Kikosi cha Tanzania vs Nigeria Leo 23/12/2025 AFCON
Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo kinashuka dimbani kuwakabili Super Eagles ya Nigeria katika mchezo wa kwanza wa Kundi C la AFCON 2025 unaochezwa Morocco, mechi ambayo imebeba uzito mkubwa kwa mustakabali wa safari ya Stars kwenye mashindano hayo. Mchezo huo unapigwa usiku wa leo Jumanne kuanzia saa 2:30 kwa saa za Tanzania katika Uwanja wa Fez, jijini Fez, ikiwa ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana kwenye fainali za AFCON baada ya takribani miaka 45.
Presha ya Kundi la Kifo
Tangu kutangazwa kwa makundi ya AFCON 2025, mashabiki wengi wa soka nchini wamekuwa na hofu wakieleza kuwa Taifa Stars imepangwa kwenye “kundi la kifo” likiwa na Nigeria, Tunisia na Uganda.
Hata hivyo, kambi ya Stars chini ya Kocha Mkuu Miguel Gamondi imeweka wazi dhamira ya kuondoa dhana ya unyonge. Kocha Gamondi na wachezaji wake wameripotiwa kuwa na kauli moja kuelekea mchezo huu wa leo, wakisisitiza kuwa lengo ni kupambana na kuandika historia mpya. Baada ya siku 699 bila kucheza mechi ya AFCON, Stars inarejea jukwaa hilo kubwa la Afrika ikitafuta mwanzo mzuri.
Historia ya Mikutano Tanzania vs Nigeria
Kwa mara ya kwanza Tanzania na Nigeria zilikutana kwenye AFCON mwaka 1980, mashindano yaliyofanyika Nigeria. Katika mchezo huo wa ufunguzi Machi 8, 1980, Nigeria iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania mjini Lagos, kabla ya baadaye kubeba ubingwa wao wa kwanza wa AFCON.
Kwa jumla, timu hizi zimekutana mara saba katika mashindano tofauti. Nigeria haijawahi kupoteza, ikishinda mechi nne na kutoka sare tatu, ikifunga mabao 11 na kuruhusu mabao matatu. Kwa upande wa Tanzania, imeambulia sare tatu na kupoteza nne, ikifunga mabao matatu pekee.
Mikutano ya hivi karibuni ilitokea katika mechi za kufuzu AFCON 2017, ambapo Tanzania ilipata sare ya 0-0 Dar es Salaam Septemba 5, 2015, kabla ya Nigeria kushinda 1-0 mjini Uyo Septemba 3, 2016.
Mastaa wa Kutazamwa
Katika kikosi cha Nigeria, macho yatakuwa kwa washambuliaji hatari Ademola Lookman na Victor Osimhen, ambao walikuwa wafungaji bora wa timu hiyo katika mechi za kufuzu wakiwa na mabao mawili kila mmoja. Pia, Alex Iwobi na Samuel Chukwueze wanaendelea kutajwa kuwa tishio kubwa katika safu ya ushambuliaji.
Kwa upande wa Kikosi cha Tanzania vs Nigeria Leo 23/12/2025 AFCON, Stars itategemea ubora wa Simon Msuva na Feisal Salum, waliokuwa wafungaji bora wa timu hiyo katika kufuzu wakiwa na mabao mawili kila mmoja. Nahodha Mbwana Samatta pia anatarajiwa kuwa mhimili muhimu katika uongozi na uzoefu uwanjani.
Kikosi cha Tanzania vs Nigeria Leo 23/12/2025 AFCON
Hapa tutakuletea kikosi rasmi cha timu ya Taifa ya Tanzania kitakachoanza dhidi ya Nigeria leo, katika mchezo wa Kundi C wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 unaochezwa jijini Fez, Morocco.
Kikosi hicho kinatarajiwa kuongozwa na nahodha Mbwana Samatta, kikihusisha wachezaji waliokuwa nguzo muhimu katika mechi za kufuzu, akiwemo Simon Msuva na Feisal Salum, ambao walionyesha mchango mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji.

Rekodi ya Taifa Stars Katika Michuano ya AFCON
Nigeria inashiriki AFCON kwa mara ya 21, ikiwa imetwaa ubingwa mara tatu (1980, 1994 na 2013). Rekodi hiyo inaipa hadhi kubwa dhidi ya Stars, ambayo katika ushiriki wake wa mwisho mara tatu haijawahi kushinda mechi yoyote ya AFCON.
Mwaka 1980 Stars ilimaliza na pointi moja, mwaka 2019 Misri ikamaliza bila pointi, huku AFCON 2023 Ivory Coast ikikusanya pointi mbili pekee. Mara zote hizo, Tanzania ilimaliza mkiani mwa kundi. Ushindi leo ungeiweka Stars kwenye rekodi mpya ya kupata pointi tatu za kwanza katika historia yake ya AFCON.
Changamoto Kubwa Dhidi ya Nigeria
Nigeria ina rekodi imara ya mashindano haya, ikiwa imefika angalau nusu fainali mara 13 tangu mwaka 1988. Pia, haijapoteza mechi ya ufunguzi katika AFCON tatu zilizopita na imepoteza mechi moja tu ya hatua ya makundi katika mashindano 14 ya mwisho.
Kwa Tanzania, changamoto kubwa imekuwa kufunga mabao kwenye mechi za ufunguzi. Tangu bao lililofungwa AFCON 1980 dhidi ya Nigeria, Stars haijawahi tena kufunga bao kwenye mechi ya kwanza ya makundi, ikishuhudiwa vipigo dhidi ya Senegal mwaka 2019 na Morocco mwaka 2023.
Mapendekezo ya Mhariri:









Leave a Reply