Mohamed Salah Awaongoza Liverpool Kuizamisha Manchester United
Mohamed Salah ameendelea kuthibitisha ubora wake uwanjani kwa kuiongoza Liverpool kupata ushindi wa kishindo wa 3-0 dhidi ya Manchester United katika uwanja wa Old Trafford. Huu ulikuwa ni mwendelezo wa matokeo mabaya kwa Manchester United dhidi ya mpinzani wao mkubwa, Liverpool, katika mchezo unaojulikana kuwa ni miongoni mwa michezo mikubwa zaidi kwenye soka la England.
Salah, ambaye amekuwa na rekodi ya kuvutia dhidi ya Manchester United, alifunga bao lake la saba mfululizo katika uwanja huo maarufu wa Old Trafford. Hakuishia hapo, pia alitoa pasi mbili za mabao kwa Luis Diaz katika kipindi cha kwanza, pasi ambazo zilizidi kuwaumiza Manchester United na kuzamisha zaidi matumaini yao katika mchezo huo.
Liverpool, ambao walikuwa wanatafuta kurejesha heshima yao dhidi ya wapinzani wao wa jadi, walionyesha tena udhibiti wao uwanjani kwa mchezo wa hali ya juu. Kwa upande wa Manchester United, ilikuwa ni ndoto mbaya zaidi kwa Casemiro, ambaye alikosa utulivu na kufanya makosa yaliyopelekea Liverpool kufunga mabao mawili kupitia Luis Diaz. Casemiro alitolewa nje kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na kijana mdogo, Toby Collyer, mwenye umri wa miaka 20.
Mohamed Salah, sasa amefunga mabao 15 dhidi ya Manchester United tangu ajiunge na Liverpool mwaka 2017. Upendo wa mashabiki wa Liverpool haukujificha pale walipoanza kumuimbia nyimbo za sifa mwishoni mwa mchezo, ishara ya kuthamini mchango wake mkubwa.
Pamoja na kuipa Liverpool ushindi mkubwa, Salah amethibitisha kuwa yeye ni mchezaji wa kiwango cha juu katika ligi kuu ya England. Alipohojiwa baada ya mchezo, Salah alikiri kuwa alitarajia mchezo kuwa mgumu zaidi, lakini Liverpool ilionyesha ubora na utawala wa hali ya juu na kushinda mechi kwa urahisi.
Changamoto za Manchester United
Kwa Manchester United, hali ya sintofahamu imeendelea kuzunguka kikosi cha Erik ten Hag. Hii mekuwa ni mara ya pili katika mechi tatu za ligi msimu huu ambapo United wamepoteza, huku ushindi wao pekee ukija dhidi ya Fulham kwa bao la dakika za mwisho.
Matumizi makubwa ya fedha katika dirisha la usajili, ikiwemo kumsajili Manuel Ugarte kwa $55 milioni, hayajazaa matunda tarajiwa kwa timu ambayo imekuwa ikihangaika kurudisha hadhi yake ya zamani.
Casemiro, aliyenunuliwa kwa gharama kubwa kutoka Real Madrid, alionekana kupoteza mwelekeo katika mchezo huu, na makosa yake yaligharimu timu yake vibaya. Uwepo wa Ugarte, ambaye anatazamiwa kuwa mrithi wa muda mrefu wa Casemiro, huenda ukawa ni ishara ya mabadiliko zaidi yanayotarajiwa katika kikosi cha Manchester United.
Mapendekezo ya Mhariri:
Weka Komenti