Nsingizini Hotspurs vs Simba Leo 19/10/2025 Saa Ngapi?
Wekundu wa Msimbazi Simba SC leo watakuwa kibaruani kuipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), baada ya watani wao wa jadi Yanga SC kufungua raundi ya pili kwa kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers huko Malawi. Hii ni nafasi muhimu kwa Simba kurejesha heshima ya soka la Tanzania barani Afrika, wakiwa wageni wa Nsingizini Hotspurs kutoka Eswatini kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya pili ya michuano hiyo.
Nsingizini Hotspurs vs Simba Leo 19/10/2025 Saa Ngapi?
Mchezo kati ya Nsingizini Hotspurs vs Simba utafanyika leo Jumapili, Oktoba 19, 2025, katika Uwanja wa Somhlolo uliopo Eswatini, na utapigwa saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki (EAT).
Simba SC Kuendeleza Rekodi Yao Barani Afrika
Simba SC, ambayo inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, inaingia katika mchezo huu ikiwa na hamasa kubwa ya kufanya vizuri baada ya kuonyesha ubora katika hatua ya awali. Klabu hiyo imekuwa chini ya uongozi wa makocha wawili msimu huu — Fadlu Davids na Hemed Suleiman ‘Morocco’ kabla ya ujio wa kocha mpya Dimitar Pantev, ambaye awali alikuwa akiifundisha Gaborone United ya Botswana.
Pantev ameahidi ushindi na furaha kwa mashabiki wa Simba, akieleza kuwa maandalizi ya timu yako vizuri licha ya changamoto ya kucheza katika uwanja wa nyasi bandia na hali ya hewa yenye baridi. Akizungumza na waandishi wa habari, Pantev alisema:
“Maandalizi yako kawaida, timu imepata motisha ya kutosha. Tutafuata mbinu tulizojiandaa nazo na kucheza soka letu la kawaida. Huenda mazingira yakawa magumu kidogo kutokana na baridi, lakini hali ni sawa kwa timu zote.”
Historia ya Simba Nchini Eswatini
Simba SC inarejea Eswatini baada ya takribani miaka saba tangu ilipocheza mara ya mwisho dhidi ya Mbabane Swallows mnamo Desemba 4, 2018. Katika mchezo huo, Simba ilishinda kwa mabao 4-0 kupitia Clatous Chama (dakika ya 28 na 32), Emmanuel Okwi (dk 51), na Meddie Kagere (dk 62). Jumla, Simba iliiondoa Mbabane Swallows kwa mabao 8-1 baada ya kushinda 4-1 katika mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam.
Nsingizini Hotspurs Wakiwa Nyumbani
Kwa upande wa Nsingizini Hotspurs, hii ni mara ya kwanza kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Eswatini msimu wa 2024/2025. Timu hiyo kwa sasa inafundishwa na Mandla David Qhogi, baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa Simon Ngomane aliyekuwa kocha wa muda.
Msimu uliopita, Nsingizini Hotspurs ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika lakini ikatolewa hatua ya awali na Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 8-0 (3-0 nyumbani na 5-0 ugenini). Hata hivyo, msimu huu wamepania kufanya historia mpya katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Rais wa klabu hiyo, Derrick Shiba, amesema kwa ujasiri kwamba matokeo ya leo yataamua hatma yao katika mashindano hayo. Alisisitiza umuhimu wa kutumia vyema faida ya kucheza nyumbani:
“Mchezo wa leo ni fainali yetu. Ni lazima tushinde nyumbani kwa sababu matokeo ya kurudiana nchini Tanzania yatategemea kile kitakachotokea hapa.”
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo ya Silver Strikers vs Yanga SC Leo 18/10/2025
- Timu Zilizofuzu Kombe la Dunia 2026
- Msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar PBZ 2025/2026
- Majina Ya Usaili Kusimamia Uchaguzi 2025 Jimbo La Temeke, Mbagala na Chamazi
- Pacome Anukia Kombe la Dunia Baada ya Ushindi 7-0 Dhidi ya Shelisheli
- Zimbabwe Yainyima Nafasi Afrika Kusini Kufuzu Kombe la Dunia
Leave a Reply