Guardiola Atangaza Kupumzika Ukocha Baada ya Mkataba Wa Man City Kuisha
London — Meneja wa Manchester City, Pep Guardiola, amefichua mpango wake wa kupumzika kutoka katika majukumu ya ukocha mara tu mkataba wake wa sasa na mabingwa hao wa England utakapomalizika. Ingawa hakufafanua ikiwa ataachana kabisa na ukocha, Guardiola alieleza bayana kuwa atachukua mapumziko ya muda usiojulikana baada ya kuhitimisha kipindi chake na klabu hiyo ifikapo Juni 2027.
Guardiola, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 54, alisaini mkataba wa nyongeza wa miaka miwili mwezi Novemba mwaka jana, hatua inayomuwezesha kuendelea kuinoa Manchester City hadi mwaka 2027. Hii inaifanya kuwa awamu yake ndefu zaidi ya ukocha katika klabu moja, akiwa ameiongoza City kwa kipindi cha miaka 11 kufikia mwisho wa mkataba huo, muda mrefu kuliko alivyodumu na Barcelona (miaka 4) na Bayern Munich (miaka 3).
Katika mahojiano maalum na ESPN, Guardiola alisema: “Baada ya mkataba wangu na City, nitasimama. Nina uhakika sijui kama nitastaafu, lakini nitapumzika.” Kauli hiyo imetafsiriwa na wengi kuwa huenda Pep akawa anakaribia kufunga ukurasa wa mafanikio wake wa kipekee kama kocha katika soka la kulipwa, angalau kwa muda.
Hata hivyo, Guardiola alisisitiza kuwa hajatangaza kuondoka mara moja wala mwisho wa msimu huu. Katika maelezo yake kwa Sky Sports, alifafanua: “Sikusema naondoka sasa au mwisho wa msimu au mwisho wa mkataba. Nilisema nikimaliza muda wangu hapa iwe mwaka mmoja, miwili, mitatu, minne, mitano — nitapumzika.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bado kuna muda wa Guardiola kuendelea kuiongoza Manchester City, lakini pia ni wazi kuwa hatua hiyo ya kupumzika tayari imewekwa akilini mwake, kama sehemu ya mpango wa baadaye.
Katika kipindi chake akiwa meneja wa Manchester City, Guardiola ameiletea klabu hiyo mafanikio makubwa, yakiwemo mataji sita ya Ligi Kuu ya England (EPL) kati ya tisa yaliyogombewa chini ya uongozi wake. Aidha, mwaka 2023, aliiongoza timu hiyo kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu — mafanikio yaliyokamilisha ubabe wa City katika soka la Ulaya na ndani ya Uingereza.
Kabla ya kujiunga na Manchester City, Guardiola alijizolea sifa nyingi akiwa na Barcelona, ambapo alishinda kila taji kubwa la klabu, ikiwemo UEFA Champions League mara mbili. Akiwa Bayern Munich, aliendeleza mafanikio kwa kutwaa mataji ya Bundesliga kila msimu katika kipindi cha miaka mitatu.
Taswira ya Baadaye Bila Guardiola
Uamuzi wa Guardiola kuchukua mapumziko, iwapo utatekelezwa kama ulivyotangazwa, unaacha maswali mengi kuhusu mustakabali wa Manchester City baada ya mwaka 2027.
Hadi sasa, haijulikani nani atarithi mikoba yake, au kama Pep ataamua kurejea uwanjani baada ya mapumziko hayo. Kwa mashabiki na wachambuzi wa soka, kauli hii ni onyo la mwanzo kuhusu kuondoka kwa mmoja wa makocha bora wa kizazi hiki.
Katika tafakari yake kuhusu namna anavyotaka kukumbukwa, Guardiola alisema: “Sidhani kama tunapaswa kuishi kufikiria kama tutakumbukwa. Nataka watu wanikumbuke wanavyotaka. Makocha wote wanataka kushinda ili tuwe na kazi ya kukumbukwa, lakini ninaamini kwamba mashabiki wa Barcelona, Bayern Munich na City wanafurahi kuona timu zangu zikicheza.”
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ratiba ya Kombe la Muungano 2025
- JKU vs Yanga Leo 01/05/2025 Saa Ngapi?
- Ratiba ya Fainali Kombe La Shirikisho Afrika CAF 2024/2025
- Kikosi cha Yanga vs Zimamoto Leo 29/04/2025
- Zimamoto VS Yanga Leo 29/04/2025 Saa Ngapi?
- Matokeo ya Zimamoto VS Yanga Leo 29/04/2025
- Simba SC Yatinga Fainali Kombe la Shirikisho Afrika Baada ya Sare na Stellenbosch
Leave a Reply