Haaland Sasa ni Miongoni mwa Wafungaji Bora 10 wa Muda Wote Man City
Erling Haaland ameweka historia mpya ndani ya Manchester City baada ya kuingia rasmi kwenye orodha ya wafungaji bora 10 wa muda wote Man City. Hii imekuja mara baada ya Mnorwe huyo kufunga mabao mawili muhimu katika ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Burnley, matokeo yaliyompa nafasi ya kupanda hadi nafasi ya 9 kwenye rekodi za mabao ya klabu hiyo.
Kwa sasa, Haaland amefikisha mabao 133 kwenye michezo 153, akiwapiku majina ya kihistoria kama Billy Gillespie na Fred Tilson, waliowahi kushikilia jumla ya mabao 132 kila mmoja. Hata hivyo, bado ana safari ndefu kufikia rekodi ya mabao 260 inayoendelea kushikiliwa na kinara wa muda wote wa City, Sergio Aguero.
Rekodi za Haaland ni za kipekee na zinaonesha ni kwa namna gani anavyotambulika kama mmoja wa washambuliaji bora zaidi katika historia ya soka la dunia. Tofauti kubwa ni kwamba, wakati Gillespie alihitaji mechi 231 na Tilson akacheza mechi 275 kufikisha mabao yao 132, Haaland ameyafikia kwa haraka zaidi akiwa na ufanisi wa ajabu mbele ya lango.
Aidha, Haaland amekuwa mfungaji bora zaidi wa muda wote wa Norway katika Premier League, akimzidi gwiji Ole Gunnar Solskjaer baada ya kufunga mabao 93 katika mechi 103 tu.
Rekodi Ndani ya Etihad Stadium
Magoli mawili dhidi ya Burnley pia yamempa nafasi ya pili kwa wingi wa mabao yaliyofungwa ndani ya Etihad Stadium. Haaland sasa ana mabao 52 katika michezo 51 pekee akiwa nyumbani, akimshinda Raheem Sterling aliyefunga 51 katika mechi 109.
Ni Sergio Aguero pekee aliyefunga zaidi ndani ya dimba hilo, akiwa na mabao 106 katika michezo 142. Hii inamfanya Haaland kuwa karibu na rekodi nyingine kubwa zaidi katika historia ya City.
Wachezaji wengine waliowahi kung’ara kwenye mabao ndani ya Etihad ni pamoja na Kevin De Bruyne (47), Carlos Tevez (38), David Silva (36), Gabriel Jesus (32), Phil Foden (31) na Yaya Touré (30).
Safari Yake Tangu 2022
Tangu kuwasili kwake kiangazi cha mwaka 2022, Haaland ameweka viwango vya juu vya ufungaji ambavyo havijawahi kushuhudiwa. Amewahi kutwaa Golden Boot ya Premier League mara mbili mfululizo (2022/23 na 2023/24).
Msimu wa 2022/23 ulikuwa wa kihistoria kwa sababu nyingi, ikiwemo kufunga mabao 36 kwenye Premier League rekodi mpya ya ligi hiyo na kumaliza msimu akiwa na jumla ya mabao 52, rekodi ya juu zaidi katika historia ya Manchester City kwa msimu mmoja.
Zaidi ya hapo, wiki hii Haaland ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kasi zaidi kufikisha mabao 50 katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, akihitaji mechi 49 pekee, akivunja rekodi ya awali iliyoshikiliwa na Ruud van Nistelrooy.
Kwa sasa, Haaland pia anaongoza chati za wafungaji wa mabao kwenye Premier League msimu huu akiwa na mabao 8 katika mechi 6.
Orodha ya Wafungaji Bora 10 wa Muda Wote Manchester City
Haaland sasa amejiunga rasmi na majina makubwa kwenye historia ya mabao ya Manchester City. Hivi ndivyo orodha inavyosimama:
- Sergio Aguero – 260
- Eric Brook – 177
- Tommy Johnson – 166
- Colin Bell – 153
- Billy Meredith – 152
- Joe Hayes – 152
- Francis Lee – 148
- Tommy Browell – 139
- Erling Haaland – 133
- Billy Gillespie & Fred Tilson – 132
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo ya Yanga vs Wiliete SC Leo 27/09/2025
- Yanga vs Wiliete SC Leo 27/09/2025 Saa Ngapi?
- Kikosi cha Yanga vs Wiliete SC Leo 27/09/2025
- KMKM Yatinga Raundi ya Pili ya CAF Baada ya Kuichapa AS Port ya Djibouti
- Sergio Busquets Atangaza Kustaafu Soka Mwishoni Mwa Msimu Huu
- Kocha Folz Aahidi Ushindi Mkubwa Mechi ya Marudiano Dhidi ya Wiliete
- Yanga SC Yazindua Jezi Mpya Ili Kulinda Mapato Dhidi ya Jezi Feki
- Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
Leave a Reply