Pantev Aandaa Mbinu Kali za kuizamisha Petro de Luanda Ligi ya Mabingwa Afrika

Pantev Aandaa Mbinu Kali za kuizamisha Petro de Luanda Ligi ya Mabingwa

MENEJA Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev ameendelea kukisuka kikosi chake kuelekea mchezo wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro de Luanda ya Angola, ambapo kwa sasa amekuwa akiwaelekeza wachezaji wake namna ya kuimaliza timu hiyo kwa mabao mengi iwezekanavyo.

Mchezo huo utapigwa Novemba 23 mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinabainisha kuwa Pantev amekuwa akiwafundisha wachezaji wake mbinu za mchezo wa wapinzani wao pamoja na maelekezo ya namna ya kuutumia udhaifu wao ili kupata mabao. Inaelezwa kuwa kocha huyo amekuwa makini kuwaonesha video za Petro de Luanda zinazoonesha muundo wa uchezaji na wachezaji wao hatari wanaohitaji kudhibitiwa.

Chanzo chetu kilifafanua kuwa Pantev ameendelea kuandaa mfumo uliotumika juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo wakati Simba ikipata ushindi wa mabao 6-0, mfumo ambao sasa unafanyiwa marekebisho ili utumike kwenye mchezo dhidi ya Petro de Luanda.

Pantev Aandaa Mbinu Kali za kuizamisha Petro de Luanda Ligi ya Mabingwa Afrika

“Kocha amewaonesha wachezaji video za Petro de Luanda jinsi wanavyocheza pamoja na wachezaji wao hatari wa kuchungwa. Pia amewaonesha udhaifu wao, ambao watautumia kuwaadhibu. Video alizonazo na taarifa ambazo amekusanya kutoka Angola zinaonesha uimara wa timu hiyo uko kwa viungo pamoja na safu ya ulinzi, kwa maana hiyo ametengeneza mfumo wa uchezaji ambao utawavuruga na kuachia mianya,” alisema mtoa habari wetu.

Aliongeza: “Anawaandaa pia viungo wa Simba kuwadhibiti viungo wa Petro de Luanda ili wasifurukute na kuua kabisa mfumo wa uchezaji wa timu.”

Aidha, chanzo hicho kiliongeza kuwa Pantev ameweka msisitizo mkubwa kwa safu ya ushambuliaji kutotumia nafasi vibaya wanapokaribia lango, akiwataka washambuliaji kuwa makini katika kila hatua ili kuhakikisha wanapata mabao ya kutosha. Inadaiwa kuwa kocha anataka ushindi wa mabao mengi ili Simba ianze hatua ya makundi ikiwa kinara wa kundi.

“Kocha anaamini kuwa kama tukipata ushindi wa mabao mengi, tutaaanza kwa kuongoza kundi na itakuwa ndiyo dira ya kuelekea katika michezo inayofuata,” kilisema chanzo hicho.

Kwa upande wa wapinzani wao, Petro de Luanda kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Angola ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza michezo sita, ikishinda minne na kupoteza miwili. Mpaka sasa, imefunga mabao 10 na kuruhusu mabao matano.

Katika mchezo wao wa mwisho, uliochezwa Novemba 9 mwaka huu, Petro ilifungwa bao 1-0 na C D Primeiro de Agosto, timu ambayo pia iliwahi kukutana na Simba kwenye michuano hiyo mwaka 2022.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri na ameahidi kuwa mashabiki watakaohudhuria Uwanja wa Benjamin Mkapa wataongeza nguvu kubwa kwa timu.

“Uwanja wa Benjamin Mkapa, ni kama ulijengwa kwa ajili ya Simba, unaweza kuona tumebaki peke yetu hapo, ni wakati wa kuendelea kuwaonesha wageni kuwa siku zote hawatokuwa salama wanapoingia kwenye uwanja huu.

“Ni uwanja unaoogopwa sana na wapinzani wanaocheza na Simba, ile amsha amsha ya mashabiki, kuwahimiza wachezaji wetu na kuwazomea wapinzani, inawachanganya sana kwa sababu pande zote nne zinakuwa za moto kwao,” alisema Ahmed.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Hat-Trick za Fernandes na Neves Zaipeleka Ureno Kombe la Dunia Baada ya Kuichapa Armenia 9-1
  2. Lyon Karibu Kumsajili Endrick Kutoka Real Madrid
  3. Wachezaji wa Simba Walioitwa Timu za Taifa November 2025
  4. Ratiba ya Yanga Klabu Bingwa 2025/2026
  5. Ratiba ya Simba Club Bingwa Afrika 2025/2026
  6. Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
  7. Ratiba ya Mechi za Ligi Kuu NBC Leo 09/11/2025
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo