Matokeo Kidato Cha Sita 2024 Yatangazwa Rasmi: Ufaulu Wafikia Asilimia 96.8
Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2024. Matokeo hayo yanaonyesha ongezeko la ufaulu wa asilimia 96.84, huku watahiniwa 24 wakifutiwa matokeo yao kutokana na udanganyifu.
Udanganyifu na Hatua Zilizochukuliwa
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed, alieleza kuwa udanganyifu umeendelea kudhibitiwa, ambapo watahiniwa 24 walibainika kuingia na simu, notisi, na kusaidiana kufanya mitihani. Watahiniwa 22 kati ya hao walikuwa ni wa kidato cha sita, huku mmoja akiwa ni wa mtihani wa ualimu daraja A na mmoja wa stashahada ya ualimu.
Takwimu za Jumla kuhusu Mtihani wa Kidato Cha Sita 2024
Jumla ya watahiniwa 113,536 walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha sita, ikiwa ni wasichana 50,614 na wavulana 62,922. Kati ya watahiniwa hao, 104,454 walikuwa ni wa shule na 9,082 ni wa kujitegemea. Watahiniwa 103,812 sawa na asilimia 99.39 walifanya mtihani huo, huku asilimia 0.61 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali.
Ufaulu wa Jumla
Watahiniwa wa shule waliofaulu ni 103,252 sawa na asilimia 99.92 ya watahiniwa wenye matokeo. Wasichana waliofaulu ni 46,615 sawa na asilimia 99.93 na wavulana ni 56,637 sawa na asilimia 99.91. Watahiniwa walioshindwa mtihani ni 84 sawa na asilimia 0.08.
Masomo yote yanaonyesha ufaulu wa kati ya asilimia 96.84 hadi 100, isipokuwa somo la Basic Applied Mathematics (BAM) ambalo lina ufaulu wa asilimia 77.55. Hata hivyo, ufaulu wa BAM umeongezeka kwa asilimia 9.02 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Watahiniwa wengi wamepata madaraja mazuri ya I-III ambapo asilimia 99.40 wamepata ufaulu mzuri. Idadi kubwa ya watahiniwa wamepata daraja la I na II ambapo daraja la I ni asilimia 46.32 na daraja la II ni asilimia 40.99. Hii inaonyesha ongezeko la ubora wa ufaulu kwa asilimia 0.10 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Matokeo ya Ualimu
Jumla ya watahiniwa 7,944 sawa na asilimia 99.81 ya watahiniwa 7,959 wenye matokeo ya mtihani wa Ualimu Daraja la A mwaka 2024 wamefaulu. Wanawake ni 4,384 sawa na asilimia 99.77 na Wanaume ni 3,560 sawa na asilimia 99.86. Watahiniwa 4,494 sawa na asilimia 56.46 wamepata ufaulu wa daraja la tatu ‘Pass’.
Baadhi ya wananchi wamepongeza matokeo hayo, wakisema kuwa ufaulu umeendelea kuongezeka. Hata hivyo, wamesisitiza umuhimu wa kuboresha elimu kwa vitendo ili kuzalisha wataalamu watakaoweza kushindana katika sekta mbalimbali za kibunifu na za kisayansi.
Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2024 yanaonyesha maendeleo makubwa katika sekta ya elimu. Hata hivyo, juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha elimu inakuwa ya vitendo na yenye ushindani wa kimataifa. Serikali na wadau mbalimbali wanapaswa kushirikiana kuboresha elimu ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Angalia Matokeo Yako Kupitia > Matokeo ya Kidato cha Sita 2024 (NECTA Form Six Results 2024)
Weka Komenti