Tanzania Yafuzu 16 Bora AFCON Kwa Mara ya Kwanza
Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeandika historia mpya ya soka la nchi hii baada ya kufuzu kwa mara ya kwanza kucheza hatua ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025). Mafanikio hayo yamepatikana kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Tunisia katika mchezo wa wa mwisho wa Kundi C uliochezwa kwenye Uwanja wa Stade Olympique de Rabat, Morocco, matokeo yaliyoihakikishia Tanzania tiketi ya hatua ya mtoano kupitia mfumo wa timu bora za nafasi ya tatu (Best Loser).
Katika mchezo huo uliokua wenye presha kubwa, Tunisia ilianza kwa kupata bao la kuongoza kipindi cha kwanza kupitia mkwaju wa penalti uliopigwa na Ismael Gharbi. Penalti hiyo ilitolewa baada ya VAR kumtaka mwamuzi Jean Jacques Ndala Ngambo kutazama tukio la beki Ibrahim Hamad kumzuia mchezaji Hazem Mastouri ndani ya boksi, wakati wa mpira wa adhabu wa Hannibal Mejbri.
Hata hivyo, Taifa Stars ilionyesha uimara na utulivu kipindi cha pili. Dakika ya tatu tu baada ya kuanza kwa kipindi hicho, Feisal Salum maarufu kama Fei Toto alisawazisha kwa shuti kali la nje ya boksi, akitumia pasi safi kutoka kwa Novatus Miroshi. Bao hilo lilirejesha matumaini na kuwa mwanzo wa historia mpya kwa Tanzania katika mashindano ya AFCON.
Nafasi ya Tatu na Tiketi ya Mtoano
Matokeo ya sare hiyo yameifanya Tanzania kumaliza nafasi ya tatu katika Kundi C ikiwa na pointi mbili, baada ya kucheza mechi tatu. Taifa Stars ilianza kundi kwa kupoteza 2-1 dhidi ya Nigeria, ikafuata sare ya 1-1 dhidi ya Uganda, kabla ya kuhitimisha kwa sare nyingine ya 1-1 dhidi ya Tunisia.
Kwa matokeo hayo, Tanzania imefanikiwa kufuzu kama moja ya timu bora za nafasi ya tatu, ikiungana na Msumbiji, Benin na Sudan. Katika msimamo wa timu za nafasi ya tatu, Tanzania imeipiku Angola kwa vigezo vya mabao ya kufunga, licha ya timu zote kuwa na pointi sawa na tofauti ya mabao ya -1. Tanzania imefunga mabao matatu, huku Angola ikifunga mawili, jambo lililoipa Stars tiketi ya kihistoria ya 16 bora.
Historia Mpya Baada ya Safari Ndefu
Huu ni ushindi wa kipekee kwa Taifa Stars, hasa ikizingatiwa kuwa katika ushiriki wake wa awali wa AFCON—1980, 2019 na 2023—timu hiyo ilikuwa ikimaliza safari yake hatua ya makundi. Safari ya AFCON 2025 imeleta sura tofauti, ikionyesha ukuaji, uzoefu na mshikamano wa kikosi cha Stars katika mashindano ya juu barani Afrika.
Mechi Ijayo Dhidi ya Morocco
Baada ya kufuzu, sasa Taifa Stars inajiandaa kwa changamoto nyingine kubwa dhidi ya wenyeji Morocco katika hatua ya 16 bora.
Mchezo huo wa mtoano unatarajiwa kuchezwa Jumapili huko Rabat. Kwa upande mwingine, Tunisia iliyomaliza nafasi ya pili katika Kundi C itakutana na Mali katika mchezo wake wa mtoano.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Msimamo wa Kundi C La Tanzania AFCON 2025
- Kikosi cha Tanzania Taifa Stars vs Uganda Leo 27/12/2025
- Matokeo ya Uganda Vs Tanzania Taifa Stars Leo 27/12/2025
- Uganda vs Tanzania Taifa Stars Leo 27/12/2025 Saa Ngapi?
- Ratiba ya Mechi za AFCON Leo 27/12/2025
- Msimamo wa Makundi AFCON 2025
- Bao la Dakika za Mwisho la Patson Daka Lainusuru Zambia Dhidi ya Mali, Mechi Ikiisha 1-1






Leave a Reply