Simba Yatolea Tamko Kuhusu Uwanja wa Marudiano CAF
Berkane, Morocco. Uongozi wa Klabu ya Simba umejitokeza kutoa ufafanuzi kwa mashabiki wake kufuatia taarifa zinazoeleza kuwa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limehamisha rasmi uwanja wa mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane kutoka Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, hadi Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kupitia kwa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, Simba imesisitiza kuwa kwa sasa nguvu zao zote zimeelekezwa katika maandalizi ya mechi ya kwanza ya fainali hiyo itakayopigwa Jumamosi, Mei 17, 2025, kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, nchini Morocco. Ahmed amewataka mashabiki kuwa watulivu na waendelee kujiandaa kwa mechi ya marudiano huku wakisubiri taarifa rasmi kutoka kwa uongozi baada ya mechi ya kwanza kumalizika.
“Taarifa rasmi kuhusiana na mechi yetu ya tarehe 25 zitatolewa punde baada ya mechi yetu ya tarehe 17. Tukishamaliza mchezo huo, tutakuja kuwaambia mustakabali wa mechi hiyo. Lakini kwa sasa, Wanasimba waendelee na maandalizi ya awali, hasa wale wa mikoani waendelee na mpango wa kuja Dar es Salaam hadi pale tutakapotoa taarifa nyingine ambayo itakuwa rasmi,” amesema Ahmed Ally.
Uwanja wa Marudiano Wahamishwa Rasmi Zanzibar
Ingawa Simba haijatoa tamko la moja kwa moja kuthibitisha mabadiliko hayo, taarifa za kuaminika zinaeleza kuwa CAF imekwishatoa maagizo ya mechi ya marudiano kupigwa Zanzibar. Tayari Klabu ya Simba, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), na Serikali wameshapokea taarifa hizo rasmi kutoka CAF.
Uamuzi huo wa CAF unakuja ikiwa ni mara ya pili kwa Simba kucheza mechi ya mashindano ya CAF msimu huu katika Uwanja wa New Amaan Complex. Awali, Simba ilitumia uwanja huo katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, ambapo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Jean Charles Ahoua, ushindi ambao uliiwezesha kufuzu hatua ya fainali.
CAF Yatoa Maagizo Mapya Kwa TFF
Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya uhakika, CAF imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanza haraka maandalizi ya mechi ya marudiano katika Uwanja wa New Amaan Complex badala ya Uwanja wa Benjamin Mkapa. Uamuzi huu unaelezwa kuwa ni pigo kwa Simba ambayo imekuwa na historia nzuri ya matokeo katika uwanja wa Mkapa, huku mechi yao ya mwisho kupoteza katika uwanja huo ikiwa ni dhidi ya Al Ahly ya Misri mnamo Machi 29, mwaka jana.
Taarifa pia zinaeleza kuwa Simba pamoja na TFF bado wanaendelea na jitihada za kuiomba CAF ifikirie upya maamuzi hayo kupitia maombi maalumu, wakizingatia umuhimu na historia ya mechi hiyo kwa klabu na mashabiki wake.
CAF Yasimamia Viwanja kwa Ajili ya CHAN na AFCON
Sababu mojawapo inayotajwa kuchangia uamuzi wa CAF ni usimamizi wake mkali juu ya viwanja vinavyotarajiwa kutumika katika mashindano ya Kimataifa, ikiwemo CHAN na AFCON. Mabadiliko haya hayajaathiri Simba pekee, kwani pia CAF imezuia Uwanja wa Nyayo nchini Kenya kutumika kwa Dabi ya Mashemeji kati ya AFC Leopards na Gor Mahia kwa hofu ya kuathiri maandalizi ya Fainali za CHAN, zitakazofanyika Kenya, Uganda, na Tanzania kuanzia Agosti 2025.
Mashabiki Watakiwa Utulivu na Subira
Licha ya mashabiki wengi kueleza kutoridhishwa na taarifa za mabadiliko ya uwanja, hasa kwa kuwa wengine tayari wameshanunua tiketi zao za kusafiri kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya mechi ya marudiano, Simba imewaomba waendelee kuwa watulivu. Uongozi umesisitiza kuwa taarifa rasmi kuhusu uwanja na maandalizi ya mechi ya marudiano itatolewa mara tu baada ya mechi ya kwanza kumalizika.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Mamelodi Sundowns Bingwa Tena wa Ligi Kuu Afrika Kusini 2024/25
- Beki wa Taifa Stars Haji Mnoga Kubaki Salford City kwa Mwaka Mwingine
- Fountain Gate Njia Panda Baada ya Kichapo Dhidi ya JKT
- Timu Zilizoshuka Daraja Ligi Kuu ya NBC 2024/2025
- Matokeo ya Yanga Vs Namungo FC Leo 13/05/2025
- Kikosi cha Yanga Vs Namungo FC Leo 13/05/2025
- Dickson Ambundo Ajiweka Sokoni Huku Fountain Gate Ikipambana Kubaki Ligi Kuu
- Yanga Yaanza Kutega Mitego ya Kumnasa Marcel Koller, Aliyekuwa Kocha Ahly
Leave a Reply