Ratiba ya Ligi Kuu NBC Leo 04/04/2026
Ligi Kuu ya NBC inaendelea tena leo Jumamosi huku mitanange mitatu ya kukatana shoka itapigwa kwenye viwanja tofauti nchini, ambapo mashabiki wa soka watashuhudia mabingwa watetezi Yanga wakishuka dimbani kuwakabili Tanzania Prisons katika pambano linalotarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi kutokana na mwenendo wa timu hizo ulivyo kwa sasa.
Yanga SC vs Tanzania Prisons
Saa 12:30 jioni | Uwanja wa KMC Complex, Mwenge – Dar es Salaam
Mabingwa watetezi Yanga wanaingia katika mchezo huu wakiwa na presha baada ya kutoka sare tatu mfululizo katika ligi. Matokeo hayo yameweka shinikizo kwa benchi la ufundi likiongozwa na kocha Pedro Goncalves.
Yanga, ambao wana rekodi ya kutopoteza mechi 36 za ligi tangu Novemba 7, 2024, wamekuwa na mabadiliko ya kiwango msimu huu. Katika mechi 16 walizocheza, wameshinda 11 na sare tano, hali inayowafanya waendelee kuongoza msimamo kwa pointi 38.
Kwa upande wa Tanzania Prisons, timu hiyo pia inapitia kipindi kigumu ikiwa haijapata ushindi katika mechi nne mfululizo. Ushindi wao wa mwisho ulikuwa Februari 14, 2026 walipoifunga Namungo FC mabao 3-2. Tangu hapo, wamepoteza mechi tatu na kutoka sare moja, wakibaki nafasi ya 15 na pointi 13.
Kocha wa Prisons, Shadrack Nsajigwa, amesema:
“Hatupo sehemu nzuri na ili tutoke chini tulipo kwa sasa ni lazima tupate matokeo mazuri katika kila mechi tunazocheza.”
Kwa upande wa Yanga, kocha msaidizi Matthew Silva alieleza:
“Tunatambua kiu ya mashabiki wetu ni kuona tunashinda… tutapambana ili kupata matokeo mazuri.”
Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Yanga ilishinda bao 1-0 kupitia kwa Laurindo ‘Depu’.
Mashujaa FC vs Pamba Jiji
Saa 10:00 jioni | Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma
Mashujaa FC watakuwa nyumbani wakisaka kulipiza kisasi dhidi ya Pamba Jiji baada ya kufungwa mabao 2-1 katika mchezo wa awali uliopigwa Oktoba 17, 2025.
Katika msimamo wa ligi, Mashujaa wako nafasi ya 11 na pointi 19 baada ya kushinda mechi nne, sare saba na kupoteza sita. Pamba Jiji, wao wapo nafasi ya tano na pointi 25 baada ya kushinda sita, sare saba na kupoteza tatu.
Takwimu zinaonyesha kuwa Mashujaa wana kumbukumbu nzuri wanapocheza nyumbani Kigoma, ambapo waliwahi kushinda mabao 2-0 katika mechi iliyopita ya uwanja huo.
Namungo FC vs JKT Tanzania
Saa 3:00 usiku | Uwanja wa Majaliwa, Lindi
Namungo FC wataingia uwanjani wakiwa wanatafuta ushindi wao wa kwanza baada ya mechi saba bila kushinda. Tangu walipoifunga KMC Januari 31, 2026, wamepoteza mechi nne na kutoka sare tatu, wakishika nafasi ya nane na pointi 21.
JKT Tanzania wao wanaingia katika mchezo huu wakiwa katika nafasi ya nne na pointi 28. Wameshinda mechi saba, sare saba na kupoteza tatu katika michezo 17 ya msimu huu.
Rekodi ya timu hizi inaonyesha ushindani mkubwa, kwani katika mechi nne zilizopita hakuna timu iliyoweza kutawala mwenzake. Mchezo wao wa mwisho ulimalizika kwa sare ya 1-1 Oktoba 19, 2025.
Mapendekezo ya Mhariri:









Leave a Reply