Yanga Kucheza na CBE SA Ya Ethiopia Klabu Bingwa Septemba 2024
Mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Young Africans Sports Club (Yanga SC), wamefuzu kushiriki raundi ya pili ya hatua ya awaali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) baada ya kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 10-0 dhidi ya Vital’O FC ya Burundi. Ushindi huu ambao bila shaka utakua katika vitabu vya historia vya michuano hii umeweka Yanga SC kwenye ramani ya soka la Afrika, wakijiandaa kukutana na klabu ya Benki ya Biashara ya Ethiopia (CBE SA) katika raundi inayofuata.
Ushindi Dhidi ya Vital’O FC: Uthibitisho wa Ubora wa Timu ya Wananchi
Yanga SC ilionyesha ukomavu wa hali ya juu walipokutana na Vital’O FC katika michezo miwili ya awali. Katika mchezo wa marudiano uliofanyika Agosti 24, 2024, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 6-0, baada ya kupata ushindi wa 4-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Agosti 17, 2024.
Mchezaji Pacome Zouzou alikuwa wa kwanza kufunga, akiweka Yanga mbele dakika ya 14, na kufuatiwa na mabao mengine kutoka kwa Clement Mzize, Clatous Chama, Prince Dube, Stephanie Aziz Ki, na Mudathir Yahaya.
Ushindi huu uliwapa Yanga SC tiketi ya kufuzu raundi ya kwanza ya CAF Champions League, huku wakikusanya pongezi na tuzo mbalimbali, ikiwemo shilingi milioni 50 kutoka kwa Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hatua Inayofuata kwa Yanga ni Kukabiliana na CBE SA ya Ethiopia
Baada ya kutinga raundi ya kwanza, Yanga SC sasa inajiandaa kwa mtihani mwingine mkubwa mbele yao, ambapo watakutana na Benki ya Biashara ya Ethiopia (CBE SA). Timu hii ya Ethiopia ilifuzu kwa raundi hii baada ya kupata ushindi wa jumla wa mabao 3-2 dhidi ya Villa SC ya Uganda. Mechi ya kwanza itachezwa Septemba 13, 2024, nchini Ethiopia, huku marudiano yakitarajiwa kufanyika Septemba 20, 2024, Tanzania, visiwani Zanzibar katika Uwanja wa New Amaan Complex, kwa mujibu wa Rais wa Yanga SC, Hersi Said.
Maandalizi ya Kocha Miguel Gamondi
Kocha Mkuu wa Yanga SC, Miguel Gamondi, ameanza maandalizi ya kina kuelekea mchezo dhidi ya CBE SA. Ameeleza kuwa ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake katika michezo iliyopita na sasa anaelekeza nguvu kwenye kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika michezo ijayo, ikiwemo michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na mechi za CAF Champions League. Gamondi amesisitiza kuwa wanahitaji kujipanga vizuri dhidi ya CBE SA kwa kufuatilia ubora wa wapinzani wao, wakiwa nyumbani na ugenini.
Matarajio ya Yanga SC Katika Michuano ya Afrika
Yanga SC imeweka malengo makubwa katika michuano ya CAF Champions League msimu huu, na wanatarajia kufanya vyema zaidi ya msimu uliopita. Ushindi dhidi ya CBE SA utawapa nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya makundi ya CAF Champions League 2024/25, hatua ambayo itawaweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuandika historia mpya katika soka la Afrika.
Mashabiki wa Yanga SC na wadau wa soka nchini Tanzania wanaendelea kuwa na matumaini makubwa ya kuona timu yao ikifanya vyema kwenye michuano hii, huku ikiwakilisha vyema taifa katika ngazi ya kimataifa.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Coastal Union Yatolewa Kombe la Shirikisho CAF
- Usajili wa Mukwala na Ahou Waanza Kulipa Msimbazi
- Matokeo Simba Vs Fountain Gate Leo 25/08/2024
- PSG Hatarini Kufungiwa Kushiriki UEFA Baada ya Mbappe Kudai €55M za Mishahara na Marupurupu
- Ronaldo Azindua Rasmi Chaneli ya YouTube
- Tabora United Yaahidi Kulipiza Kisasi kwa Namungo Mchezo Ujao wa Ligi Kuu
- Ateba Tayari Kutinga Uwanjani: Simba SC vs Fountain Gate
Weka Komenti