Simba Warudi Sokoni Kusaka Mshambuliaji Mpya Kuongeza Makali
Simba Sports Club, baada ya kuchapwa bao 1-0 na watani wao wa jadi Yanga katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii, wameamua kurudi sokoni kutafuta mshambuliaji mpya kabla ya dirisha kubwa la usajili kufungwa Agosti 15. Uamuzi huu umekuja baada ya viongozi wa klabu na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, kuonesha kutoridhishwa na safu ya ushambuliaji ya timu.
Benchi la ufundi linataka mshambuliaji mpya atakayekuja kusaidiana na Steve Mukwala huku Fred Michael akitarajiwa kupata nafasi ndogo ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza. Habari kutoka ndani ya klabu zinasema kuwa viongozi wote wa Simba, akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji, wamekubaliana kuwa wanahitaji mshambuliaji mpya haraka iwezekanavyo.
Uongozi wa Simba unaamini kuwa timu inacheza vizuri lakini inakosa mshambuliaji mwenye uchu wa mabao. Kwa hivyo, wameingia sokoni kumsaka mchezaji wa aina hiyo ambaye atatangazwa kabla ya dirisha dogo kumalizika. Kuna uwezekano kuwa mchezaji mmoja ataondoka kumpisha mshambuliaji huyo mpya, huenda akawa Ayoub Lakred, au Fred Michael.
Viongozi wa Simba wanayo majina kadhaa ya wachezaji ambayo wanayafanyia kazi, lakini bado hawajafikia uamuzi wa mwisho. Kocha Fadlu Davids amekuwa akilalamikia safu yake ya ushambuliaji hata kwenye mechi tatu za kirafiki walizocheza nchini Misri, akisema kuwa zinatengenezwa nafasi nyingi lakini hazitumiwi. Baada ya mechi dhidi ya Yanga, alikiri kuwa bado kuna tatizo katika safu yake ya ushambuliaji na atalifanyia kazi kabla ya Ligi Kuu kuanza.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Crescentius Magori, alisema bado hawajamaliza kusajili mpaka dirisha litakapofungwa, lakini kabla ya hapo wanachama na mashabiki wategemee chochote kutokea.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Tanzania Yamaliza Olimpiki 2024 Mikono Mitupu
- Matokeo ya Simba Vs Coastal union Leo Ngao ya Jamii 11/08/2024
- Kikosi Cha Simba VS Coastal union Ngao ya Jamii 11/08/2024
- Matokeo ya Ngao ya Jamii 2024
- Ratiba ya Mechi za Yanga Ligi Kuu NBC 2024/2025
- Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara 2024/2025 (NBC Premier league)
Weka Komenti