Kocha Gamondi Asaini Kukiongoza Kikosi cha Taifa Stars Mpaka 2028

RASMI: Kocha Gamondi Asaini Kukiongoza Kikosi cha Taifa Stars Mpaka 2028

DAR ES SALAAM, Tanzania – Mapinduzi ya soka nchini Tanzania yamechukua sura mpya baada ya Serikali kuthibitisha rasmi kuwa mtaalamu wa ufundi, Miguel Gamondi, amekabidhiwa rungu la kuinoa timu ya Taifa, Taifa Stars, kwa mkataba wa miaka miwili.

Akizungumza kwa kujiamini mbele ya vyombo vya habari, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, ameweka wazi kuwa hatua hiyo ni sehemu ya uwekezaji mkubwa wa kimkakati.

“Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Paul Makonda, ameweka wazi kuwa, Kocha Miguel Gamondi amesaini rasmi mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha timu ya Taifa ya soka ya Tanzania (Taifa Stars). Kwa sasa timu ni mali ya Gamondi,” alisema Mhe. Makonda.

Kocha Gamondi Asaini Kukiongoza Kikosi cha Taifa Stars Mpaka 2028

Kutoka ‘Ukaimu’ Mpaka Kupewa Dhamana Kamili

Gamondi, ambaye awali alikuwa akihudumu kama Kaimu Kocha Mkuu baada ya kuondoka kwa Hemed Suleiman ‘Morocco’, amethibitisha ubora wake kwa vitendo. Chini ya uongozi wake wa muda, aliiongoza Taifa Stars kutinga hatua ya 16 Bora ya AFCON 2025 nchini Morocco—safari iliyoishia mikononi mwa wenyeji Morocco katika mazingira ya kitatanishi.

Mkataba huu mpya unatazamwa kama daraja la kuelekea AFCON 2027, ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji wa pamoja na nchi za Kenya na Uganda. Lengo kuu ni kuhakikisha bendera ya taifa inapeperushwa kwa kishindo katika ardhi ya nyumbani.

Ahadi ya Gamondi: Furaha Zaidi kwa Watanzania

Baada ya kuweka saini mkataba huo utakaomuweka nchini mpaka mwaka 2028, Miguel Gamondi hakuchelewa kutoa cheche zake. Kocha huyo ameahidi kiwango cha soka ambacho kitazidi mafanikio ya kutinga 16 bora yaliyopatikana hivi karibuni.

“Ni jukumu langu kuhakikisha timu inafanya vizuri na kuleta sifa kwa Tanzania na mashabiki kufurahia. Nipo tayari kufanya kazi hiyo. Nashukuru mashabiki kwa kuniunga mkono,” alisema Gamondi, akisisitiza utayari wake wa kujenga kikosi imara.

Mikakati ya Serikali na Maagizo kwa Wadau

Waziri Makonda amebainisha kuwa Serikali imemwaga fedha ili kumwezesha Gamondi kuandaa programu za muda mrefu (long-term programs) ambazo zitasaidia kukuza vipaji vya wachezaji wa ndani.

Aidha, Waziri alitumia fursa hiyo kutoa maelekezo mazito kwa mamlaka za michezo:

Baraza la Michezo Tanzania (BMT): Kutakiwa kufanya tathmini ya kina kwanini mashirikisho mengine hayaleti mataji kama soka.

Mchezo wa Ngumi: Makonda alieleza hamu yake ya kuona mabondia wakubwa duniani kama Mike Tyson wakialikwa nchini ili kuimarisha soka la ngumi na kutengeneza ajira kwa vijana.

Mchakato wa Klabu ya Simba: Msajili wa Vyama vya Michezo, Abel Ngilangwa, ametakiwa kukamilisha mchakato wa umiliki wa klabu ya Simba ndani ya mwezi huu kwa kufuata sheria na kanuni ili kuondoa mkwamo wa kiuongozi.

Pongezi kwa Klabu za Kimataifa

Katika hatua nyingine, Mhe. Makonda alizipongeza klabu za Simba, Yanga, Azam na Singida Black Stars kwa kufika hatua ya makundi ya michuano ya CAF msimu huu. Licha ya klabu hizo kutopenya kwenda robo fainali, Waziri amezitaka kujipanga vyema msimu ujao ili kufika hatua ya fainali na kuleta kombe nchini.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Msimamo Kundi la Yanga Klabu Bingwa 2025/2026
  2. Kikosi cha Yanga VS JS Kabylie Leo 15/02/2026
  3. Msimamo wa Kundi la Azam Kombe la Shirikisho CAF 2025/2026
  4. Simba SC Yaichapa Stade Malien Nyumbani na Kuvunja Ukame wa Ushindi CAF
  5. Viingilio vya Mechi ya Simba vs Stade Malien 14/02/2026
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo