo huo baada ya kupokea kadi nyekundu katika mechi ya kwanza iliyochezwa wiki iliyopita.

Aidha, klabu hiyo imeeleza shukrani zake kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuridhia ombi la kuruhusu Morocco, ambaye kwa sasa ni kocha wa Taifa Stars, kusaidia kikosi hicho kwa muda hadi pale utaratibu wa kumpata kocha mpya wa kudumu utakapokamilika.

Rekodi ya Hemed Morocco

Kabla ya kutua Simba, Morocco amekuwa akiiendesha Taifa Stars, akiiwezesha kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024. Uzoefu huo unampa nafasi ya kuiongoza Simba katika kipindi kigumu, hasa kutokana na umuhimu wa michuano ya kimataifa kwa hadhi na matarajio ya klabu.

Kuondoka kwa Benchi la Ufundi la Fadlu Davids

Kuondoka kwa Fadlu Davids kumeacha pengo kubwa, kwani aliondoka pamoja na benchi lake lote la ufundi, akiwemo msaidizi wake Darien Wilken. Kupitia ujumbe wa kuaga, Wilken alieleza heshima aliyoipata ndani ya Simba na kusisitiza kuwa klabu hiyo imekuwa zaidi ya timu kwake, bali ni familia.

“Kwa muda niliokaa hapa nimejifunza na kushirikiana na jumuiya yenye shauku na matarajio makubwa. Simba itaendelea kuwa sehemu muhimu ya safari yangu ya ukocha, na nitaendelea kuisapoti,” alisema Wilken.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Ratiba ya Mechi za Leo 22/09/2025
  2. Matokeo ya Gaborone United vs Simba leo 20/09/2025
  3. Hiki Apa Kikosi cha Simba vs Gaborone United leo 20/09/2025
  4. Viwango Vya FIFA Duniani 2025 (FIFA Rankings)
  5. Taifa Stars Yashuka Nafasi Nne Katika Orodha Mpya ya Viwango vya FIFA
  6. Benfica Yampa Mourinho Kibarua cha Kuiongoza kwa Miaka Miwili
  7. Yanga Yaanza Msimu wa Ligi ya Mabingwa Kwa Ushindi wa 3-0
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo