Azam FC Yamwaga Mamilioni Ili Kumbakiza Nyota Wake Fei Toto

Azam FC Yamwaga Mamilioni Ili Kumbakiza Nyota Wake Fei Toto

Mabosi wa Azam FC wameonyesha wazi nguvu zao za kifedha baada ya kumwaga mamilioni ya pesa ili kuhakikisha wanamshikilia nyota wao, Zanzibar Finest, Feisal Salum maarufu kama Fei Toto, kwa msimu wa 2025/2026 na kwingineko. Kiungo huyo tegemeo wa Wanarambaramba sasa ameweka saini ya kuendelea kusalia klabuni hadi mwaka 2027, jambo linaloifanya dili hili kuwa moja kati ya madili makubwa zaidi kwenye historia ya Azam FC na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azam FC Yamwaga Mamilioni Ili Kumbakiza Nyota Wake Fei Toto

Awali, mkataba wa Fei Toto ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu wa 2025/2026, lakini sasa ameongeza mwaka mmoja zaidi. Habari kutoka ndani ya klabu zinathibitisha kuwa Azam FC imemlipa Dola 200,000 (takribani Shilingi milioni 520) kama ada ya kusaini mkataba mpya.

Zaidi ya hapo, Fei Toto ametengewa mshahara mnono ambao unasemekani ni milioni 80 kwa mwezi kabla ya kodi. Hii inamaanisha kwa mwaka atavuna takribani Shilingi milioni 960, huku akibaki na Shilingi milioni 50 kwa mwezi baada ya makato, sawa na Shilingi milioni 600 kwa mwaka. Kwa jumla, katika mwaka mmoja wa nyongeza, kiungo huyo atakusanya Shilingi bilioni 1.1 baada ya makato ya kodi.

Mbali na mshahara na ada ya usajili, Azam FC imempa Fei Toto nafasi ya kupata udhamini wa matangazo kutoka kwa moja ya kampuni zilizo chini ya umiliki wa Azam. Hii inaongeza thamani ya mkataba wake na kumuweka katika nafasi ya kipekee kati ya wachezaji wazawa wanaocheza Ligi Kuu.

Uamuzi wa Azam FC kumpa Fei Toto mkataba huu mnono unazikata rasmi tamaa klabu kongwe za Yanga SC na Simba SC, ambazo zimekuwa zikimuwinda kwa nguvu katika dirisha la usajili. Kwa dili hili, Azam FC imeonyesha kuwa iko tayari kulinda nyota wake kwa gharama yoyote.

Takwimu Zilizomfanya Awe Lulu Sokoni

Uchezaji bora wa Fei Toto katika misimu miwili iliyopita umechangia pakubwa uamuzi wa kumweka klabuni.

  • Msimu wa 2023/2024: Alimaliza akiwa mfungaji wa pili bora kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mabao 19 na pasi 7 za mwisho.
  • Msimu wa 2024/2025: Aliongoza chati ya pasi za mwisho kwa pasi 13 na kufunga mabao 4.

Uwezo wake si tu kwenye klabu, bali pia kwenye Taifa Stars, ambapo aling’ara katika mashindano ya CHAN 2024, akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi dhidi ya Burkina Faso.

Kauli ya Uongozi wa Azam FC

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’, amefafanua kuwa kuongeza mkataba wa Fei Toto ni matokeo ya mchango wake mkubwa kwa timu. “Fei alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na sisi. Tuliona umuhimu wa kumuongeza mwaka mmoja zaidi ili aendelee kutupa mchango wake mkubwa. Ni mchezaji mzuri na tunafurahia kuendelea naye,” alisema Popat.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Ifahamu Gaborone United Wapinzani wa Simba Ligi ya Mabingwa CAF 2025/2026
  2. Makundi ya CHAN 2025 Yatangazwa
  3. Ifahamu Wiliete Benguela Wapinzani wa Yanga CAF 2025/2026
  4. Simba Yatangaza Bei ya Jezi Zao Mpya za 2025-2026
  5. Msimamo wa Makundi CHAN 2025
  6. Ratiba ya Mechi za Leo 12/08/2025 CHAN
  7. Ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2025/2026
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo