Real Madrid Yapoteza 2-5 Dhidi ya Atletico Madrid, Kichapo cha Kwanza kwa Xabi Alonso LaLiga
Hatimaye, Xabi Alonso amepoteza mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (LaLiga) baada ya Real Madrid kukubali kichapo kizito cha mabao 5-2 dhidi ya Atletico Madrid katika Dabi ya Jiji la Madrid, iliyopigwa kwenye dimba la Metropolitano. Matokeo haya yanaweka rekodi ya kwanza kwa Alonso tangu achukue majukumu ya kuiongoza Los Blancos msimu huu.
Mchezo Ulivyokua
Mchezo ulianza kwa kasi, ambapo wenyeji Atletico Madrid walipata bao la kuongoza dakika ya 14 kupitia kichwa safi cha Robin Le Normand, aliyemzidi nguvu Aurelien Tchouameni baada ya krosi ya Giuliano Simeone. Hata hivyo, Real Madrid hawakukaa kimya, na Kylian Mbappe alisawazisha bao hilo baada ya kupokea pasi maridadi kutoka kwa Arda Guler na kumalizia kwa ustadi.
Dakika chache baadaye, Guler aliongeza bao la pili kwa Real Madrid baada ya kazi nzuri ya Vinicius Junior, akipiga shuti la nusu voli lililomshinda Jan Oblak. Lakini Atletico walihakikisha wanaondoka mapumziko wakiwa sare 2-2, kufuatia kichwa cha Alexander Sorloth kilichomshinda Thibaut Courtois sekunde chache kabla ya kipenga cha mapumziko.
Onyesho la Alvarez
Kipindi cha pili kiligeuka kuwa uwanja wa Julian Alvarez. Straika huyo wa Argentina alifunga mabao mawili ndani ya dakika 12, likiwemo la penalti baada ya Nicolas Gonzalez kuumizwa na buti ya juu ya Guler. Baadaye, Alvarez aliongeza bao la bure kupitia mpira wa adhabu uliomshinda Courtois dakika ya 63.
Real Madrid walijitahidi kurudi mchezoni, lakini mashambulizi yao yaliwaacha wazi na Atletico kutumia nafasi hiyo. Antoine Griezmann alihitimisha ushindi mnono wa 5-2 kwa Los Rojiblancos kwa bao safi la dakika za majeruhi.
Takwimu Muhimu za Mchezo
Kwa mujibu wa takwimu, Atletico Madrid walistahili ushindi huu baada ya kuandikisha kiwango cha mabao yaliyotarajiwa (xG) cha 2.31 ikilinganishwa na 0.58 ya Real Madrid. Pia walipiga mashuti 13 dhidi ya sita ya wageni.
Julian Alvarez, ambaye tayari alikuwa amefunga hat-trick katika ushindi wa katikati ya wiki dhidi ya Rayo Vallecano, aliendeleza kiwango chake kwa mabao ya mpira uliokufa. Alijumuika na Luis Suarez kama mchezaji pekee wa Atletico karne hii kufunga bao la penalti na la mpira wa moja kwa moja wa adhabu katika mechi moja ya LaLiga.
Kichapo hiki kinamaanisha Alonso ameshindwa kuendelea na rekodi ya ushindi mtupu tangu aingie LaLiga, na kushindwa kufuata nyayo za Vanderlei Luxemburgo, kocha wa mwisho wa Real Madrid kushinda michezo yake saba ya kwanza kwenye ligi mwaka 2005.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo ya Yanga vs Wiliete SC Leo 27/09/2025
- Yanga vs Wiliete SC Leo 27/09/2025 Saa Ngapi?
- Kikosi cha Yanga vs Wiliete SC Leo 27/09/2025
- KMKM Yatinga Raundi ya Pili ya CAF Baada ya Kuichapa AS Port ya Djibouti
- Sergio Busquets Atangaza Kustaafu Soka Mwishoni Mwa Msimu Huu
- Kocha Folz Aahidi Ushindi Mkubwa Mechi ya Marudiano Dhidi ya Wiliete
- Yanga SC Yazindua Jezi Mpya Ili Kulinda Mapato Dhidi ya Jezi Feki
- Msimamo wa Ligi kuu NBC Tanzania 2025/2026
Leave a Reply