Elie Mpanzu Kwenye Rada za Yanga na Simba
Katika hekaheka za soko la usajili la dirisha dogo, jina la Elie Mpanzu limeibuka kuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka nchini Tanzania. Winga huyu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) anawindwa na klabu mbili kongwe za Simba SC na Yanga SC, ambazo zote zimeonesha nia thabiti ya kumleta nchini na kuimarisha vikosi vyao. Hii ni hatua muhimu kwa timu zote mbili zinazojiandaa kwa michuano ya ndani na kimataifa.
Kwa muda mrefu sasa, Simba SC imekuwa ikitajwa katika mbio za kusaka huduma ya Mpanzu na iliwahi kuripotiwa kua wapo kwenye mazungumzo ya kumsajili tangu msimu uliopita. Hata hivyo, mpango huo ulivunjika baada ya AS Vita, klabu ya Mpanzu ya zamani, kuvuruga mazungumzo hayo dakika za mwisho. Baada ya Simba kushindwa kumpata winga huyo, Mpanzu alikimbilia Ubelgiji kujiunga na KRC Genk, ambako aliendelea kucheza kwa kiwango cha juu.
Licha ya kushindwa kumnasa kwenye dirisha kubwa, Simba haikukata tamaa na bado ilikuwa kwenye mazungumzo ya kumrejesha winga huyo nchini. Lakini, mara tu baada ya habari za Simba kufufua mazungumzo na Mpanzu, Yanga SC nayo ilijitokeza kumsaka kwa nguvu kubwa, ikiweka dau la juu zaidi ili kumnyakua nyota huyo.
Simba SC ilianza mazungumzo mapema kwa kumwekea Mpanzu ofa ya dola 130,000 kwa ajili ya kumshawishi kusaini mkataba. Hata hivyo, Yanga SC, ikiwa na nia ya kumzidi mpinzani wake, iliweka dau la dola 150,000, jambo lililoibua ushindani mkali kati ya klabu hizo mbili.
Mpanzu, akiwa bado nchini Ubelgiji, alithibitisha kuwa Yanga SC na Simba SC zote zimemfuata na kumwekea ofa, lakini bado hajafanya maamuzi ya mwisho kuhusu ni klabu gani atajiunga nayo. “Ni kweli Yanga wamenifuata wakati naendelea na mazungumzo na Simba, lakini bado sijaamua maamuzi ya mwisho. Nakuja Tanzania hivi karibuni,” alisema Mpanzu.
Sababu za Yanga Kumuwinda Mpanzu
Yanga SC imekuwa na upungufu katika nafasi ya winga, hasa upande wa kulia, ambapo Denis Nkane na Maxi Nzengeli wamekuwa wakiichezea. Kwa upande wa kushoto, Farid Mussa pekee ndiye anayeonekana kuwa na kiwango bora, lakini kuongezeka kwa Mpanzu kutaimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo. Kocha Miguel Gamondi amekuwa akitumia mifumo inayotegemea zaidi viungo, na hivyo ujio wa Mpanzu utaongeza mbinu mpya kwenye safu ya ushambuliaji wa Yanga.
Kwa muda mrefu, Yanga SC na Simba SC zimekuwa zikishindana kwenye soko la usajili, wakinyang’anyana wachezaji wenye uwezo mkubwa. Mfano mzuri ni usajili wa hivi karibuni wa Yusuf Kagoma kutoka Singida FG, ambaye alizua mvutano mkubwa kati ya klabu hizi mbili.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Yanga Yafanya ‘Homework’ ya Kutosha, Gamondi Apania Tiketi ya Makundi
- Fadlu Davids Afurahishwa na Ngome ya Ulinzi Simba
- Zahera Aanza Tambo Baada ya Ushindi wa Kwanza wa Namungo Ligi Kuu
- Msimamo NBC Premier league 2024/2025 | Ligi Kuu Bara
- Azam FC Yalenga Ushindi wa Kwanza Ligi Kuu Dhidi ya Simba
- Gamondi Apania Ushindi Mnono Mechi ya Marudiano Dhidi ya CBE
- CAF Yaagiza Uchunguzi Dhidi ya Vurugu Walizofanyiwa Simba Libya
Weka Komenti