Simba Yaanza Ligi Kuu 2025/26 Kwa Ushindi wa 3-0 Dhidi ya Fountain Gate
TIMU ya Simba SC imeanza msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara 2025/26 kwa moto, ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wa kuvutia uliopigwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Wekundu wa Msimbazi yamefungwa na beki wa kati, Rushine De Reuck raia wa Afrika Kusini dakika ya tano, kiungo wa kati kutoka Ivory Coast, Jean Charles Ahoua dakika ya 37, na mshambuliaji mwenye kasi raia wa Ghana, Jonathan Sowah aliyekamilisha karamu ya mabao dakika ya 57. Huu ulikuwa mchezo wa kwanza kabisa kwa Simba SC msimu huu, wakionesha nia yao ya kutwaa taji tangu mwanzo. Kwa upande wa Fountain Gate, huu ni mchezo wao wa pili baada ya kuanza kwa kufungwa 1-0 na Mbeya City Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati, mkoani Manyara, ikionesha kuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa mwanzoni mwa ligi.
Ahoua Aendeleza Ubabe, Awatesa Fountain Gate Tena
Kiungo mshambuliaji na kinara wa upachikaji mabao msimu uliopita ndani ya Ligi Kuu Bara, Charles Ahoua, ameendelea pale alipoishia msimu uliopita kwa kuitesa tena Fountain Gate, akifunga na kutoa asisti katika ushindi wa 3-0 wa Simba dhidi ya Fountain Gate.
Msimu uliopita, dhidi ya Fountain Gate kwenye Uwanja wa KMC Complex, Simba ilishinda 4-0 na Ahoua alichangia kwa kufunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao. Mabao mengine katika mchezo huo yalifungwa na Edwin Balua, Steven Mukwala, na Valentino Mashaka.
Leo, kiungo huyo aliyetupia mabao 16 msimu uliopita, ameanza kwa kishindo kwa kutoa pasi iliyozaa bao la kwanza la Simba Yaanza Ligi Kuu 2025/26 Kwa Ushindi wa 3-0 Dhidi ya Fountain Gate dakika ya tano ya mchezo. Ahoua alichonga kona murua iliyounganishwa kwa kichwa na beki Rushine De Reuck, na kuweka bao la mapema kambani.
Licha ya Fountain Gate kuingia kinyonge na kushindwa kuendana na kasi ya mchezo wa Simba, mchezaji wao Elie Mokono hakutaka kuonyesha unyonge, akijaribu mara kwa mara kulenga lango la Simba akiwa nje ya 18. Alifanikiwa kusaidia timu hiyo kuambulia kona moja dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Hata hivyo, kona hiyo haikuwa na madhara langoni mwa Simba kutokana na umakini mkubwa wa safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Ahoua alitumia dakika 37 kuifungia Simba bao la pili, akipokea pasi safi kutoka kwa kiungo mkabaji, Yusufu Kagoma, na kukwamisha mpira wavuni. Mabao hayo mawili yalidumu hadi dakika ya 45, huku Fountain Gate wakiwa wameambulia kuchonga kona moja pekee hadi mwamuzi alipopuliza kipyenga kuashiria mapumziko.
Mabadiliko Yaongeza Burudani, Sowah Afunga Kitabu Cha Mabao
Kipindi cha pili, Benchi la Ufundi la Simba lilifanya mabadiliko ya mapema. Mzamiru Yassin na Kibu Denis walitoka, nafasi zao zikichukuliwa na Morice Abraham na Alassane Kante. Mabadiliko haya yaliongeza burudani kwa mashabiki wachache waliojitokeza Uwanja wa Mkapa kushuhudia Simba Yaanza Ligi Kuu 2025/26 Kwa Ushindi wa 3-0 Dhidi ya Fountain Gate.
Mchezo ulikuwa unachezwa upande mmoja, huku kipa wa Simba, Moussa Camara, mara kadhaa akisogea juu kutoa maelekezo kwa wachezaji wenzake. Dakika ya 57, Jonathan Sowah alishindilia msumari wa tatu akipokea krosi safi kutoka kwa Elie Mpanzu.
Simba ilifanya mabadiliko mengine baadaye, akitoka mfungaji wa bao la kwanza, Rushine De Reuck, na nafasi yake kuchukuliwa na Wilson Nangu. Pia, Shomari Kapombe alimpisha David Kameta, na Yusuph Kagoma akatoka na kuingia Neo Maema.
Licha ya kipindi cha pili Simba kuonesha kiwango kizuri kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na benchi la ufundi, walishindwa kutumia nafasi nyingine walizotengeneza kwa kuingia mara kwa mara langoni kwa Fountain Gate. Hata hivyo, walijikuta wakimaliza mchezo kwa ushindi huo wa mabao 3-0, ikiwa ni ishara njema ya kuanza msimu wao wa Ligi Kuu 2025/26.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania 2025/2026
- Matokeo ya Yanga vs Pamba Jiji Leo 24/09/2025
- Vilabu Bora Afrika 2025 (CAF Club Ranking 2025)
- Hat-Trick ya Mayele Yaipa Pyramids Ubingwa wa FIFA African-Asian-Pacific
- Ratiba ya NBC Premier league 2025/2026
- Serikali Yatoa Ufafanuzi Pamba Jiji Kufanya Mazoezi Gizani Uwanja wa Taifa
- Ratiba ya Mechi za Leo 24/09/2025
Leave a Reply