Simba Yapokewa Dar kwa Shangwe Kubwa Baada ya Mtanange Mkali Zanzibar

Simba Yapokewa Dar kwa Shangwe Kubwa Baada ya Mtanange Mkali Zanzibar

Kikosi cha Simba Sports Club kimewasili leo mchana jijini Dar es Salaam kikitokea Zanzibar, ambako kilishiriki mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane. Mchezo huo ulipigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, ambapo timu hiyo ya Tanzania ililazimishwa sare ya bao 1-1. Matokeo hayo yaliipa RS Berkane ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu wa 2024/2025.

Licha ya Simba kukosa taji hilo, timu hiyo imepokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wake pindi ilipowasili bandarini saa 7:10 mchana kwa njia ya boti. Baada ya kukamilisha taratibu za ukaguzi bandarini, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi waliingia moja kwa moja kwenye basi rasmi la timu hiyo, wakilakiwa kwa furaha isiyo kifani kutoka kwa mashabiki waliokuwa wakisubiri kwa hamu.

Mapokezi hayo yaliongozwa na vikundi vya mashabiki waliokuwa na ngoma na nyimbo za kushangilia mafanikio ya Simba, licha ya kupoteza taji. Mashabiki hao waliimba nyimbo mbalimbali zikiwasifu wachezaji, makocha, na viongozi wa klabu hiyo, wakionesha heshima kwa juhudi zilizowezesha timu hiyo kufika hatua ya fainali ya michuano ya kimataifa barani Afrika.

Shangwe hizo zilikuwa na mvuto mkubwa kiasi cha kusababisha baadhi ya shughuli bandarini kusimama kwa muda, kutokana na idadi kubwa ya watu waliokusanyika kushuhudia mapokezi hayo. Hali hiyo ilidhihirisha ukubwa wa ushawishi wa Simba na mshikamano wa mashabiki wake katika nyakati zote — za ushindi na changamoto.

Simba Yapokewa Dar kwa Shangwe Kubwa Baada ya Mtanange Mkali Zanzibar

Msafara wa timu uliondoka bandarini huku mashabiki wakiendelea kuushangilia, kabla ya hatimaye kutawanyika kwa amani. Tukio hilo limeonesha wazi kuwa Simba haikurejea mikono mitupu. Kwa kufika fainali, klabu hiyo imejihakikishia zawadi ya Shilingi bilioni 2.7 kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ikiwa ni heshima kubwa kwa soka la Tanzania.

Katika mchezo wa jana, bao la Simba lilifungwa na Joshua Mutale ambae pia alitajwa kuwa man of the match, huku RS Berkane wakisawazisha kupitia mchezaji wao Soumaila Sidibe. Sare hiyo ilisababisha Simba kukosa ubingwa, lakini haikupunguza thamani ya mafanikio yake kwenye mashindano hayo.

Mapendekezo ya Mhariri:

  1. Rs Berkane Yabeba Ubingwa Kombe la Shirikisho Afrika 2024/2025
  2. Ndoto ya Ubingwa Shirikisho ya Simba Yazimwa Baada ya Sare Amaan Complex
  3. Simba vs Berkane Leo 25/05/2025 Saa Ngapi?
  4. Matokeo ya Simba vs RS Berkane Leo 25/05/2025
  5. KIKOSI CHA SIMBA VS BERKANE LEO 25/05/2025 – FAINALI YA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA
  6. Rais Mwinyi Aahidi Mamilioni Kwa Simba Wakishinda Kombe la Shirikisho
  7. Mamelodi Sundowns Yatoshana Nguvu na Pyramids FC Pretoria
Nina uzoefu wa miaka zaidi 6 katika uandishi wa habari nchini Tanzania. Shauku yangu ni kuleta habari muhimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu na Michezo