Matokeo ya Kidato cha Nne 2025/2026 (NECTA Form Four Results)
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limetangaza rasmi Matokeo ya Kidato cha Nne 2025/2026, yakihusisha mtihani wa kitaifa wa Certificate of Secondary Education Examination (CSEE) uliofanyika kuanzia Novemba 17 hadi Desemba 05, 2025.
Matokeo hayo yametangazwa leo, Jumamosi Januari 31, 2026, na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Profesa Said Mohammed, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Profesa Said Mohammed, jumla ya watahiniwa 569,883 walifanya mtihani huo wakiwa wamesajiliwa katika shule 5,864 nchini kote, huku watahiniwa wa kujitegemea wakiwa 25,927 waliosajiliwa katika vituo 813.
Taarifa ya awali ya NECTA ya Novemba 16, 2025, ilieleza kuwa idadi ya watahiniwa wa mwaka 2025 imeongezeka kwa asilimia 7.67 ikilinganishwa na mwaka 2024. Kati ya watahiniwa wa shule 569,914 waliosajiliwa, wavulana walikuwa 266,024 sawa na asilimia 47, huku wasichana wakiwa 303,859 sawa na asilimia 53.
Mahudhurio ya watahiniwa katika mtihani yalifikia asilimia 97.5, sawa na wanafunzi 555,606 waliohudhuria mtihani kikamilifu.
Kwa upande wa ufaulu, takwimu zinaonesha kuwa matokeo ya mwaka 2025 yameimarika, ambapo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.61 na kufikia asilimia 94.98. Jumla ya watahiniwa 526,620 wamefaulu kwa kupata daraja la I, II, III na IV.
Aidha, ufaulu wa watahiniwa waliopata daraja la kwanza hadi la tatu umeongezeka, ambapo wanafunzi 255,404 wamepata daraja hizo, sawa na asilimia 46.1 ya watahiniwa wote waliofaulu.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo, Profesa Said Mohammed alisema:
“Matokeo ya mwaka huu yanaonesha mwenendo mzuri wa kitaaluma, hasa katika ongezeko la ufaulu wa jumla na idadi ya wanafunzi waliopata daraja za juu, jambo linaloashiria kuimarika kwa ubora wa elimu ya sekondari nchini.”
NECTA imewataka wanafunzi na wazazi kuendelea kutumia njia rasmi za baraza hilo kupata matokeo, ikiwemo tovuti ya NECTA na mifumo ya kidijitali iliyotangazwa, ili kuepuka taarifa zisizo sahihi au upotoshaji wa matokeo.
Jinsi ya Kuangalia Matokeo ya Kidato cha Nne 2025/2026 (NECTA Form Four Results)
Kama wewe ni miongoni mwa maelfu ya wanafunzi waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne 2025, au mzazi au mlezi wa mhitimu wa Kidato cha Nne, na ungependa kujua jinsi ya kuangalia Matokeo ya Kidato cha Nne 2025/2026 mara tu yatakapotangazwa rasmi na NECTA, basi hapa tumekuletea muongozo wa kina kukujuza namna unavyoweza kuangalia matokeo kwa urahisi zaidi.
Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) hutumia mfumo wa mtandaoni kutangaza matokeo ya mitihani yote ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na mtihani wa CSEE. Mfumo huu ni salama, rahisi kutumia, na unapatikana kwa wananchi wote wenye kifaa chenye intaneti.
Ili Kuangalia Matokeo ya Kidato cha Nne 2025 Mtangaoni Futa Hatua Zifuatazo
Baada ya matokeo kutangazwa rasmi, watahiniwa na wadau wa elimu wanatakiwa kutumia tovuti rasmi ya NECTA pekee ili kupata taarifa sahihi. Zifuatazo ni hatua rasmi za kufuata wakati wa kuangalia Matokeo ya Kidato cha Nne 2025/2026:
- Tembelea tovuti rasmi ya NECTA kwa kuandika anwani ya www.necta.go.tz
kwenye kivinjari cha simu au kompyuta. - Fungua sehemu ya “Results” au “Matokeo” iliyopo kwenye menyu kuu ya tovuti.
- Chagua mtihani wa CSEE, unaojulikana kama mtihani wa Kidato cha Nne.
- Bofya linki ya Matokeo ya Kidato cha Nne 2025/2026 mara itakapowekwa wazi.
- Tafuta matokeo kwa kutumia jina la shule au namba ya mtihani (Index Number) ya mhitimu.
- Angalia, pakua, au chapisha matokeo kwa matumizi ya kumbukumbu au hatua zinazofuata za kitaaluma.
Angalia Hapa Matokeo ya Kidato cha Nne 2025
Video ya Mwongozo wa Kuangalia Matokeo ya Kidato cha Nne Mtandaoni
Ili kusaidia uelewa wa mchakato wa kuangalia matokeo, video ifuatayo imeandaliwa kama nyenzo ya elimu inayoelezea hatua kwa hatua utaratibu wa kuangalia Matokeo ya Kidato cha Nne kupitia tovuti rasmi ya NECTA:
Malengo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE)
Mtihani wa CSEE una malengo makuu yafuatayo:
- Kupima maarifa na ujuzi uliopatikana na mwanafunzi katika masomo mbalimbali ya sekondari.
- Kutathmini uwezo wa mwanafunzi kutumia maarifa hayo katika kutatua changamoto za kijamii, kisiasa, kiuchumi, na kiteknolojia.
- Kubaini wanafunzi wenye uwezo wa kuendelea na elimu ya sekondari ya juu au kujiunga na vyuo vya kati na taasisi za mafunzo.
Mhitimu wa CSEE anatarajiwa kuonyesha uwezo wa ufahamu, matumizi, uchambuzi, uundaji, na tathmini ya maarifa katika shughuli mbalimbali za maisha binafsi na maendeleo ya taifa.
Masomo Yanayofanyiwa Mtihani wa Kidato cha Nne
Masomo ya Lazima (Core Subjects)
Kila mtahiniwa wa CSEE anatakiwa kufanya masomo saba ya lazima:
- Civics
- History
- Geography
- Kiswahili
- English Language
- Biology
- Basic Mathematics
Masomo ya Ziada
Mtahiniwa anaweza kuchagua masomo ya ziada kutoka:
- Sayansi asilia: Physics, Chemistry
- Masomo ya biashara: Commerce, Book Keeping
- Masomo ya uchumi wa nyumbani
- Masomo ya ufundi na teknologia mbalimbali
Masomo ya Hiari
Mtahiniwa anaweza kuchagua somo moja la hiari miongoni mwa: Bible Knowledge, Elimu ya Dini ya Kiislamu, Fine Art, Music, Physical Education, French, Literature in English, Arabic, Agricultural Science, Information and Computer Studies, au Additional Mathematics.
Kumbuka: Hakuna mtahiniwa anayeruhusiwa kusajili zaidi ya masomo kumi kwa mtihani mmoja wa CSEE.
Historia Fupi ya NECTA
NECTA ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa mwaka 1973 kwa sheria ya Bunge Na. 21, ikiwa na jukumu la kusimamia mitihani yote ya kitaifa nchini Tanzania. Kabla ya kuanzishwa kwake, mitihani ilisimamiwa na Wizara ya Elimu baada ya Tanzania Bara kujiondoa kwenye East African Examinations Council (EAEC) mwaka 1971.
Baada ya kuanzishwa, NECTA ilichukua rasmi usimamizi wa mitihani ya kitaifa, huku masuala ya mitaala yakiendelea kusimamiwa na taasisi nyingine hadi kuanzishwa kwa Tanzania Institute of Education (TIE) mwaka 1993. Hadi sasa, NECTA ina zaidi ya wafanyakazi 350 na makao yake makuu yapo Kijitonyama, Dar es Salaam.
Matokeo ya Kidato cha Nne 2025/2026 ni hatua muhimu katika safari ya elimu ya mwanafunzi nchini Tanzania. Ingawa tarehe rasmi ya kutangazwa bado haijatolewa, mwelekeo wa miaka ya nyuma unaonyesha kuwa matokeo haya yanaweza kutangazwa siku yeyote mwezi huu wa Januari. Wanafunzi, wazazi, na walimu wanapaswa kufuatilia taarifa rasmi za NECTA na kutumia njia sahihi za kupata matokeo ili kuhakikisha usahihi na usalama wa taarifa.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo ya Mtihani wa Kidato Cha Pili 2025 (NECTA FTNA Results)
- Matokeo ya Darasa la Nne 2025/2026 (NECTA SFNA Results)
- NECTA Yatangaza Usajili wa Watahiniwa wa Kujitegemea CSEE na FTNA 2026
- Matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba 2025/2026 NECTA
- Fomu za Kujiunga Vyuo Vya VETA 2026
- Majina ya Waliochaguliwa Kujiunga na Vyuo vya VETA 2026









Leave a Reply