Coastal Union Yapiga Hesabu Kali Kumchukua Anicet Kiazayidi
TANGA, TANZANIA — Klabu ya Coastal Union imeanza mipango ya kuhakikisha inampata aliyekuwa kocha wa Tabora United, Anicet Kiazayidi, kwa ajili ya kuiongoza timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa uongozi wa Coastal Union unafanya mazungumzo ya ndani na kupanga mikakati madhubuti ya kumleta kocha huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambaye aliwahi kuiongoza Tabora United kwa mafanikio kabla ya kuachana na timu hiyo.
Timu hiyo, ambayo hapo awali ilikuwa chini ya kocha Juma Mwambusi, ililazimika kufanya mabadiliko ya benchi la ufundi kufuatia matokeo yasiyoridhisha. Baada ya kuondoka kwa Mwambusi, nafasi ya ukocha ilichukuliwa na Joseph Lazaro, ambaye kwa sasa pia yupo kwenye hatihati ya kupoteza nafasi hiyo kutokana na mwenendo wa timu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka chanzo cha kuaminika ndani ya Coastal Union, klabu hiyo inaamini kuwa Anicet Kiazayidi anaweza kuirudisha timu hiyo kwenye kiwango kizuri kilichoonekana msimu uliopita, kabla ya kuanza kupata matokeo yasiyo ya kuridhisha katika msimu huu wa Ligi Kuu.
“Coastal inaamini kuwa, ikimpata Anicet timu hiyo inaweza kurejea kwenye ubora wake wa msimu uliopita, kutokana na kile ambacho wamekiona kwa Tabora United. Ni kocha mzuri kweli, hivyo kama mabosi watafikia makubaliano, basi tutakuwa naye na mtamuona. Kwa sasa jina lake ndilo lililopo vichwani mwa matajiri hao wa Tanga,” kilieleza chanzo hicho.
Anicet, ambaye anatoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliiongoza Tabora United kwa mafanikio kabla ya kuondoka. Hata hivyo, aliripotiwa kutofautiana na uongozi wa juu wa klabu hiyo, hali iliyosababisha kuachana nao.
Kwa sasa, kocha huyo hana timu yoyote anayoifundisha, jambo linalowapa Coastal Union fursa nzuri ya kumsajili bila ugumu wowote wa kisheria wala masharti magumu ya kuvunja mkataba.
Hali ya Coastal Union Katika Msimamo wa Ligi
Katika msimu uliomalizika, Coastal Union ilimaliza ligi katika nafasi ya nne na kufanikiwa kushiriki michuano ya kimataifa ya CAF.
Hata hivyo, msimu huu hali si shwari kwani hadi sasa klabu hiyo ipo katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 31, baada ya kushinda mechi saba, kutoka sare mara 10 na kupoteza michezo 11.
Msimu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara unatarajiwa kufikia tamati ifikapo Juni 22, huku klabu nyingi zikiwa zimebakisha michezo miwili pekee. Coastal Union kwa sasa inaonekana kulazimika kufanya maamuzi ya haraka na yenye tija kuhusu benchi lake la ufundi ili kurekebisha mwenendo wa timu kabla ya msimu mpya kuanza.
Mapednekezo ya Mhariri:
- Chelsea Yaipiga Bao Manchester United Usajili wa Liam Rory Delap
- Xabi Alonso Aahidi Kurejesha Ufalme wa Real Madrid
- Singida BS Yashindwa Kutamba Mbele ya Simba Ligi Kuu NBC
- Waliochaguliwa JKT Mujibu wa Sheria 2025 – Pakua PDF Hapa!
- Erik Ten Hag Atambulisha Rasmi Kama Kocha Mkuu Bayer Leverkusen
- Al Hilal ya Ibenge Yabeba Kombe la Ligi Kuu Mauritania 2024/25
Leave a Reply