KMKM Yatinga Raundi ya Pili ya CAF Baada ya Kuichapa AS Port ya Djibouti

KMKM Yatinga Raundi ya Pili ya CAF Baada ya Kuichapa AS Port ya Djibouti

Miamba wa soka visiwani Zanzibar, KMKM, wameendelea kutandika historia kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) baada ya kusonga mbele kwa kishindo hadi raundi ya pili. Hii ni kufuatia ushindi muhimu wa mabao 2-1 walioupata dhidi ya AS Port ya Djibouti kwenye dimba la New Amaan Complex, Unguja. Ushindi huo umeifanya KMKM kufuzu kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya awali pia kuibuka na ushindi wa 2-1 katika mchezo wa kwanza ugenini.

KMKM Yatinga Raundi ya Pili ya CAF Baada ya Kuichapa AS Port ya Djibouti

Safari ya KMKM Raundi ya Kwanza

KMKM, ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho Zanzibar pamoja na Ngao ya Jamii, waliingia dimbani wakiwa na morali ya juu. Timu hiyo ilitumia vyema faida ya ushindi wa awali na kuendeleza moto wao mbele ya mashabiki waliokuwa wamejazana Amaan.
Katika dakika ya 43, nahodha wa kikosi hicho, Ahmed Ishaka ‘Babui’, aliwapa mashabiki burudani ya mapema kwa kufumania nyavu na kuwapa KMKM uongozi hadi mapumziko.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa huku pande zote zikionekana kutafuta nafasi ya kusonga mbele. Dakika ya 61, AS Port walipata pigo baada ya kumkosa beki wao wa kati Mohammed Saleh, aliyeonyeshwa kadi. Dakika kumi baadaye, KMKM nao walimpoteza beki wao, Mohammed Mtumwa Hassan, hali iliyofanya mchezo kuchezwa kwa wachezaji 10 kwa kila upande.

AS Port waliweza kusawazisha dakika ya 84, lakini furaha yao haikudumu kwani dakika chache kabla ya filimbi ya mwisho, KMKM waliongeza bao la pili na kuhitimisha ushindi wa mabao 2-1. Ushindi huu ukawapeleka rasmi raundi ya pili ya michuano ya CAF, hatua ambayo timu hiyo inataka kuandika historia mpya kwa soka la Zanzibar.

Kocha Hababuu Afunguka

Kocha wa KMKM, Hababuu Ali, hakuweza kuficha furaha yake baada ya kipute hicho. Alieleza wazi kuwa siri ya mafanikio ilikuwa ni maandalizi ya kina na mshikamano wa wachezaji.

“Hii ni hatua muhimu kwa KMKM, lakini bado safari ni ndefu. Tunahitaji kuongeza nguvu na kujiandaa vyema kwa raundi ijayo,” alisema Hababuu.

Kuelekea Raundi Inayofuata

Baada ya kutinga raundi ya pili, KMKM sasa inasubiri mshindi kati ya Azam FC ya Tanzania na El Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini. Azam FC wanaonekana kuwa na nafasi nzuri baada ya kushinda mchezo wa kwanza kwa mabao 2-0 ugenini.

Mbali na KMKM, timu zingine zilizojihakikishia nafasi ya raundi ya pili ni Ferroviario Maputo ya Msumbiji, ambayo iliiondoa AS Fanalamanga ya Madagascar, pamoja na Royal Leopards ya Eswatini waliowapiga Young Africans ya Namibia kwa jumla ya mabao 7-0.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Viingilio Mechi ya Yanga vs Wiliete SC 27/09/2025
  2. Sergio Busquets Atangaza Kustaafu Soka Mwishoni Mwa Msimu Huu
  3. Kocha Folz Aahidi Ushindi Mkubwa Mechi ya Marudiano Dhidi ya Wiliete
  4. Yanga SC Yazindua Jezi Mpya Ili Kulinda Mapato Dhidi ya Jezi Feki
  5. Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
  6. Wafungaji Bora Ligi Kuu ya NBC Tanzania 2025/2026
  7. Uwanja wa Jamhuri Dodoma Kuwa Makazi Mapya ya Mtibwa Sugar
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo