Shirikisho la Soka Zanzibar Laitwanga KVZ Faini ya Milioni 3 Kisa Vurugu
Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) limeichukulia hatua kali klabu ya KVZ kwa kuhusishwa na vitendo vya vurugu vilivyotokea katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ZFF Cup) dhidi ya timu ya Uhamiaji, kwa kuiadhibu kwa faini ya shilingi milioni 3.
Adhabu hiyo imetolewa baada ya ZFF kupokea na kuchambua ripoti mbalimbali kutoka kwa mwamuzi wa mchezo, kamisaa, mratibu wa mechi pamoja na maofisa wa usalama waliokuwepo uwanjani siku ya tukio. Mechi hiyo ya nusu fainali ilichezwa tarehe 11 Juni 2025 katika Uwanja wa Mao A, Unguja, ambapo KVZ ilipata ushindi wa mabao 2-1 na kufuzu hatua ya fainali.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka kwa Katibu wa Kamati ya Mashindano ya ZFF, Ali Bakar Ali ‘Cheupe’, vurugu zilianza mara baada ya kipenga cha mwisho. Baadhi ya mashabiki na wachezaji wa Uhamiaji walidaiwa kuwafuata waamuzi na kuwazungumzia maneno yasiyofaa. Hata hivyo, walinzi wa usalama (Stewards) waliingilia kati na kuwaondoa nje ya uwanja.
Hali ilibadilika ghafla pale ambapo mashabiki pamoja na baadhi ya askari wa KVZ walivamia uwanja wakiwa wameficha sura zao na wakibeba silaha. Waliripotiwa kuwashambulia wachezaji wa Uhamiaji pamoja na benchi lao la ufundi, jambo lililosababisha taharuki kubwa na kuhitaji uingiliaji wa haraka wa maafisa wa usalama.
Kamati ya Mashindano ya ZFF ilizingatia ushahidi uliopatikana kupitia picha za video na taarifa zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zinazoonyesha vurugu hizo. Kwa mujibu wa kanuni za Mashindano ya ZFF 2024/2025, sura ya ishirini (3) (ii&iii), klabu ya KVZ imeamriwa kulipa faini ya Shilingi milioni 3 kabla ya kushiriki fainali ya ZFF Cup inayotarajiwa kuchezwa tarehe 22 Juni 2025.
ZFF imeonya kuwa kutokulipa faini hiyo ndani ya muda uliowekwa kutaiweka KVZ katika hatari ya kuchukuliwa hatua zaidi za kinidhamu kama ilivyoelekezwa na kanuni husika.
Mbali na adhabu dhidi ya KVZ, Kamati hiyo pia imetoa onyo kali kwa kiongozi wa Uhamiaji FC, Mwinyi Hamad, kutokana na ushiriki wake katika vurugu hizo. Endapo atahusishwa tena na vitendo kama hivyo, ZFF itamchukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sura ya ishirini (3)(i) ya kanuni hizo.
Mwamuzi Thobias Warriko Afungiwa kwa Miezi Mitatu
Katika hatua nyingine, Kamati ya Waamuzi ya ZFF imemfungia mwamuzi wa pambano hilo, Thobias Warriko, kwa muda wa miezi mitatu kutokana na kushindwa kutafsiri vyema sheria za mchezo wa soka katika mechi hiyo ya nusu fainali.
Tarehe 12 Juni 2025, klabu ya Uhamiaji ilitoa taarifa rasmi ikieleza kuwa wachezaji wake saba pamoja na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi walijeruhiwa vibaya kwenye vurugu hizo. Majeruhi hao walifikishwa katika Kituo cha Polisi Madema ambako walipewa PF3 kwa ajili ya kuanza mchakato wa matibabu.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Tetesi Za Usajili Simba Leo 2025/2026
- Genaro Gattuso Ateuliwa Kuwa Kocha Mpya wa Timu ya Taifa ya Italia 2025
- Bayern Munich Yaitandika Auckland City Magoli 10–0 Kombe la Dunia la Vilabu FIFA
- Mechi Dhidi ya Coastal Union na Azam FC Kuamua Hatma ya Fountain Gate Ligi Kuu
- Ratiba ya Kombe la Dunia la Vilabu 2025
- Form Five Selection 2025: Majina Waliochaguliwa Kidato cha Tano 2025/2026 Yatangazwa!
- Al Ahly Yatoka Sare na Inter Miami ya Messi Kombe la Dunia la Vilabu FIFA 2025
Leave a Reply