Mbappé Ashinda Tuzo ya Mfungaji Bora Ulaya na La Liga kwa Mwaka 2024/25

Mbappé Ashinda Tuzo ya Mfungaji Bora Ulaya na La Liga kwa Mwaka 2024/25

Mshambuliaji wa klabu ya Real Madrid, Kylian Mbappé, ameandika historia mpya katika mchezo wa soka baada ya kutwaa tuzo mbili kubwa za ufungaji – Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya (European Golden Shoe) na Tuzo ya Pichichi kwa kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga). Huu ni ushindi wa kihistoria ambao unampa Mbappé nafasi ya kipekee katika orodha ya washambuliaji wakubwa barani Ulaya.

Katika msimu wake wa kwanza akiwa na Real Madrid baada ya kujiunga kwa uhamisho wa bure akitokea Paris Saint-Germain (PSG), Mbappé amefunga jumla ya mabao 31 kwenye La Liga. Kiasi hiki cha mabao kimemfanya awe kinara wa mabao siyo tu katika ligi ya Uhispania bali pia katika ligi tano bora barani Ulaya – ambazo ni La Liga, Premier League, Serie A, Bundesliga, na Ligue 1.

Kwa mafanikio haya, Mbappé amekuwa mchezaji wa kwanza wa Real Madrid kushinda Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya tangu Cristiano Ronaldo alivyotwaa tuzo hiyo akiwa na klabu hiyo. Mbappé pia amejiunga na orodha ndogo ya wachezaji wa Real Madrid waliowahi kutwaa tuzo hiyo, ambayo ni pamoja na Hugo Sánchez na Ronaldo mwenyewe.

Mbappé Ashinda Tuzo ya Mfungaji Bora Ulaya na La Liga kwa Mwaka 2024/25

Kanuni ya Alama Iliyompa Ushindi

Ingawa mshambuliaji wa Sporting CP ya Ureno, Viktor Gyökeres, alifunga mabao 39 katika ligi ya nyumbani, bado Mbappé ameshinda tuzo hiyo kwa mfumo wa alama unaozingatia ushindani wa ligi. Kulingana na mfumo huo, bao moja lililofungwa katika mojawapo ya ligi tano bora Ulaya linahesabiwa kwa pointi mbili, huku bao kutoka ligi ya hadhi ya kati likihesabiwa kwa pointi 1.5.

Kwa msingi huo, mabao 31 ya Mbappé katika La Liga yamempa pointi 62, na kumuweka juu ya Gyökeres ambaye, licha ya mabao mengi, alipata pointi 58.5 tu. Nyota wa Liverpool Mohamed Salah alimaliza msimu akiwa na pointi 58 baada ya kufunga mabao 29.

Ushindani Mkali na Mafanikio ya Kipekee

Mbappé, mwenye umri wa miaka 26, ameonyesha kiwango cha juu sana katika msimu wake wa kwanza nchini Uhispania. Katika mechi 55 alizoichezea Real Madrid katika mashindano yote, amefunga jumla ya mabao 43, ambapo 31 kati ya hayo yalitokana na michezo ya La Liga.

Mafanikio haya yamemuwezesha kuvunja rekodi iliyowekwa na mshambuliaji wa zamani wa Madrid, Alfredo Di Stéfano, ambaye alifunga mabao 27 katika msimu wake wa kwanza na klabu hiyo. Aidha, Mbappé amevuka pia rekodi ya Cristiano Ronaldo ya mabao 33 aliyoweka katika msimu wake wa kwanza mwaka 2009-2010.

Katika moja ya mechi kubwa za La Liga – El Clásico dhidi ya FC Barcelona – Mbappé alifanikiwa kufunga mabao matatu (hat-trick), jambo ambalo limeongeza heshima yake katika historia ya Real Madrid na soka la Uhispania kwa ujumla.

Tuzo ya Pichichi na Heshima ya Kifaransa

Mbappé pia ameshinda Tuzo ya Pichichi kwa kuwa mfungaji bora wa La Liga 2024/25, akiwapiku washambuliaji wakubwa akiwemo Robert Lewandowski wa Barcelona, aliyefunga mabao 27. Lewandowski alikuwa mtetezi wa tuzo hiyo, baada ya kuibuka mshindi msimu uliopita.

Kwa upande wa heshima ya taifa, Mbappé amekuwa Mfaransa wa kwanza kutwaa Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya tangu Thierry Henry alipofanya hivyo miaka ya 2004 na 2005 akiwa na Arsenal.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Rs Berkane Yabeba Ubingwa Kombe la Shirikisho Afrika 2024/2025
  2. Ndoto ya Ubingwa Shirikisho ya Simba Yazimwa Baada ya Sare Amaan Complex
  3. Simba vs Berkane Leo 25/05/2025 Saa Ngapi?
  4. Matokeo ya Simba vs RS Berkane Leo 25/05/2025
  5. KIKOSI CHA SIMBA VS BERKANE LEO 25/05/2025 – FAINALI YA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA
  6. Rais Mwinyi Aahidi Mamilioni Kwa Simba Wakishinda Kombe la Shirikisho
  7. Mamelodi Sundowns Yatoshana Nguvu na Pyramids FC Pretoria
  8. Simba Yapokewa Dar kwa Shangwe Kubwa Baada ya Mtanange Mkali Zanzibar
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo