Ibenge Afungua Kampeni za Ligi Kuu kwa Ushindi wa 2-0 Dhidi ya Mbeya City

Ibenge Afungua Kampeni za Ligi Kuu kwa Ushindi wa 2-0 Dhidi ya Mbeya City

Waoka mikate, Azam FC wameanza msimu wa Ligi Kuu Bara 2025/26 kwa kishindo baada ya kuwalaza ‘Purple Nation’ Mbeya City FC mabao 2-0 katika dimba la Azam Complex, Chamazi. Ushindi huu umempa kocha mpya Florent Ibenge mwanzo mzuri kwenye safari yake ya kwanza ya kufundisha timu ya Tanzania.

Ibenge Afungua Kampeni za Ligi Kuu kwa Ushindi wa 2-0 Dhidi ya Mbeya City

Azam FC Yaonyesha Makali Uwanjani

Mchezo huu uliokuwa wa kwanza kwa Azam kwenye Ligi Kuu, ulitawaliwa na nidhamu ya mchezo na mbinu sahihi. Dakika ya 32, Nassro Saadun aliwavusha wenyeji mbele baada ya kumalizia mpira wa kona uliopangwa vyema na Feisal Salum, kisha kumpata Abdul Suleiman Sopu aliyetoa pasi murua ya bao hilo.

Hadi mapumziko, timu zote zilionekana kushambuliana kwa zamu, lakini ulinzi wa pande zote mbili ulikuwa imara. Sekunde chache baada ya kipindi cha pili kuanza, Azam waliongeza bao la pili kupitia kiungo wao Feisal “Fei Toto” Salum. Bao hilo lilitokana na umakini wa Baraket Hmidi ambaye alitengeneza nafasi na kumpa pasi safi Feisal kumalizia kwa ustadi.

Mbeya City Yajaribu Kupambana Bila Mafanikio

Mbeya City ambayo ilikuwa ikicheza mchezo wake wa pili wa ligi baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate, ilionyesha juhudi kubwa kutafuta matokeo. Kocha wao Malale Hamsini alifanya mabadiliko kadhaa kwa kuwatoa Habib Kyombo na Eliud Ambokile na kuingiza Peter Mwalyanzi pamoja na Hamad Majimengi. Hata hivyo, maboresho hayo hayakubadili matokeo ya uwanjani.

Mbinu na Mabadiliko ya Ibenge

Kocha Ibenge, licha ya kuongoza kwa mabao mawili, hakuacha kikosi chake kikiwa na upungufu wa nguvu. Alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Saadun, Sadio Kanoute, Sopu na Baraket na nafasi zao kuchukuliwa na Jephte Kitambala, James Akaminko, Muhsin Malima na Pape Doudou Diallo. Hatua hiyo ilidumisha uimara wa kikosi na kuhakikisha ushindi unakamilika kwa alama tatu muhimu.

Nyota wa mchezo alichaguliwa kuwa Baraket Hmidi, ambaye mchango wake ulionekana wazi kupitia nafasi alizotengeneza, ikiwemo kusaidia bao la pili lililofungwa na Feisal.

Baada ya ushindi huu wa 2-0, Azam FC sasa inarudi mazoezini kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Merreikh FC Bentiu. Mchezo huo utapigwa Septemba 28, kwenye Uwanja wa Azam Complex. Azam wakiwa wameshinda mabao 2-0 ugenini, wanahitaji ushindi wowote au sare ili kufuzu hatua inayofuata ya michuano hiyo.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania 2025/2026
  2. Matokeo ya Yanga vs Pamba Jiji Leo 24/09/2025
  3. Vilabu Bora Afrika 2025 (CAF Club Ranking 2025)
  4. Hat-Trick ya Mayele Yaipa Pyramids Ubingwa wa FIFA African-Asian-Pacific
  5. Ratiba ya NBC Premier league 2025/2026
  6. Serikali Yatoa Ufafanuzi Pamba Jiji Kufanya Mazoezi Gizani Uwanja wa Taifa
  7. Ratiba ya Mechi za Leo 24/09/2025
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo