CAF Yaagiza Uchunguzi Dhidi ya Vurugu Walizofanyiwa Simba Libya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeagiza uchunguzi kufanywa kuhusu vurugu zilizowakumba wachezaji wa Simba SC na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo nchini Libya. Hii ni baada ya mechi ya Kombe la Shirikisho la CAF dhidi ya Al Ahli Tripoli, ambapo matukio ya fujo yaliripotiwa kabla, wakati, na baada ya mchezo huo uliochezwa Jumapili iliyopita.
Motsepe: Hatutakubali Vurugu Kupunguza Heshima ya Soka Afrika
Rais wa CAF, Patrice Motsepe, akiwa nchini Kenya kwa mkutano wa watendaji wakuu wa shirikisho hilo, aliagiza uchunguzi wa haraka dhidi ya tukio hilo. Alisisitiza kuwa soka la Afrika haliwezi kudhalilishwa kwa vurugu, na hatakubali timu yoyote kuhusika katika vitendo vya aina hiyo. “Kama rais, sitavumilia kuona timu yoyote ikihusishwa na vurugu zinazoleta taswira mbaya kwa soka la Afrika,” alisema Motsepe wakati akijibu maswali ya wanahabari.
Mwandishi Collins Okinyo aliyeshuhudia mkutano huo alieleza kuwa Motsepe hakujua kuhusu tukio hilo mpaka alipoulizwa na mmoja wa waandishi wa habari. “Alishtushwa sana baada ya kuambiwa. Mara moja akaamuru mmoja wa maafisa wa CAF, Samson Adam, kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu vurugu zilizoripotiwa,” aliongeza Okinyo.
Malalamiko Rasmi ya Simba SC kwa CAF
Ingawa Simba SC haikutangaza rasmi kuhusu tukio hilo mara baada ya mechi, vyanzo mbalimbali vinaripoti kuwa tayari klabu hiyo imetuma malalamiko rasmi kwa CAF. Simba inalalamikia vurugu za mashabiki wa Al Ahli Tripoli, ambapo wachezaji wao walishambuliwa kwa kurushiwa chupa za maji, plastiki, na lugha za matusi, ikiwa ni pamoja na kauli za kibaguzi. Viongozi wa Simba walikusanya ushahidi uliothibitisha vurugu hizo na kuuwasilisha kwa CAF, wakitafuta hatua kali kuchukuliwa dhidi ya Al Ahli Tripoli.
Taarifa kutoka kwa vyombo vya habari na waandishi waliokuwepo uwanjani zinaeleza kuwa vurugu hizo zilianza wakati wa mechi na ziliendelea baada ya mchezo kumalizika.
Chupa za maji zilirushwa kwa wachezaji wa Simba, na hali ilikuwa ya hatari kiasi cha kuwafanya wakimbilie vyumbani kwa ulinzi. Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, alithibitisha tukio hilo, akieleza kuwa mashabiki wa Al Ahli Tripoli walifanya fujo kwa muda mrefu, huku wachezaji wa Simba wakilazimika kubaki vyumbani hadi vurugu zilipotulia.
Simba SC Kuendelea na Maandalizi ya Mechi ya Marudiano
Baada ya kurudi nchini Tanzania, kikosi cha Simba SC tayari kimeanza maandalizi ya mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahli Tripoli, utakaofanyika Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Kikosi hicho kilitawanyika katika makundi mawili wakati wa safari yao ya kurejea, huku kundi moja likipitia Uturuki na jingine likipitia Cairo, Misri.
Kocha Mkuu wa Simba SC, Fadlu Davids, amesema kuwa kikosi chake kiko tayari na hana majeruhi. Amewataka wachezaji wake kuendelea na maandalizi ya kikamilifu kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
“Mpango wetu wa awali wa kucheza ugenini umefanikiwa kwa kuhakikisha hatupotezi mechi. Sasa tunaelekeza nguvu kwenye kuhakikisha tunapata ushindi nyumbani ili tuweze kufuzu hatua ya makundi,” alisema Davids.
Simba SC inahitaji ushindi katika mchezo huo wa marudiano ili kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la CAF. Kocha Davids amesisitiza kuwa sare haitoshi, na hivyo anaandaa mbinu za kushambulia kuhakikisha timu yake inapata ushindi wa muhimu nyumbani.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ratiba ya Mechi za Leo 18 September 2024
- Kipa wa CBE Aeleza Hofu Yake Kuelekea Mchezo wa Pili Ligi ya Mabingwa, Amtaja Prince Dube
- Marefa Mechi za Simba na Yanga Klabu Bingwa Afrika
- Viingilio Mechi ya Yanga Vs CBE 21/09/2024
- Vituo Vya Kukata Tiketi Mechi ya Yanga Vs CBE 21/09/2024
- Mbappe Aanza na Goli Mechi ya Kwanza UEFA Akiwa na Madrid
- Fei Toto Atamani Bato Lake na Aziz Ki liendelee
Weka Komenti