Milos Kerkez Ajiunga Rasmi na Liverpool kwa Ada ya Pauni Milioni 40
Klabu ya Liverpool imetangaza rasmi kumsajili beki wa kushoto, Milos Kerkez, kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 40, akitokea Bournemouth. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 anakuwa miongoni mwa usajili muhimu katika dirisha hili, akiungana na Jeremie Frimpong na Florian Wirtz kama sehemu ya wachezaji wapya waliotua Anfield kuelekea msimu mpya wa 2025/26.
Kerkez ambaye ni mzaliwa wa Serbia lakini anaiwakilisha timu ya taifa ya Hungary, amesaini mkataba wa miaka mitano na Liverpool, hatua ambayo inamfanya kuwa sehemu ya kikosi kinachojengwa upya chini ya safu mpya ya uongozi wa kiufundi.
Safari ya Kerkez: Kutoka Bournemouth Hadi Anfield
Baada ya kung’ara kwa misimu miwili akiwa na Bournemouth, Kerkez ameonyesha ubora mkubwa kwenye nafasi ya beki wa kushoto. Katika msimu wa 2024/25, alicheza mechi 38 mfululizo kwenye Ligi Kuu ya England (Premier League), akisaidia Bournemouth kufikisha pointi 56 kiwango cha juu zaidi katika historia ya klabu hiyo.
Katika kipindi chake huko, Kerkez alifunga magoli 2 na kutoa ‘assists’ 8, akijijengea heshima kama mmoja wa mabeki chipukizi bora zaidi barani Ulaya. Ubora huo umevutia Liverpool ambao wameamua kumuongeza kwenye kikosi chao kuelekea msimu mpya wa mashindano.
Historia Fupi ya Kerkez Kabla ya Bournemouth
Licha ya kuwa kijana, Kerkez ana historia ya kipekee kisoka. Mnamo mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 17, alipokea simu kutoka kwa gwiji wa AC Milan, Paolo Maldini, ambaye alimsihi ajiunge na miamba hao wa Serie A. Bila kusita, Kerkez alihamia Italia, ingawa hakupata nafasi ya kucheza mechi yoyote ya mashindano akiwa na Milan.
Mwaka mmoja baadaye, alihamia klabu ya AZ Alkmaar ya Uholanzi kabla ya kusajiliwa na Bournemouth mnamo Julai 2023. Huko ndipo alipoanza kuonyesha kiwango chake halisi, jambo lililomfanya kuvutia macho ya Liverpool.
Baada ya kusaini mkataba, Kerkez alielezea furaha yake kwa kusema:
“Ni heshima kubwa sana kwangu, ni ndoto kutimiza kucheza kwa moja ya vilabu vikubwa duniani, klabu kubwa zaidi England. Nimefurahi mno na nasubiri kwa hamu kuanza mazoezi na kujiandaa kwa msimu mpya.”
Usajili Mwingine wa Liverpool Dirisha Hili
Mbali na Kerkez, Liverpool tayari wamekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji Florian Wirtz kwa ada ya kihistoria ya pauni milioni 116 na beki wa kulia Jeremie Frimpong kwa pauni milioni 29.5, wote kutoka Bayer Leverkusen. Aidha, kipa wa Hungary chini ya miaka 21, Armin Pecsi, naye amejiunga kwa ada ya hadi pauni milioni 1.5.
Liverpool pia wanatarajiwa kumalizia usajili wa kipa wa timu ya taifa ya Georgia, Giorgi Mamardashvili, kutoka Valencia kwa ada ya pauni milioni 25 pamoja na nyongeza ya pauni milioni 4.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Kikosi cha Tanzania CHAN 2024: Wachezaji Kuingia Kambini Julai 7, 2025
- Yanga Yailaza Simba 2-0 na Kutwaa Kombe la Ligi Kuu Kwa Mara ya 31
- Mechi ya Yanga vs Simba Kupigwa Chini ya Uangalizi wa Waamuzi Kutoka Misri
- Tetesi Za Usajili Simba Leo 2025/2026
- Tetesi Za Usajili Yanga Leo 2025/2026
- Ratiba ya Mechi za Leo Ligi Kuu ya NBC 22/06/2025
- TFF Yafunga Rasmi Zoezi la Uchukuaji wa Fomu za Uongozi – Wagombea 25 Wajitokeza
Leave a Reply