Fadlu Davids Afurahishwa na Ngome ya Ulinzi Simba
Simba SC imeendelea kudhihirisha ubora wake katika safu ya ulinzi, jambo ambalo limemfanya kocha mkuu, Fadlu Davids, kufurahia maendeleo makubwa ya timu yake, hususan eneo la ulinzi. Katika mechi za hivi karibuni, ngome ya Simba haijaruhusu bao, hali inayompa matumaini makubwa kuelekea mechi ngumu za mashindano ya ndani na kimataifa.
Ukuta Imara wa Simba
Simba imecheza mechi mbili za Ligi Kuu ya NBC bila kuruhusu bao lolote, na ilipokutana na Al Ahly Tripoli kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, timu hiyo ilifanikiwa pia kutoruhusu bao kwenye ardhi ya Libya.
Ingawa Simba iliruhusu bao moja tu kwenye Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC, kwa sasa beki Henock Inonga, aliyekuwa tegemeo msimu uliopita, haonekani kukumbukwa kutokana na uimara wa safu mpya ya ulinzi.
Mchezaji ambaye amekuwa kiungo muhimu katika mafanikio haya ya ulinzi ni Che Malone Fondoh, beki kutoka Cameroon. Katika mchezo dhidi ya Al Ahly Tripoli, Che Malone alionekana kuibuka kinara kwa kuzima mashambulizi mengi ya wapinzani, akifanikiwa kuharibu mashambulizi sita, likiwemo moja la penalti ambalo wapinzani walidhani wangestahili kupewa.
Wengine Walioko Ngome ya Simba
Mbali na Che Malone, beki mwingine aliyepata sifa kubwa ni Abdulrazack Hamza, ambaye anacheza kama pacha wa Malone. Katika mchezo dhidi ya Al Ahly Tripoli, Hamza alifanikiwa kuzuia mashambulizi matatu ya wapinzani na ameendelea kuwa chaguo muhimu kwenye safu ya ulinzi ya Simba, nafasi iliyomweka nje beki wa kigeni Chamou Karaboue.
Kipa mpya wa Simba, Moussa Camara, pamoja na mabeki wa pembeni Shomari Kapombe na nahodha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, nao walikuwa na mchango mkubwa katika kuzuia mashambulizi ya Al Ahly Tripoli. Camara alifanikiwa kuokoa krosi mbili muhimu ambazo kama zingepita, huenda Simba wangejikuta wakiruhusu bao.
Safu hii imara ya ulinzi ya Simba mara ya mwisho kuruhusu bao ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Yanga SC, ambao ndio timu pekee iliyofunga dhidi ya wachezaji hao wanne wa ulinzi. Mbele yao, kiungo mkabaji Deborah Fernandez Mavambo ameendelea kuwasaidia mabeki kwa kuziba mianya ya mashambulizi ya wapinzani.
Changamoto kwa Henock Inonga
Wakati Simba ikijivunia ngome yake imara, hali imekuwa tofauti kwa beki wa zamani wa Simba, Henock Inonga, ambaye kwa sasa anakipiga katika timu ya FAR Rabat ya Morocco. Inonga amekuwa akiruhusu mabao kwa kasi, ambapo timu yake imeruhusu mabao matatu ndani ya mechi tatu za mashindano msimu huu. Kwa upande mwingine, Simba wameruhusu bao moja tu kwenye mechi tano walizocheza msimu huu.
Kauli ya Fadlu Davids
Kocha Fadlu Davids, ameeleza kuwa anaridhishwa na kiwango cha safu ya ulinzi ya Simba. Akizungumza kuhusu mafanikio ya ngome ya ulinzi, alisema kuwa kuna maelewano mazuri kati ya wachezaji wa ulinzi, jambo ambalo limepelekea uimara wa ukuta wa timu hiyo.
“Mpaka sasa nadhani eneo la ulinzi limeimarika vizuri, ukiangalia inaonekana kuna maelewano mazuri kwa watu wanaocheza pale. Kadiri tunavyoendelea kupata mechi ngumu za mashindano, zinatusaidia kutuweka sawa zaidi,” alisema Fadlu.
Hata hivyo, Simba inakabiliwa na mtihani mgumu katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripoli, utakaopigwa Jumapili ya wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Baada ya sare ya 0-0 kwenye mchezo wa kwanza nchini Libya, Simba inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kusonga mbele. Hata hivyo, Fadlu alisisitiza umuhimu wa tahadhari.
“Matokeo ya 0-0 tukiwa tunarudi nyumbani yanatutaka kuwa makini zaidi ya ilivyokuwa mechi ya kwanza. Tukifanya makosa ya kuruhusu bao, hasa tukiwa bado hatujapata bao, itatuweka kwenye presha kubwa,” aliongeza Fadlu.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Zahera Aanza Tambo Baada ya Ushindi wa Kwanza wa Namungo Ligi Kuu
- Azam FC Yalenga Ushindi wa Kwanza Ligi Kuu Dhidi ya Simba
- Gamondi Apania Ushindi Mnono Mechi ya Marudiano Dhidi ya CBE
- CAF Yaagiza Uchunguzi Dhidi ya Vurugu Walizofanyiwa Simba Libya
- Ratiba ya Mechi za Leo 18 September 2024
- Kipa wa CBE Aeleza Hofu Yake Kuelekea Mchezo wa Pili Ligi ya Mabingwa, Amtaja Prince Dube
- Marefa Mechi za Simba na Yanga Klabu Bingwa Afrika
- Viingilio Mechi ya Yanga Vs CBE 21/09/2024
Weka Komenti