Singida Black Stars Tayari Kuivaa Kengold FC Katika Ligi ya NBC
Klabu ya Singida Black Stars imejiandaa vilivyo kwa mechi yao ya kwanza katika Ligi Kuu ya NBC msimu huu, ambapo watakutana na Kengold FC tarehe 18 Agosti kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Kocha mkuu wa Singida Black Stars, Patrick Aussems, amekiri kuwa mechi ya ufunguzi ya msimu ni changamoto kubwa hasa inapokuwa ni mechi ya ugenini. Hata hivyo, ameonyesha kujiamini na maandalizi ya kikosi chake, akisisitiza umuhimu wa kushinda mechi hiyo ya kwanza.
“Tumekuwa tukiandaa timu kwa takriban wiki tano hadi sita, na sasa ni wakati wa kuonyesha matunda ya mazoezi yetu. Wachezaji wote wana ari na morali ya juu kuelekea mechi ya Jumapili hii, japokuwa tunacheza ugenini,” alisema Aussems.
Kocha huyo aliongeza kuwa anaamini wachezaji wake wote wako katika hali nzuri kiafya na kiakili, wakiwa tayari kukabiliana na changamoto yoyote watakayoipata uwanjani. “Tunaelewa kuwa itakuwa mechi ngumu, hivyo tunahitaji kuwa tayari kisaikolojia na kuendelea kuwa na motisha. Kiufundi tupo imara, na tunahitaji kuwa na umakini na akili timamu,” aliongeza.
Kwa upande wake, mchezaji wa Singida Black Stars, Jimmyson Mwanuke, amewataka mashabiki wa timu hiyo walioko mkoani Mbeya kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao. Mwanuke alisisitiza kuwa uwepo wa mashabiki katika uwanja wa Sokoine utakuwa na mchango mkubwa katika kupata ushindi na kuwafanya wachezaji wawe na morali zaidi.
“Tunategemea nguvu na shauku ya mashabiki wetu kutupeleka kwenye ushindi. Uwepo wao kwenye uwanja unaweza kuwa na tofauti kubwa, na tunataka kuwatia moyo kwa kucheza vizuri na kuonesha kiwango bora,” alisema Mwanuke.
Kengold FC, ambayo inafanya debut yake katika Ligi Kuu ya NBC baada ya kushinda Ligi ya Championship, nayo inatarajia kuanza kampeni yao kwa kishindo. Baada ya mchezo dhidi ya Singida Black Stars, Kengold FC itaelekea kwenye mechi yao inayofuata dhidi ya Fountain Gate FC tarehe 11 Septemba katika Uwanja wa Tanzanite, Kwaraa.
Kwa ujumla, mechi hii inatarajiwa kuwa ya kusisimua, huku kila timu ikitaka kuanza msimu kwa ushindi. Mashabiki wa soka kote nchini wanatarajia kuona burudani ya hali ya juu na ushindani mkali kati ya timu hizi mbili.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Awesu Kurudi KMC Baada ya Uamuzi wa Kamati ya Sheria ya TFF
- Mfalme Mpya Madrid, Mbappé Afunga Katika Mechi ya Kwanza
- Janga la Majeruhi Laendelea Kuiandama Azam FC
- Matokeo Ya Ligi Kuu Ya NBC Tanzania 2024/2025
- Vilabu Bora Afrika 2024/2025 (CAF Club Ranking)
- Lawi Aelezea Kuhusu Kukwama kwa Uhamisho Wake Ubelgiji
- Mashujaa FC Yafunga Dirisha la Usajili kwa Kumnasa Kibaya
Weka Komenti