Waamuzi wa Mechi ya Yanga vs Simba 01/03/2026
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga SC, wanatarajiwa kukutana uso kwa uso na watani wao wa jadi Simba SC katika pambano la Ligi Kuu Bara litakalotikisa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Machi 1, 2026 kuanzia saa 2:15 usiku.
Homa ya Kariakoo Dabi imepanda maradufu huku mashabiki wakihesabu saa kuelekea mchezo huo ambao unatajwa kuwa wa 115 kati ya timu hizo tangu kuanzishwa kwa Ligi Bara mwaka 1965. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mechi hiyo pia itakuwa ya kwanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara, lakini tayari timu hizo zilishakutana mapema katika Ngao ya Jamii Septemba 16, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Yanga ilishinda bao 1-0 kupitia kwa Pacome Zouzoua dakika ya 54.
Katika kuelekea pambano hilo kubwa, Shirikisho limetangaza rasmi waamuzi wa mechi ya Yanga vs Simba 01/03/2026, ambao watasimamia dakika 90 za mchezo huo wenye mvuto mkubwa nchini.
Orodha ya Waamuzi wa Mechi ya Yanga vs Simba 01/03/2026
Kwa mujibu wa taarifa rasmi, waamuzi watakaochezesha dabi hiyo ni:
- Mwamuzi wa kati: Nassoro Mwinchui (Tanga)
- Mwamuzi Msaidizi 1: Kassim Mpanga (DSM)
- Mwamuzi Msaidizi 2: Hamdani Said (Mtwara)
- Mwamuzi wa Akiba: Ramadhan Kayoko (DSM)
- Mtathmini wa Waamuzi: Israel Mjuni (DSM)
Uteuzi wa waamuzi hao unakuja wakati presha ya pambano hilo ikiendelea kupanda, huku kila upande ukihitaji ushindi ili kujihakikishia mwanzo mzuri wa msimu katika Ligi Kuu Bara.
Historia na Muktadha wa Dabi
Kariakoo Dabi imeendelea kubaki miongoni mwa mechi zenye mvuto mkubwa barani Afrika, ikitajwa kushika nafasi ya nne kwa ubora na ushindani wake. Tangu mwaka 1965, Simba na Yanga zimekutana mara 115 katika Ligi Bara, jambo linaloonesha ukubwa wa historia ya pambano hilo. Katika mechi sita zilizopita za mashindano mbalimbali, Simba haijapata ushindi dhidi ya Yanga.
Aidha, katika mechi ya mwisho ya msimu wa 2024/2025 iliyopigwa Juni 15 mwaka jana, Simba ilipoteza kwa mabao 2-0, matokeo yaliyoiwezesha Yanga kutwaa taji la nne mfululizo.
Mchezo wa Machi 1, 2026 utakuwa wa kwanza kwa Ligi Kuu Bara kuchezwa Zanzibar kati ya vigogo hao, ingawa timu hizo tayari zimeshawahi kukutana visiwani humo katika michuano mingine ikiwamo Kombe la Mapinduzi na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) miaka ya 1975 na 1992.
Mapendekezo ya Mhariri:









Leave a Reply