Ateba Tayari Kutinga Uwanjani: Simba SC vs Fountain Gate
Klabu ya Simba SC imepata ahueni kubwa baada ya straika wao mpya, Lionel Christian Ateba, kukamilisha taratibu zote za kisheria zilizokuwa zikimkwamisha kuanza kucheza rasmi.
Ateba, ambaye alijiunga na Simba hivi karibuni kutoka USM Alger ya Algeria, anatarajiwa kuonekana uwanjani kwa mara ya kwanza katika mechi ya Jumapili ijayo dhidi ya Fountain Gate, itakayofanyika kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, Ateba alikuwa tayari kwa kucheza tangu alipojiunga na timu, lakini alikosa ruhusa ya kisheria inayohitajika kwa wachezaji wa kigeni kucheza nchini Tanzania.
Hali hii ilimfanya kukosa mechi ya awali dhidi ya Tabora United. Hata hivyo, Ahmed amethibitisha kuwa sasa straika huyo amepata kibali cha kuishi nchini, cha kufanya kazi, pamoja na leseni ya kucheza soka (ITC), hivyo anatarajiwa kujiunga kikamilifu na timu katika mechi dhidi ya Fountain Gate.
“Ateba alikuwa fiti kwa sababu alikuwa akifanya mazoezi na timu yake ya awali, USM Alger. Sasa, baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria, yuko tayari kuanza safari yake na Simba SC. Iwapo ataanza kwenye kikosi cha kwanza au ataingia kama mchezaji wa akiba, hilo litaamuliwa na kocha, lakini muhimu ni kwamba kila kitu kiko tayari,” alisema Ahmed.
Mabadiliko kwenye Kikosi cha Simba SC
Katika hatua nyingine, Ahmed Ally alithibitisha kuwa klabu ya Simba SC imeachana rasmi na straika Freddy Michael, ambaye alijiunga na timu hiyo kutoka Green Eagles ya Zambia msimu uliopita. Freddy anatarajiwa kujiunga na USM Alger, ambako atakuwa chini ya kocha aliyekuwa akifundisha Simba, Abdelhak Benchikha.
“Tumemuachia Freddy baada ya kocha Fadlu kutoridhishwa na kiwango chake na kuhitaji mshambuliaji mpya. Nafasi yake imechukuliwa na Ateba, ambaye anaonekana kuwa na uwezo mkubwa zaidi,” Ahmed aliongeza.
Freddy Michael ataungana na wachezaji wenzake wa zamani wa Simba, akiwemo Babacar Sarr na Sadio Kanoute, katika timu ya USM Alger, na kuendelea kuonesha uwezo wake chini ya kocha Benchikha.
Maandalizi ya Mechi Dhidi ya Fountain Gate
Simba SC, baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu, imeendelea na mazoezi makali chini ya uangalizi wa kocha Fadlu Davids. Ahmed ameeleza kuwa kocha huyo anaendelea kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mechi iliyopita, ili kuhakikisha timu inakuwa na muunganiko mzuri zaidi.
“Ukweli ni kwamba kikosi chetu kimeonyesha uwezo mkubwa, lakini bado kuna baadhi ya mapungufu ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi. Kikosi kina wachezaji wengi wapya ambao wanaonekana kuwa na kasi na nguvu, lakini bado wanahitaji muda wa kuzoeana. Mara watakapozoeana, naamini timu itakuwa tishio zaidi,” Ahmed alisema kwa kujiamini.
Simba SC, ambayo kwa sasa ipo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya ushindi wao dhidi ya Tabora United, inatarajia kuendeleza kasi hiyo katika mechi ijayo dhidi ya Fountain Gate, ambapo mashabiki wana matumaini makubwa ya kumuona straika wao mpya, Ateba, akiibuka na moto uwanjani.
Mapendekezo ya Mhariri:
Weka Komenti