Simba Yaitandika JKT na Kujiweka Kwenye Njia ya Ligi ya Mabingwa
Bao la kiungo Fabrice Ngoma alilofunga katika dakika za nyongeza kabla ya mapumziko, limetosha kuiwezesha Simba SC kuondoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi 63, hatua inayoiweka karibu zaidi na nafasi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, ikiwafuata kwa karibu watani wao wa jadi, Yanga SC.
Katika dakika za awali za mchezo, Simba ilionekana kuwa na kiu ya kutafuta bao la mapema, ikiliandama lango la JKT Tanzania kwa mashambulizi ya kasi. Licha ya juhudi hizo, safu ya ulinzi ya wenyeji JKT ilionekana kuwa imara kwa kiasi kikubwa hadi dakika ya 45 ya kipindi cha kwanza. Hata hivyo, presha ya Simba ilizaa matunda katika dakika saba za nyongeza kabla ya mapumziko.
Bao hilo lilianzia katika kona fupi iliyochorwa kwa ustadi na Jean Charles Ahoua, ambaye alimpa pasi fupi Joshua Mutale. Mutale alimuachia mshambuliaji Steven Mukwala aliyewazidi ujanja mabeki wa JKT kabla ya kupiga krosi murua iliyokamilishwa vyema na Ngoma. Hilo linakuwa bao la nne kwa kiungo huyo msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kupumzishwa katika mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa ambapo Simba ilishinda 2-1.
Katika kipindi cha pili, JKT Tanzania ilianza kwa kufanya mabadiliko ya haraka, ikimtoa Najim Magulu na kumwingiza Hassan Dillunga. Mabadiliko hayo yalileta uhai kwenye safu ya ushambuliaji ya JKT, ambao walitafuta bao la kusawazisha kwa nguvu mpya. Hata hivyo, uimara wa safu ya ulinzi ya Simba na umakini wa wachezaji wake waliweza kuhimili mashambulizi hayo bila kuruhusu bao.
Kocha wa Simba alionekana kuwa na mkakati wa kulinda ushindi huo, huku akifanya mabadiliko ya kimkakati katika kikosi chake. Steven Mukwala, Debora Mavambo, Jean Charles Ahoua, Joshua Mutale na Valentine Nouma walipumzishwa na nafasi zao kuchukuliwa na Elie Mpanzu, Che Fondoh Malone, Leonel Ateba, Ladack Chasambi na Mohamed Hussein. Mabadiliko haya yalilenga kuimarisha ulinzi na kuongeza nguvu mpya katika mashambulizi ya kushtukiza.
Kwa upande wa JKT Tanzania, nao walifanya mabadiliko kwa nyakati tofauti, ambapo Abrahim Seif alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Said Ndemla, Ramadhan Kichuya alimpisha Japhar Abdul, huku Edward Songo akichukua nafasi ya Hassan Mohammed. Pamoja na jitihada hizo, timu hiyo haikuweza kupata bao la kusawazisha kutokana na uimara wa kipa wa Simba pamoja na nidhamu ya juu ya wachezaji wa timu hiyo.
Ushindi huu ni wa pili mfululizo kwa Simba katika mechi zao za viporo, ambapo awali waliibuka na ushindi dhidi ya Mashujaa. Sasa wamebakiwa na michezo miwili dhidi ya Pamba Jiji na KMC ili kufikia idadi ya mechi 26 sawa na vinara wa Ligi Kuu, Yanga SC ambao wanaongoza kwa pointi 70.
Kwa upande wa JKT Tanzania, hii ni mara ya pili wanapoteza mchezo kwenye uwanja wao wa nyumbani msimu huu, mara ya kwanza ikiwa Februari 13 walipofungwa pia 0-1 na Singida Black Stars. Katika jumla ya mechi 14 walizocheza nyumbani, JKT wameshinda nne, kutoka sare nane na kupoteza mbili. Hivi sasa wanashikilia nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi kwa pointi 32 baada ya mechi 27, huku wakisalia na michezo mitatu pekee kabla ya kufunga msimu.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo JKT Tanzania vs Simba Leo 05/05/2025
- Sababu 3 Zilizofanya CAS Kuitupilia Mbali Kesi ya Yanga
- Shauri la Yanga CAS Lapigwa Chini, Kariakoo Derby kupangiwa Tarehe
- Kipagwile Aibuka Mchezaji Bora Ligi Kuu April 2025, Ambwaga Pacome
- Guardiola Atangaza Kupumzika Ukocha Baada ya Mkataba Wa Man City Kuisha
- Ratiba ya Kombe la Muungano 2025
- JKU vs Yanga Leo 01/05/2025 Saa Ngapi?
- Ratiba ya Fainali Kombe La Shirikisho Afrika CAF 2024/2025
- Kikosi cha Yanga vs Zimamoto Leo 29/04/2025
- Zimamoto VS Yanga Leo 29/04/2025 Saa Ngapi?
Leave a Reply