Yanga Sc Yalazimishwa Sare Ya 0-0 Na Mbeya City
Wananchi, Young Africans SC wamejikuta wakidondosha pointi muhimu kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kulazimishwa sare tasa ya 0-0 na wenyeji Mbeya City FC katika dimba la Sokoine jijini Mbeya. Kwa matokeo hayo, Yanga SC wanakua wamefikisha jumla ya pointi 4 baada ya michezo miwili na kupanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimi wa 2025/2026, huku Purple Nation wakipaa hadi nafasi ya saba kwa alama 4 baada ya michezo mitatu.
Hii ikiwa ni sare ya kwanza ya Kocha Mkuu wa Yanga, Roman Folz, tangu atambulishwe rasmi kikosini, matokeo hayo yametoa taswira ya changamoto mpya kwa mabingwa hao watetezi. Kabla ya mchezo huu, Yanga SC walikuwa na rekodi ya ushindi katika michezo minne mfululizo, ikiwemo Ngao ya Jamii dhidi ya watani wa jadi, Simba SC, na michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Willete ya Angola ambayo waliimaliza kwa jumla ya mabao 5-0.
Kwa upande wa Mbeya City, walikuwa wakitafuta kuendeleza mwendelezo mzuri baada ya kushinda dhidi ya Fountain Gate kwa bao 1-0 na kupoteza 2-0 dhidi ya Azam FC. Ikumbukwe pia, timu hizi zilikutana mara ya mwisho Juni 6, 2023 katika mchezo uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3, huku City wakitangulia mabao matatu kupitia Richardson Ngy’ondya (mawili) na George Sangija, na Yanga kusawazisha kupitia Bernard Morison (mawili) na Salum Aboubakar.
Mchezo Ulivyokuwa Dimba la Sokoine
Dakika tano za mwanzo zilishuhudia Yanga wakilisakama lango la Mbeya City kwa kasi, lakini kipa Beno Kakolanya pamoja na safu ya ulinzi ya City wakawa imara. Baada ya hapo, wenyeji walicharuka na kuufanya mchezo kuwa wa mashambulizi kwa pande zote mbili.
Katika kipindi cha kwanza, Yanga walipata kona tatu dhidi ya moja ya City, lakini nafasi zote hazikuzaa matunda. Mbeya City walipiga mashuti mawili nje na moja lililolazimisha kipa Djigui Diara kudaka kwa umakini, huku Kakolanya akiokoa mashuti mawili ya hatari kutoka kwa washambuliaji wa Yanga. Takribani mashuti matano zaidi ya Yanga yaliishia nje ya lango.
Mchezaji aliyeng’aa zaidi kipindi cha kwanza alikuwa beki Ibrahim Ame wa Mbeya City kwa kuokoa mashambulizi kadhaa ya hatari, huku upande wa Yanga akitajwa zaidi Pacome ZouZoua aliyewapa wakati mgumu mabeki wa City.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuongeza mashambulizi, lakini Mbeya City walifanya mabadiliko mapema, kumtoa Willy Mwani aliyeumia na kumuingiza Peter Mwalyanzi. Yanga nao walibadili safu ya ushambuliaji: Doumbia alitoka nafasi yake ikachukuliwa na Ecua, kisha Maxi Nzengeli na Duke Abuya wakatolewa kuwapisha Kouma na Edmund John dakika ya 67. Dakika ya 79, Israel Mwenda alimpisha mshambuliaji hatari Prince Dube, lakini bado matokeo hayakubadilika.
Kauli Baada ya Mchezo
Akizungumza mara baada ya mchezo, Kocha Folz alikiri ugumu aliokutana nao, akisisitiza kuwa sehemu kubwa ya changamoto ilikuwa katika safu ya ushambuliaji kushindwa kutumia nafasi walizopata. Ameahidi kutumia muda wa mapumziko ya ligi kusahihisha makosa hayo, huku akiwataka mashabiki kuwa wavumilivu.
Kwa upande wake, Afisa Habari wa Yanga Ally Kamwe alisema wamesikia kilio cha mashabiki waliopaza sauti kwa maneno ya “Hatumtaki” baada ya mchezo, lakini uongozi unafanya tathmini ya kina kabla ya kuchukua maamuzi yoyote. Alisisitiza pia kuwa Uwanja wa Sokoine umeendelea kuwa mgumu kwa Yanga kupata matokeo mazuri, jambo linalothibitisha ugumu wa sare hii ya 0-0.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Matokeo ya Yanga vs Mbeya City Leo 30/09/2025
- Ratiba ya Mechi za Leo 30/09/2025 Ligi Kuu ya NBC
- Ratiba ya Kombe la Shirikisho Afrika CAF 2025/2026
- Mbeya City vs Yanga sc Leo 30/09/2025 Saa Ngapi?
- Arsenal yapata ushindi wa dakika za mwisho dhidi ya Newcastle United
- Wapinzani wa Simba Raundi ya Pili Ligi ya Mabingwa Afrika CAF
- Azam FC Yafuzu Raundi ya Pili CAFCC Baada ya Ushindi wa 4-0 Dhidi ya El Merriekh
- Simba vs Gaborone Leo 28/09/2025 Saa Ngapi?
- Singida Black Stars Yatinga Raundi Ya Pili Kombe la Shirikisho Afrika
Leave a Reply