Klabu ya Simba Sc Imetangaza Kuachana na Saido Ntibazonkiza
Mashabiki wa Simba wamekua na hisia tofauti kufuatia tangazo rasmi kutoka klabu ya Simba SC kuhusu kuachana na mshambuliaji wao mahiri, Saido Ntibazonkiza. Mchezaji huyu raia wa Burundi, ambaye alijiunga na Wekundu wa Msimbazi katika dirisha dogo la usajili mwaka 2023 akitokea Geita Gold, ameweza kufanya mambo makubwa ndani ya muda mfupi aliodumu klabuni hapo.
Klabu ya Simba Sc Imetangaza Kuachana na Saido Ntibazonkiza
Ntibanzonkiza ameichezea Simba kwa muda wa mwaka mmoja na nusu pekee, lakini ndani ya kipindi hiki kifupi, Saido ameweza kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi katika kikosi cha Simba. Ubora wake wa kupandisha mashambulizi na kupachika mabao uwanjani ulimfanya kuwa mfungaji bora wa timu katika misimu yote miwili aliyoitumikia, akitia kimiani mabao mengi muhimu yaliyoisaidia Simba kushinda mechi mbalimbali na kumaliza katika nafasi za juu za msimamo wa ligi.
Katika msimu wa 2022/23 Ntibazonkiza alifunga jumla ya mabao 17 katika Ligi Kuu ya NBC, akishiriki tuzo ya mfungaji bora na Fiston Mayele wa Yanga SC. Lakini uwezo wake haukuishia hapo; kiungo huyu mshambuliaji pia alitajwa kuwa kiungo bora wa msimu huo, akionyesha ubora wake katika kuchezesha timu na kuunda nafasi za kufunga.
Pia katika msimu wa 2023/2024 Saido ameisaidia klabu ya Simba kushinda ngao ya jamii huku akifunga mabao 11 na assist 3 kwa msimu wa 23/24. Idadi hii ya magoli inamfanya Saido kuwa ndio mfungaji bora wa klabu ya simba kwa msimu huu uliomalizika.
Uongozi wa klabu ya Simba SC, umemtakia kila la kheri Ntibazonkiza katika maisha yake mapya ya soka nje ya klabu hiyo. Katika taarifa yao, uongozi wa Simba umebainisha kuwa kuondoka kwa Ntibazonkiza ni sehemu ya mipango yao ya kufanya maboresho makubwa katika kikosi chao kwa msimu ujao wa 2024/25.
Mapendekezo Ya Muhariri:
Weka Komenti