Erik Ten Hag Atambulisha Rasmi Kama Kocha Mkuu Bayer Leverkusen
KLABU ya Bayer Leverkusen imemtangaza rasmi Mholanzi Erik ten Hag kuwa kocha wake mpya, akichukua nafasi ya Mhispania Xabi Alonso ambaye amejiunga na Real Madrid ya kwao. Uamuzi huu umekuja baada ya Alonso kuiongoza Leverkusen kwa mafanikio makubwa, kabla ya kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita. Kwa mujibu wa taarifa rasmi, Leverkusen watapokea kiasi cha euro milioni 13 hadi 15 kutoka Real Madrid kama fidia kwa kuondoka kwa Alonso.
Ten Hag, mwenye umri wa miaka 55, amepewa mkataba wa kuinoa timu hiyo hadi mwaka 2027. Uteuzi huu unakuja katika kipindi ambacho klabu hiyo kutoka Bundesliga inahitaji msukumo mpya kufuatia kushuka kwa kasi ya matokeo yao mwishoni mwa msimu, licha ya mafanikio ya awali ya kushinda taji la ligi bila kupoteza mechi yoyote katika msimu wa 2023-2024.
Katika taarifa yake ya kwanza baada ya kutangazwa rasmi, ten Hag alisema:
“Bayer04 ni moja ya klabu bora kabisa nchini Ujerumani na pia ni miongoni mwa timu za kiwango cha juu barani Ulaya. Klabu hii ina mazingira mazuri sana ya kufanya kazi, na mazungumzo niliyofanya na viongozi wake yamenivutia sana.”
Ten Hag anakabiliwa na changamoto kadhaa katika kibarua chake kipya. Kwanza, atalazimika kujenga kikosi kipya kutokana na kuondoka kwa baadhi ya wachezaji muhimu wa timu hiyo akiwemo Jonathan Tah, Jeremie Frimpong, na hasa Florian Wirtz ambaye alikuwa mhimili mkubwa wa mafanikio ya klabu hiyo. Kupoteza wachezaji hao kunahitaji uongozi wa kiufundi wenye maono ya kuleta mabadiliko ya haraka katika kikosi hicho.
Ingawa majukumu yanayomkabili ni magumu, Erik ten Hag anakuja na uzoefu mkubwa wa kimataifa. Kabla ya kuifundisha Manchester United, alihudumu kama kocha wa Ajax Amsterdam ambapo alishinda mataji matatu ya Eredivisie na kuifikisha timu hiyo hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2018-2019. Ufanisi huo ulimpa sifa kubwa kama kocha mwenye mbinu za kisasa na uwezo wa kukuza vipaji.
Aidha, huu si mara ya kwanza kwa ten Hag kufanya kazi nchini Ujerumani. Kati ya mwaka 2013 na 2015, alikuwa kocha mkuu wa kikosi cha pili cha Bayern Munich – Bayern Munich II – wakati huo akiwa chini ya usimamizi wa Pep Guardiola.
Akiwa na timu hiyo, aliweza kushinda taji la Regionalliga Bayern na aliwahi kufundisha wachezaji kama Mitchell Weiser, hatua iliyompatia uzoefu muhimu katika mazingira ya soka la Ujerumani.
Kwa sasa, mashabiki wa Bayer Leverkusen wanasubiri kuona mwelekeo mpya utakaochukuliwa na klabu hiyo chini ya usimamizi wa ten Hag. Licha ya kuondoka kwa nyota wake kadhaa, klabu hiyo bado ina historia ya kushindana katika ngazi ya juu na sasa inatazamiwa kujenga upya kikosi chake kwa malengo ya kuendelea kuwa miongoni mwa vilabu bora barani Ulaya.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Kevin De Bruyne Atajwa Kujiunga na Mabingwa wa Serie A Napoli
- Mac Allister Awindwa Kuziba Pengo la Modric Real Madrid
- Mbappé Ashinda Tuzo ya Mfungaji Bora Ulaya na La Liga kwa Mwaka 2024/25
- Simba Yapokewa Dar kwa Shangwe Kubwa Baada ya Mtanange Mkali Zanzibar
- Rs Berkane Yabeba Ubingwa Kombe la Shirikisho Afrika 2024/2025
- Ndoto ya Ubingwa Shirikisho ya Simba Yazimwa Baada ya Sare Amaan Complex
- Rais Mwinyi Aahidi Mamilioni Kwa Simba Wakishinda Kombe la Shirikisho
Leave a Reply