Taoussi Atuliza Presha Kabla ya Azam Kukipiga na Coastal
Klabu ya Azam FC inajiandaa kupambana na Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam. Huku mechi hii ikiwahusisha timu zinazotofautiana kimaendeleo kwenye msimamo wa ligi, kocha wa Azam, Rachid Taoussi, anaonekana kutuliza presha huku akisisitiza kuwa anahitaji muda zaidi kuimarisha kikosi chake licha ya ushindi wa mabao 4-0 walioupata dhidi ya KMC katika mechi iliyopita.
Rachid Taoussi, ambaye ametua Azam hivi karibuni akitokea Morocco, amekuwa akisisitiza kuwa bado anajifunza timu na wachezaji wake. Ingawa alifurahishwa na ushindi wa KMC, anaamini kuwa timu yake inahitaji kuendelea kuimarika.
“Tuna wachezaji wenye uwezo mkubwa kiufundi na morali ya ushindi ipo juu. Kurejea kwa wachezaji waliokuwa majeruhi na waliokuwa kwenye timu za taifa kumesaidia kuongeza nguvu kikosini,” alisema Taoussi.
Mkakati wa Muda Mrefu kwa Ajili ya Azam
Kocha huyo alieleza kuwa lengo lake sio mafanikio ya haraka bali ni kujenga timu imara kwa muda mrefu. Akizungumza kuhusu mechi zao za awali, alikiri kuwa timu haikuwa katika uwezo wake kamili kwenye mechi dhidi ya Pamba Jiji kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa nje.
Lakini sasa, baada ya wiki mbili za mazoezi, wachezaji wameonyesha kuelewa vyema maelekezo aliyowapa. “Katika mazoezi tumekuwa tukijifunza kuhusu nidhamu ya kiufundi, na hilo limeanza kuzaa matunda.”
Taoussi aliongeza kuwa moja ya mikakati muhimu kwenye timu yake ni kuhakikisha wachezaji wanajua ni wapi wanatakiwa kuwa wakati timu inashambulia na wakati wanapoteza mpira. “Tunapopoteza mpira, tunarudisha haraka ndani ya sekunde 5-7, na tunapokuwa na mpira, tunakuwa makini na kutengeneza nafasi za kufunga,” alifafanua.
Taoussi ameonya wachezaji wake dhidi ya kulewa na ushindi wao wa mabao 4-0 dhidi ya KMC, akisisitiza kuwa kazi bado haijakamilika. “Ni muhimu tusibweteke na kusherehekea ushindi huu, tunapaswa kuelekeza nguvu kwenye mechi zinazokuja,” alisema huku akiongeza kuwa kila mechi inahitaji mbinu tofauti na timu zote zinapaswa kupewa heshima. “Kila mechi ni changamoto mpya, na lazima tujipange vizuri dhidi ya kila timu tunayoikabili.”
Moja ya malengo ya kocha huyo ni kuleta mabadiliko kwenye kikosi kwa kuwapa nafasi wachezaji chipukizi kutoka akademi ya Azam. “Ni muhimu klabu yetu kutoa nafasi kwa vijana chipukizi ili waongeze nguvu kwenye timu kuu.
Pia tutahakikisha kuwa wachezaji waliocheza mechi nyingi wanapata muda wa kupumzika ili kuepuka majeraha,” alisema Taoussi, akionyesha kuwa anajali maendeleo ya wachezaji wake kwa muda mrefu.
Coastal Union na Uhitaji wa Pointi
Kwa upande mwingine, Coastal Union wameanza msimu kwa kusuasua, wakifanikiwa kukusanya pointi moja tu kwenye michezo mitatu waliyocheza. Timu hiyo ilipoteza mechi mbili za awali na kwa sasa inakabiliwa na presha kubwa ya kujitahidi kutoka kwenye nafasi ya chini ya msimamo wa ligi. Hii inawafanya kuwa wapinzani hatari, kwani wanahitaji ushindi ili kujinasua kwenye hali hiyo ngumu.
Mapendekezo ya Mhariri:
Weka Komenti