Arsenal yapata ushindi wa dakika za mwisho dhidi ya Newcastle United
Klabu ya Arsenal FC imeibuka na ushindi wa goli mbili kwa moja dhidi ya Newcastle United baada ya kufanya comeback ya nguvu kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England (EPL) uliopigwa katika dimba la St. James’ Park.
Magoli ya Arsenal yalifungwa na Mikel Merino dakika ya 86 kabla ya Gabriel Magalhães kupigilia msumari wa pili dakika ya 96 kupitia mpira wa kona uliopigwa na nahodha Martin Ødegaard. Awali, wenyeji Newcastle walikuwa mbele kwa goli la kichwa lililowekwa kambani na Nick Woltemade katika kipindi cha kwanza. Ushindi huu unaifanya Arsenal kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na alama 13, nyuma ya vinara Liverpool wenye pointi 15.
Mikel Arteta na vijana wake walianza chini ya shinikizo kubwa kutokana na historia ya hivi karibuni dhidi ya Newcastle kwenye uwanja huo, ambapo Arsenal walikuwa wamepoteza michezo mitatu mfululizo. Hata hivyo, ushindi huu wa dakika za lala salama umewapa mashabiki wa Gunners sababu ya kuamini kwamba safari ya ubingwa bado ipo mikononi mwao.
Kocha Arteta alisisitiza umuhimu wa ushindi huo akisema:
“Tulijadili kuhusu kufikia kiwango kinachofuata na namna tunavyopaswa kujifunza kutokana na makosa ya nyuma. Leo tumepata nafasi ya kuonyesha ubora na malengo yetu. Ushindi huu ni moja ya matukio makubwa ya msimu, hasa baada ya kuanza vibaya katika uwanja ambao ulikuwa mgumu kwetu. Timu imeonyesha ari ya kupigania kila dakika.”
Arteta pia alisisitiza kuwa ushindi huo ni ishara kwamba Arsenal inaweza kushindana kwa mbinu mbalimbali na kushinda katika mazingira magumu.
Changamoto kwa Newcastle United
Kwa upande wa wenyeji Newcastle, kocha Eddie Howe alionekana kukatishwa tamaa na namna walivyopoteza alama muhimu dakika za mwisho. Hii ni mara ya pili msimu huu kikosi chake kinapoteza mchezo kwenye muda wa nyongeza baada ya Liverpool kufanya hivyo mapema mwezi Agosti.
“Sidhani kama tulicheza mechi yetu bora, lakini kama tungeweza kushinda 1-0 ingekuwa faida kubwa kwetu. Kwa bahati mbaya tulishindwa kudumu na matokeo. Kasi na nguvu za mchezo huu zilikuwa changamoto kubwa. Tulipaswa kujibu changamoto hizo lakini hatukufanya vizuri kwenye mabao tuliyoruhusu. Goli la mwisho lilikuwa pigo kubwa sana.” – Eddie Howe.
Zaidi, Newcastle walipata pigo lingine baada ya beki wao wa pembeni, Valentino Livramento, kuondolewa uwanjani kutokana na majeraha ya goti. Howe alisema wanaendelea kufanya vipimo ili kubaini ukubwa wa tatizo.
Nafasi ya Arsenal kwenye mbio za ubingwa
Ushindi huu unakuja mara tu baada ya Liverpool kupoteza mchezo wao wa kwanza wa msimu, jambo lililowapa Arsenal nafasi ya kupunguza pengo. Arteta alieleza kuwa kwa muda mrefu ilionekana kama nafasi hiyo ingetoweka, lakini kikosi chake kiliamini hadi dakika ya mwisho.
Kwa mashabiki wa Arsenal, ushindi huu si wa pointi tatu pekee bali ni wa kisaikolojia – ushindi unaoonyesha uthabiti, nguvu na imani ya kupigania ubingwa baada ya misimu mitatu wakimaliza nafasi ya pili.
“Kushinda kwa namna tulivyofanya, wow – ni hisia nzuri sana! Soka ni hisia, na leo tumepitia hisia nzuri sana mwishoni mwa mchezo,” alisema Arteta kwa furaha.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo ya Simba vs Gaborone Leo 28/09/2025
- Ratiba ya Mechi za Leo 28/09/2025
- Singida Black Stars Yatinga Raundi Ya Pili Kombe la Shirikisho Afrika
- Real Madrid Yapoteza 2-5 Dhidi ya Atletico Madrid, Kichapo cha Kwanza kwa Xabi Alonso LaLiga
- Haaland Sasa ni Miongoni mwa Wafungaji Bora 10 wa Muda Wote Man City
- Yanga Yatinga Raundi ya Pili CAF Champions League Baada ya Ushindi wa 2-0
- KMKM Yatinga Raundi ya Pili ya CAF Baada ya Kuichapa AS Port ya Djibouti
- Viingilio Mechi ya Yanga vs Wiliete SC 27/09/2025
Leave a Reply