Morocco Yatinga Fainali ya CHAN Baada ya Kuifunga Senegal kwa Penalti
Morocco imefuzu fainali ya CHAN 2024 baada ya kuifunga Senegal kwa mikwaju ya penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120 kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, Kampala, Jumanne usiku.
Matokeo haya yameiwezesha Morocco, maarufu kama Atlas Lions, kucheza fainali ya tatu ya CHAN ndani ya kipindi cha miaka sita, wakitarajia kukutana na Madagascar katika fainali itakayopigwa Jumamosi jijini Nairobi.
Mchezo ulianza kwa kasi huku mabingwa watetezi Senegal wakionekana wenye nidhamu na kujiamini. Bao la kuongoza lilifungwa na Joseph Layousse dakika ya 16 baada ya kupiga kichwa kizuri kutoka kona ya Libasse Guèye.
Hata hivyo, Morocco haikusubiri muda mrefu kusawazisha. Dakika saba baadaye, Sabir Bougrine alipiga shuti kali nje ya eneo la hatari lililopaa moja kwa moja kwenye nyavu za juu, na kuirejesha Morocco mchezoni kwa sare ya 1-1.
Kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika, timu zote mbili zilipata nafasi za kuongeza mabao lakini walikosa umakini. Layousse alikosa tena kwa kichwa cha karibu, huku kipa Marc Diouf wa Senegal akiokoa mpira wa Anas Bach upande wa pili.
Kabumbu Sali Lapigwa Kipindi cha Pili na Dakika za Nyongeza
Kipindi cha pili kilikuwa na mchezo wa tahadhari zaidi. Morocco ilianza kumiliki mpira zaidi, huku Senegal wakiendelea kuwa hatari kupitia mipira ya adhabu na kona. Makipa wa timu zote walikuwa mashujaa. El Mehdi Al Harrar wa Morocco aliokoa michomo kadhaa ya Layousse na Seyni Ndiaye, huku Diouf wa Senegal akiokoa mipira ya Youssef Mehri na Oussama Lamlaoui.
Makocha walifanya mabadiliko ya wachezaji ili kuongeza nguvu. Morocco iliingiza Ayoub Khairi na Salaheddine Errahouli, huku Senegal ikiwapa nafasi Insa Boye na Ababacar Sarr. Licha ya juhudi zote, dakika za nyongeza zilikosa mabao.
Nafasi bora zaidi ilikuja dakika ya 119, ambapo kichwa cha Lamlaoui kilipanguliwa na Diouf, na sekunde chache kabla, Bonaventure Fonseca wa Senegal alipiga shuti juu ya lango la Morocco.
Mikwaju ya Penalti: Morocco Yafuzu kwa Ukomavu
Kwa kuwa mchezo ulikuwa sare ya 1-1, penati zilihitajika kuamua mshindi. Morocco ilipiga mikwaju yake mitano kwa usahihi kupitia Hrimat, Lamlaoui, Khairi, Bach, na Mehri.
Senegal ilianza vibaya baada ya nahodha Seyni Ndiaye kugonga mwamba katika mkwaju wa kwanza. Ingawa Vieux Cissé, Baye Ciss, na Daouda Ba walipata penalti zao, haikutosha kuizuia Morocco kushinda kwa jumla ya 5-3.
Kauli za Makocha Baada ya Mechi
Kocha wa Morocco Tarik Sektioui aliisifu timu yake kwa ustahimilivu na ukomavu wao:
“Ilikuwa mechi ngumu dhidi ya mabingwa watetezi, lakini wachezaji walionesha utulivu kwenye nyakati muhimu. Tumepambana kufikia hatua hii, sasa tunataka kulitwaa taji tena,” alisema Sektioui.
Kwa upande mwingine, kocha wa Senegal Souleymane Diallo alionekana kujivunia vijana wake licha ya kupoteza:
“Hii ni kizazi kipya chenye ujasiri na nidhamu. Penalti huwa na ukatili wake, lakini mustakabali wa timu yetu bado ni mzuri,” alisema Diallo.
Morocco vs Madagascar: Fainali Yakibabe
Morocco sasa itakutana na Madagascar katika fainali ya CHAN 2024 kwenye Uwanja wa Moi Sports Centre Kasarani, Nairobi. Wakati huo huo, Senegal itacheza mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu dhidi ya Sudan jijini Dar es Salaam.
Kwa Morocco, hii ni nafasi nyingine ya kurejesha ubabe wao barani Afrika na kujiweka sawa na rekodi za mataji ya CHAN. Kwa Senegal, ndoto ya kutetea ubingwa imeisha, lakini heshima na matumaini kwa kizazi kipya vimebaki hai.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Simba SC Yasogeza Tarehe ya Uzinduzi wa Jezi Mpya 2025/2026
- Viingilio Simba Day 2025
- Ligi Kuu Zanzibar ZPL 2025/2026 kuanza Septemba 20
- Jezi Mpya za Yanga 2025/2026 | Picha za Jezi Mpya za Yanga
- Bei ya Jezi Mpya za Yanga 2025/2026
- Matokeo ya Taifa Stars vs Morocco Leo 22/08/2025 CHAN
- Kikosi cha Taifa Stars vs Morocco Leo 22/08/2025 CHAN
- Cv ya Neo Maema Kiungo Mpya wa Simba 2025/2026
- Wafungaji Bora CHAN 2025
Leave a Reply