Clatous Chama Aipa Singida Bs Ubingwa Wa CECAFA Kagame Cup 2025
Dar es Salaam, Septemba 15, 2025; Mwamba wa Lusaka, Clatous Chota Chama, aliibuka shujaa wa fainali baada ya kufunga mabao mawili na kuipeleka Singida Black Stars (Singida BS) kutwaa kwa mara ya kwanza ubingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu CECAFA Kagame Cup 2025, kufuatia ushindi wa mabao 2–1 dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan katika fainali iliotimua vumbi katika viunga vya dimba la KMC Complex.
Kikosi cha Singida BS kilianza mchezo kwa kasi, wakitumia vizuri mipira ya haraka katikati ya uwanja. Dakika ya 20, Chama aliandika bao la kwanza kwa shuti kali baada ya kuunganisha pasi safi, akiweka mashabiki wao katika hali ya furaha. Hata hivyo, Al Hilal walijibu mapema dakika ya 31 kupitia Taha Abdelrazig, na kufanya matokeo kuwa 1–1 hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilishuhudia Singida BS wakirejea wakiwa na ari mpya. Dakika ya 58, Chama tena alitimiza ahadi yake kwa kufunga bao la pili baada ya kumalizia krosi safi kutoka kwa Kelvin Kijili, bao lililothibitisha kwa nini jina lake limekuwa gumzo kwenye mashindano haya.
Ushindi wa Kihistoria kwa Singida Black Stars
Baada ya bao hilo la pili, wachezaji wa Singida BS walionyesha nidhamu ya hali ya juu wakilinda uongozi hadi filimbi ya mwisho. Ushindi huu uliandika historia mpya, ukiwa ni mara ya kwanza klabu hiyo kutwaa Kombe la Kagame, na kujiunga na orodha ya vilabu vya Tanzania vilivyowahi kubeba taji hilo, vikiwemo Simba, Yanga na Azam.
Tuzo Binafsi: Chama Ang’aa, Mnata Apewa Heshima
Kwa mchango wake mkubwa, Clatous Chama alinyakua tuzo mbili – Mchezaji Bora wa Mechi na Mfungaji Bora wa Mashindano. Mlinda mlango wa Singida BS, Metacha Mnata, naye aliibuka mshindi wa tuzo ya Kipa Bora kutokana na uchezaji wake thabiti kwenye mashindano yote.
Akizungumza mara baada ya mechi, Chama alisema:
“Timu pinzani ilikuwa bora kuliko sisi. Tulifuata maelekezo ya kocha na tukapata ushindi. Timu ni kubwa kuliko mchezaji yeyote, na kila mmoja anatakiwa kujua malengo ya timu kabla ya yake binafsi. Mashindano haya yametusaidia kuimarisha umoja wetu na kutuandaa kwa Kombe la Shirikisho Afrika.”
Kauli ya Kocha Miguel Gamondi
Kocha wa Singida BS, Miguel Gamondi, alionyesha fahari kwa wachezaji wake akisema:
“Nawapongeza kwa juhudi kubwa walizoonyesha. Clatous Chama amethibitisha ubora wake, na uwepo wa mchezaji kama yeye unarahisisha kuendesha soka la kushambulia. Mashabiki waendelee kutuunga mkono, tutaendelea kuwaletea furaha.”
Mapendekezo ya Mhariri:
- Bao la Dakika za Jioni Dhidi ya Burnley Lairudisha Liverpool kileleni EPL
- Man City Yaibuka na Ushindi wa 3-0 Dhidi ya Manchester United
- Kelvin John Aendeleza Moto Baada ya Kuifungia Aalborg Goli 2 Wakiilaza Middelfart 4-0
- Msimamo Ligi Kuu Ujerumani Bundesliga 2025/2026
- Juventus Yaicharaza Inter Milan 4-3 Ligi Kuu Italia
- Singida BS Yatinga Fainali ya CECAFA Kagame Cup Baada ya Kuifunga KMC 2-0
- Ratiba 16 Bora Ndondo Cup 2025
- Ratiba ya Mechi za Leo 14 September 2025
- Sare Dakika za Mwisho Yaizuia Chelsea Kukaa Kileleni mwa Msimamo wa EPL
Leave a Reply