Tabora Utd Yalizamisha Jahazi la Kagera Mchana
Tabora United imezidi kujiongezea umaarufu katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, katika mchezo uliopigwa leo mchana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.
Ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa Tabora United katika msimu huu, huku Kagera Sugar ikipokea kipigo cha tatu mfululizo, jambo linalozidi kuzamisha matumaini ya timu hiyo inayonolewa na kocha Paul Nkata kutoka Uganda.
Mchezo ulianza kwa kasi, huku Tabora United ikionesha dhamira ya kutafuta pointi tatu muhimu. Bao pekee la mchezo huo lilifungwa dakika ya 32 kwa mkwaju wa penalti baada ya mshambuliaji wa Tabora, Yacouba Songne, kufanyiwa madhambi na beki wa Kagera Sugar, Saleh Seif. Mkwaju huo ulipigwa na kiungo Asiedu Shedrak, ambaye aliukwamisha wavuni kwa ustadi, na kumwacha kipa wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda, bila cha kufanya.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Tabora United kuwa mbele kwa bao 1-0, licha ya jitihada za Kagera Sugar kusawazisha. Katika kipindi cha pili, timu zote ziliongeza kasi ya mashambulizi, lakini umakini mdogo wa washambuliaji ulifanya mechi kuisha bila mabadiliko ya matokeo. Kagera Sugar ilijitahidi kutafuta bao la kusawazisha, huku Tabora United ikisaka kuongeza bao la pili, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda.
Ushindi wa leo unaiweka Tabora United katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi sita baada ya michezo mitatu.
Timu hiyo pia imeonyesha uwezo mkubwa wa kusimama imara mbele ya wapinzani wake, kwani kabla ya mchezo wa leo, ilifanikiwa kuichapa Namungo kwa mabao 2-1 ikiwa ugenini Lindi. Ushindi huo dhidi ya Kagera Sugar unadhihirisha dhamira ya Tabora United ya kujitengenezea jina kubwa msimu huu.
Kocha wa Tabora United, Francis Kimanzi, alielezea furaha yake baada ya mchezo huo kwa kuwapongeza wachezaji wake kwa kufuata maelekezo yake kwa ufanisi. “Nawapongeza wachezaji wangu kwa ushindi dhidi ya Kagera Sugar.
Walicheza kwa nidhamu na kufuata maelekezo tuliyowapa. Ushindi huu ni wa muhimu sana kwa timu yetu na umetupa motisha zaidi kuelekea michezo inayofuata,” alisema Kimanzi.
Kimanzi aliongeza kuwa, kwa msimu uliopita, Kagera Sugar iliweza kuwafunga nyumbani na kupata alama nne dhidi yao, lakini ushindi wa leo unaonyesha kwamba Tabora United imefuta uteja na imejipanga vyema kwa msimu huu. “Makosa ambayo yamekuwa yakitokea tutayafanyia kazi, ili tuwe na timu imara zaidi,” alisisitiza.
Kwa upande wa Kagera Sugar, hali inaonekana kuwa ngumu zaidi. Kikosi hicho kimepoteza mechi tatu mfululizo, jambo ambalo si la kawaida kwa timu hiyo. Kocha Paul Nkata alikiri kuwa matokeo haya ni pigo kubwa kwa timu yake, lakini aliweka wazi kuwa kikosi chake kinakosa bahati licha ya kujitahidi katika kila mchezo.
“Tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini hatukuwa na bahati ya kuzitumia. Tumepoteza mechi tatu mfululizo, jambo ambalo si nzuri kwa morali ya timu,” alisema Nkata.
Nkata aliahidi kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza katika michezo ya awali, akisema kuwa wamekuwa wakifanya makosa yanayojirudia, ambayo yanawagharimu. Aliongeza kuwa lengo lao ni kurejea nyumbani na kujipanga upya ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwenye mechi zinazofuata.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Fountain Gate Yazindua Dimba la Tanzanite Kwaraa kwa Ushindi Ligi Kuu
- Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara 2024/2025
- Heritier Makambo Ashangazwa na Ubora wa Ligi Kuu
- Mudathir Atema Cheche za Moto Kwa Wanaoponda Wachezaji Wazawa
- Nyota Wa Kuchungwa Zaidi Mechi Ya Al Ahli Vs Simba
- Rekodi za Yanga CAF Dhidi ya Timu za Ethiopia
- Ahmed Ally Atema Nyongo Kuhusu Kagoma
- Yao Arejea Mazoezini Yanga, Gamondi Ashusha Presha
Weka Komenti