Kennedy Musonda Atimkia Israel Baada ya Kumaliza Mkataba na Yanga

Kennedy Musonda Atimkia Israel Baada ya Kumaliza Mkataba na Yanga

SIKU moja tu baada ya kuwaaga rasmi mashabiki wa Yanga SC na kutamatisha safari yake ya mafanikio ndani ya klabu hiyo ya kihistoria, mshambuliaji hatari kutoka Zambia, Kennedy Musonda, ametimkia Israel ambapo amejiunga na klabu ya Hapoel Ramat Gan inayoshiriki Ligi Daraja la Pili maarufu kama Liga Leumit.

Musonda ameandika historia ndani ya Yanga SC kwa kipindi cha miaka miwili na nusu alichokaa nchini Tanzania, akiondoka akiwa ameacha alama isiyofutika kwa Wananchi. Katika muda huo mfupi lakini wa mafanikio, amefanikiwa kufunga mabao 34 na kutoa asisti 13, huku akinyakua mataji matatu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, matatu ya Kombe la FA, na ngao za jamii mbili, mafanikio yanayodhihirisha kiwango chake cha juu na mchango wake mkubwa kwa timu.

Kennedy Musonda Atimkia Israel Baada ya Kumaliza Mkataba na Yanga

Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti, Musonda alieleza kuwa anaondoka Yanga akiwa na furaha na fahari ya mafanikio aliyoyapata, ingawa haikuwa kazi rahisi. Amedokeza kuwa licha ya changamoto na kupanda na kushuka, alifanikiwa kuweka alama yake na sasa anaangalia mbele kuandika historia nyingine mpya akiwa nje ya mipaka ya Tanzania.

“Haijawa rahisi kuhitimisha maisha yangu ndani ya Yanga licha ya panda shuka, lakini nafurahi nimefanikiwa kutwaa mataji na nimeacha kitu cha kuzungumzwa ndani ya timu hiyo. Sasa ni wakati wangu kwenda sehemu nyingine,” alisema Musonda.

Nyota huyo ambaye pia ni tegemeo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zambia, amefichua kuwa tayari amejiunga na Hapoel Ramat Gan ya Israel na atakuwa sehemu ya kikosi hicho msimu ujao wa mashindano. Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi muda wa mkataba wake akisema ataweka bayana taarifa hizo katika siku zijazo.

“Ni kweli naenda Israel. Suala la mkataba wa muda gani nitakufahamisha sio sasa, kikubwa ni kwamba nimeshapata timu mpya na nitakuwa Israel msimu ujao,” aliongeza kwa kujiamini.

Kennedy Musonda amesisitiza kuwa kuondoka kwake Yanga si mwisho wa mafanikio yake, bali ni mwanzo wa ukurasa mpya kwenye maisha yake ya soka. Amesema alipojiunga na Yanga hakutegemea kufanya makubwa, lakini leo anaondoka akiwa shujaa – jambo linalompa motisha kuwa anaweza kufanikisha makubwa zaidi pia akiwa Israel.

“Safari moja huanzisha nyingine. Nilipofika Yanga sikuwa na matarajio makubwa, lakini nimefanikiwa. Naam, naamini hata huko Israel nitaandika historia nyingine nzuri,” alisema kwa matumaini makubwa.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Tetesi Za Usajili Yanga Leo 2025/2026
  2. Tetesi Za Usajili Simba Leo 2025/2026
  3. PSG Yatinga Nusu Fainali Baada ya Kuichapa Bayern Munich 2-0 Marekani
  4. Azam FC Yamtambulisha Florent Ibenge Kama Kocha Mkuu Mpya
  5. Namungo Yampigia Hesabu Ally Salim Kama Mrithi wa Beno Kakolanya
  6. Wallace Karia Abaki Bila Mpinzani Baada ya Wagombea Watano Kuenguliwa
  7. Ibenge Atua Tanzania Kujiunga Rasmi na Azam FC kwa Msimu wa 2025/26
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo