Kevin De Bruyne Atajwa Kujiunga na Mabingwa wa Serie A Napoli
Kiungo wa kati wa Manchester City, Kevin De Bruyne, mwenye umri wa miaka 33, anaripotiwa kuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wake kuelekea mabingwa wa Serie A, Napoli, ndani ya kipindi kifupi kijacho. Awali, nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji alikuwa akihusishwa na vilabu vya Saudi Arabia na Marekani, ambako vilikuwepo vilabu vilivyokuwa tayari kutoa ofa kubwa ili kumnasa. Hata hivyo, De Bruyne alikataa ofa hizo, akisisitiza kuwa bado ana uwezo na nia ya kuendelea kucheza soka la ushindani barani Ulaya.
Kwa mujibu wa taarifa mpya zilizotolewa na viongozi wa Napoli, hatua ya kumleta De Bruyne inakaribia kutangazwa rasmi kabla ya kuanza kwa dirisha la usajili la majira ya kiangazi mnamo Juni 1. Rais wa klabu hiyo, Aurelio De Laurentiis, amethibitisha kuwa mazungumzo yamefikia hatua ya juu zaidi, na uhamisho huo unaweza kukamilika hivi karibuni.
“Ninaamini kweli kwamba Kevin De Bruyne sasa atajiunga nasi,” alisema De Laurentiis kupitia mahojiano na Rai. “Nimeambiwa tayari amenunua nyumba nzuri… Nilizungumza naye, mkewe, na mtoto wake asubuhi ya leo. Ilikuwa ni mazungumzo mazuri sana,” aliongeza kwa hisia.*
Hata hivyo, licha ya hali hiyo kuonekana kuwa nzuri, De Laurentiis alitoa tahadhari kuwa bado ni muhimu kuwa waangalifu hadi mikataba itakaposainiwa rasmi.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa michezo wa Napoli, Giovanni Manna, aliongeza uzito wa taarifa hizi kwa kusema kuwa klabu hiyo imekuwa ikifanya kazi ya ndani kwa miezi kadhaa ili kuhakikisha kuwa De Bruyne anajiunga nao.
“Tumekuwa tukifanyia kazi dili la Kevin De Bruyne kwa miezi mingi… na sasa tunaelekea ukingoni mwa safari hii,” alisema Manna kwa ujasiri.
Kevin De Bruyne amekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Manchester City kwa kipindi cha zaidi ya muongo mmoja, akifanikiwa kushinda jumla ya mataji 18, yakiwemo mataji sita ya Ligi Kuu ya England (EPL) pamoja na treble ya kihistoria mwaka 2023.
Katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Fulham, alipewa heshima ya kipekee ya kuagwa na mashabiki na wachezaji wenzake, tukio lililozua hisia kubwa ndani ya uwanja wa Etihad.
Iwapo uhamisho huu utakamilika, De Bruyne ataungana na wachezaji wawili mashuhuri waliowahi kung’ara England — Scott McTominay, kiungo wa zamani wa Manchester United, na mshambuliaji wa kimataifa wa Ubelgiji Romelu Lukaku — wanaotarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Napoli msimu ujao.
Napoli walifanikiwa kutwaa ubingwa wao wa nne wa Serie A baada ya kuwashinda Cagliari kwa mabao 2-0, hatua ambayo imedhihirisha nia ya klabu hiyo kuimarika zaidi kwa kujenga kikosi cha ushindani katika ngazi ya bara. Ushindi huo unaweza kuwa kichocheo kikubwa kwa De Bruyne kuhamia rasmi katika klabu hiyo yenye malengo makubwa.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Mac Allister Awindwa Kuziba Pengo la Modric Real Madrid
- Mbappé Ashinda Tuzo ya Mfungaji Bora Ulaya na La Liga kwa Mwaka 2024/25
- Simba Yapokewa Dar kwa Shangwe Kubwa Baada ya Mtanange Mkali Zanzibar
- Rs Berkane Yabeba Ubingwa Kombe la Shirikisho Afrika 2024/2025
- Ndoto ya Ubingwa Shirikisho ya Simba Yazimwa Baada ya Sare Amaan Complex
- Simba vs Berkane Leo 25/05/2025 Saa Ngapi?
- KIKOSI CHA SIMBA VS BERKANE LEO 25/05/2025 – FAINALI YA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA
Leave a Reply