Azam FC Yafuzu Raundi ya Pili CAFCC Baada ya Ushindi wa 4-0 Dhidi ya El Merriekh
Klabu ya Azam FC imefanikiwa kutinga raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 4-0 dhidi ya El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini.
Wawakilishi hao wa Tanzania walijihakikishia nafasi hiyo kwa kushinda mabao 2-0 ugenini katika mchezo wa kwanza kabla ya kukamilisha kazi nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kwa ushindi mwingine wa 2-0.
Katika pambano la marudiano lililochezwa jijini Dar es Salaam, Azam FC ilidhihirisha ubora wake kwa kufunga mabao mawili katika kila kipindi. Beki wa kati, Yoro Diaby, alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 16, na Nassoro Saadun akiongeza bao la pili sekunde chache kabla ya kipenga cha mapumziko kupulizwa. Matokeo hayo yalitosha kuipeleka Azam FC mbele kwa kishindo, ikiendeleza moto wa kocha wao mpya Florent Ibenge, ambaye alijiunga na timu hiyo mwanzoni mwa msimu huu akitokea Al Hilal ya Sudan.
Safari ya Azam FC na Hatua Inayofuata
Kwa ushindi huo, Azam FC sasa inajiandaa kuvaana na KMKM FC ya Zanzibar katika raundi ya pili ya CAFCC. Mechi hizo zinatarajiwa kupigwa kati ya tarehe 17 na 26 Oktoba, ambapo mshindi atapata nafasi ya kusonga mbele hadi hatua ya makundi—hatua ambayo Azam FC inawania kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwake mwaka 2004, ilipojulikana kwa jina la Mzizima.
KMKM FC yenyewe imefuzu hatua hiyo kwa kuiondoa AS Port ya Djibouti kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya kushinda mechi zote mbili kwa matokeo ya 2-1 visiwani Zanzibar. Hivyo, pambano kati ya Azam na KMKM linatarajiwa kuwa la kuvutia kwa kuwa litawakutanisha wawakilishi wawili wa Tanzania walioko kwenye kiwango bora.
Licha ya kupata matokeo mazuri, Azam ina nafasi ya kutafakari upungufu wake katika umaliziaji. Katika mchezo wa marudiano, washambuliaji wao akiwemo Japhte Kitambala, Hamdi Barakat, Suleiman ‘Sopu’ na kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’, walishindwa kutumia nafasi nyingi walizopata, jambo linaloweza kuwa changamoto iwapo halitashughulikiwa mapema kabla ya mechi kubwa za raundi ya pili.
Wawakilishi wa Tanzania Katika CAF 2024/2025
Azam inakuwa timu ya tano kutoka Tanzania kufuzu hatua ya pili ya mashindano ya CAF msimu huu. Kabla yao, KMKM FC na Singida Black Stars walitangulia Kombe la Shirikisho, huku Simba SC na Young Africans (Yanga SC) zikisonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Hata hivyo, si kila mwakilishi wa Tanzania aliyeweza kufanikisha safari hiyo. Klabu ya Mlandege SC, iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa, iliondoshwa na Insurance ya Ethiopia baada ya kupoteza kwa jumla ya mabao 4-3, licha ya ushindi wa 3-2 nyumbani uliokuwa hafifu kufuta kipigo cha 2-0 walichopokea ugenini.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo ya Simba vs Gaborone Leo 28/09/2025
- Ratiba ya Mechi za Leo 28/09/2025
- Singida Black Stars Yatinga Raundi Ya Pili Kombe la Shirikisho Afrika
- Real Madrid Yapoteza 2-5 Dhidi ya Atletico Madrid, Kichapo cha Kwanza kwa Xabi Alonso LaLiga
- Haaland Sasa ni Miongoni mwa Wafungaji Bora 10 wa Muda Wote Man City
- Yanga Yatinga Raundi ya Pili CAF Champions League Baada ya Ushindi wa 2-0
- KMKM Yatinga Raundi ya Pili ya CAF Baada ya Kuichapa AS Port ya Djibouti
- Viingilio Mechi ya Yanga vs Wiliete SC 27/09/2025
Leave a Reply