Kikosi cha Tanzania Taifa Stars vs Morocco Leo 04/01/2026
Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Tanzania, Taifa Stars, leo itashuka katika Uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat kuivaa Morocco katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Mchezo huu unaotarajiwa kuchezwa leo tarehe 04/01/2026, unaweka Taifa Stars katika jukwaa kubwa zaidi la soka la Afrika, ukiwa ni mtihani wa kihistoria dhidi ya wenyeji wa mashindano hayo.
Kwa mara ya kwanza katika historia ya ushiriki wake AFCON, Tanzania imefanikiwa kufuzu kushiriki katika hatua ya mtoano, jambo linaloipa mechi ya leo uzito mkubwa kitaifa na kikanda. Mashabiki wa soka nchini wanaelekeza macho Rabat, wakisubiri kuona kitakachotokea katika pambano hili gumu dhidi ya moja ya mataifa yenye rekodi bora barani Afrika.
Safari ya Taifa Stars Kufikia Hatua ya 16 Bora
Taifa Stars imeingia hatua hii baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu ya Kundi C lililokuwa na Nigeria, Tunisia na Uganda. Kupitia mfumo wa timu bora zilizomaliza nafasi ya tatu, Tanzania iliungana na Benin, Sudan na Msumbiji kupata tiketi ya kuendelea.
Katika mechi za makundi, Stars ilikusanya sare mbili na kupoteza mchezo mmoja, lakini uimara wa safu ya ulinzi na nidhamu ya kiufundi ulimwezesha kocha Miguel Gamondi kuiweka timu kwenye ushindani hadi dakika ya mwisho. Mfumo wa 5-4-1 uliotumika hususan katika sare ya 1-1 dhidi ya Tunisia uliipa Stars sifa ya kuwa timu ngumu kufungika.
Morocco: Wenyeji na Wagombea wa Ubingwa
Kwa upande wa Morocco, Atlas Lions waliingia hatua ya 16 bora wakiwa vinara wa Kundi A baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare moja, wakikusanya jumla ya pointi saba. Timu hiyo iliruhusu bao moja pekee katika hatua ya makundi, ikionyesha uimara mkubwa wa safu yake ya ulinzi. Morocco inabeba presha kubwa ya mashabiki wake ikizingatiwa kuwa ni wenyeji wa mashindano, huku matarajio yakiwa ni kutinga hatua za juu na hatimaye kulitwaa taji la AFCON kwa mara ya pili tangu walipofanya hivyo mwaka 1976.
Licha ya matokeo mazuri, kocha Walid Regragui amekuwa akikosolewa na baadhi ya wadau kuhusu mbinu zake, jambo linaloifanya mechi ya leo kuwa mtihani wa kimkakati pia.
Kikosi cha Tanzania Taifa Stars vs Morocco Leo 04/01/2026
Hapa tutakuletea kikosi rasmi cha Tanzania Taifa Stars kitakachoanza leo dhidi ya Morocco katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 itakayochezwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat.
Taifa Stars inatarajiwa kushuka uwanjani ikiwa na mchanganyiko wa wachezaji wenye uzoefu na vipaji vilivyoonyesha kiwango kizuri katika hatua ya makundi. Kikosi hicho kinajumuisha baadhi ya wachezaji waliowahi kuifunga Morocco mwaka 2013 akiwemo Mbwana Samatta, pamoja na nyota waliotoa mchango muhimu katika safari ya kufuzu hatua hii kama Simon Msuva, Feisal Salum na Shomari Kapombe.
Kocha Miguel Gamondi anatarajiwa kuendelea na falsafa yake ya nidhamu ya kiufundi, akitumia mfumo ulioipa timu uimara wa ulinzi katika mechi zilizopita, huku lengo likiwa ni kuhimili presha ya wenyeji na kutumia nafasi chache zitakazopatikana mbele ya lango la Morocco.
Kikosi kamili cha kuanza kitawekwa rasmi na benchi la ufundi muda mfupi kabla ya mchezo kuanza, lakini matarajio ya mashabiki wa soka nchini ni kuona Taifa Stars ikishuka uwanjani kwa ari, umoja na dhamira ya kupigania taifa katika moja ya mechi kubwa zaidi katika historia ya soka la Tanzania.
Kauli za Ndani ya Kambi ya Taifa Stars
Kiungo wa Taifa Stars, Feisal Salum (Fei Toto), amesema kikosi kipo huru kisaikolojia na kinaiheshimu Morocco bila kuogopa ukubwa wa jina lao.
“Tunajua Morocco ni timu kubwa yenye wachezaji wa kiwango cha juu, lakini hatujaenda kinyonge. Tutapambana kutafuta matokeo,” alisema Fei Toto.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, pia alisisitiza kuwa timu haina presha na inaingia uwanjani kwa morali ya kupigania taifa.
“Wachezaji wako salama na tumeridhishwa na kiwango chao kwenye mechi zilizopita. Tunajua mchezo ni mgumu, lakini wamejipanga kulipigania taifa,” alisema Karia.
Mapendekezo ya Mhariri:










Leave a Reply