Mechi Dhidi ya Coastal Union na Azam FC Kuamua Hatma ya Fountain Gate Ligi Kuu
Wakati msimu wa 2024/2025 wa Ligi Kuu ya NBC ukielekea ukingoni, Fountain Gate imeweka mikakati kabambe ya kupambania nafasi ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao, huku macho yote yakielekezwa kwenye mechi zao mbili za mwisho dhidi ya Coastal Union na Azam FC.
Timu hiyo ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi, bado ina matumaini makubwa ya kusalia kwenye ligi bila kulazimika kushiriki mchujo wa kuwania kubaki.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Fountain Gate Academy, Japhet Makau, mechi hizo mbili zilizobaki ni fursa muhimu kwa timu hiyo kuthibitisha uwezo wao na kujihakikishia nafasi katika msimu ujao wa Ligi Kuu. Fountain Gate itashuka dimbani Jumatano dhidi ya Coastal Union, kabla ya kumaliza msimu kwa kukipiga na Azam FC tarehe 22 Juni.
Makau amesema kuwa timu hiyo inajiandaa kwa ari na matumaini makubwa, akisisitiza kuwa hawana hofu ya kushuka daraja wala kushiriki play-off, kwani wanaamini watafanya vizuri katika mechi hizo mbili zilizobaki.
“Nawaambia hatuchezi play-off. Tukutane msimu ujao tukiwa imara zaidi. Tuna mipango kabambe ya kujijenga upya na kurudi tukiwa timu shindani zaidi,” alisema Makau kwa msisitizo.
Mbali na mapambano ya uwanjani, Fountain Gate pia inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha ustawi wa wachezaji wake. Hivi karibuni, klabu hiyo iliingia makubaliano rasmi na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kupitia ushirikiano maalum wa kuanzisha na kusimamia Sports Cardiology Program – mpango wa uchunguzi wa awali wa afya ya moyo kwa wanamichezo.
Mpango huo unalenga kuhakikisha kuwa wachezaji wanapimwa afya kabla ya kushiriki mazoezi au mechi, ikiwa ni hatua ya kuzuia matatizo makubwa ya kiafya kama vile vifo vya ghafla vinavyosababishwa na matatizo ya moyo ambayo huweza kuwa hayajatambuliwa.
“Kwa miaka yote nane ya shule zetu, hatujawahi kupata majanga ya kiafya kwa wanamichezo wetu. Hatuwezi kusubiri miujiza tu, tunachukua hatua ya makusudi kulinda afya ya vijana wetu,” alieleza Makau.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Dkt. Angela Muhozya, alifafanua kuwa ushirikiano huo ni wa kipekee na unalenga kuziba pengo katika huduma za kinga, hususan kwa wanamichezo chipukizi nchini. Amesema mpango huo utatekelezwa katika shule zote 15 za Fountain Gate zilizopo maeneo mbalimbali ya Tanzania.
“Lengo kuu ni kubaini matatizo ya moyo mapema kabla hayajasababisha madhara makubwa. Hii itasaidia kuzuia vifo vya ghafla vya moyo ambavyo vimeshuhudiwa mara kadhaa hata kwa wanamichezo waliokuwa na afya nzuri kwa nje,” alisema Dkt. Angela.
Wakati timu ya wakubwa ikiendelea na juhudi za kubaki ligi kuu, vijana wa Fountain Gate pia wanaonesha kuwa na uwezo mkubwa wa ushindani. Makau alieleza kuwa timu yao ya vijana chini ya miaka 20 ilikuwa na nafasi ya kuchukua ubingwa katika michuano yao ya hivi karibuni, lakini walipoteza nafasi hiyo kwa bao la utata dhidi ya Azam FC.
“Timu yetu ya vijana ilikuwa na haki ya kuwa mabingwa, lakini bao la utata limetufanya tumalize nafasi ya pili. Hili limetupa motisha ya kurudi tukiwa na nguvu mpya msimu ujao,” alisema Makau.
Kwa ujumla, hatma ya Fountain Gate kwenye Ligi Kuu msimu huu iko mikononi mwao wenyewe.
Matokeo ya mechi dhidi ya Coastal Union na Azam FC yatakuwa ya kihistoria, kwani yanaweza kuamua kama timu hiyo itaendelea kuwa sehemu ya ushindani wa juu wa soka la Tanzania, au la. Kwa maandalizi yanayoendelea ndani na nje ya uwanja, ni wazi kwamba Fountain Gate haijakata tamaa, bali inajiandaa kupambana hadi dakika ya mwisho.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ratiba ya Kombe la Dunia la Vilabu 2025
- Al Ahly Yatoka Sare na Inter Miami ya Messi Kombe la Dunia la Vilabu FIFA 2025
- Liverpool Yakamilisha Dili la Pauni Milioni 116 Kumsajili Florian Wirtz
- Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB Almasi Kasongo Asimamishwa Kazi na TFF
- Steven Mguto Ajiuzulu Uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)
- Msimamo wa Makundi ya Kombe la Dunia la Vilabu 2025
- Franco Mastantuono Ajiunga Rasmi na Real Madrid | Habari Kamili
- Benchi la Ufundi Kengold Njiapanda, Maandalizi Dhidi ya Simba Yakosa Mwelekeo
Leave a Reply