Yanga vs Simba 01/03/2026 Saa Ngapi?
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga SC, wanatarajiwa kuvaana na watani wao wa jadi Simba SC katika pambano kubwa la Ligi Kuu litakalopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Jumapili ya Machi 1, 2026 kuanzia saa 2:15 usiku.
Huku masaa yakihesabika kuelekea mchezo huo, presha ya dabi hiyo imeendelea kupanda miongoni mwa mashabiki, wanachama na wadau wa soka nchini wanaosubiri kwa hamu kushuhudia sura nyingine ya ushindani mkubwa zaidi katika kandanda ya Tanzania.
Timu hizo tayari zilishakutana msimu huu katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Septemba 16, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Simba ilipoteza kwa bao 1-0, lililofungwa na Pacome Zouzoua dakika ya 54.
Mchezo wa Jumapili pia utakuwa wa kwanza kwa vigogo hao wa Ligi Kuu kukutana Zanzibar katika mechi ya ligi, ingawa waliwahi kucheza visiwani humo katika mashindano mengine, yakiwamo Kombe la Mapinduzi na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kagame Cup, mwaka 1975 na 1992.
Simba inaingia kwenye pambano hilo ikisaka ushindi wake wa kwanza dhidi ya Yanga baada ya kushindwa kupata ushindi katika mechi sita mfululizo zilizopita za mashindano mbalimbali. Katika mechi ya mwisho iliyofunga msimu wa 2024-2025, Simba ilifungwa mabao 2-0, matokeo yaliyoipa Yanga ubingwa wa nne mfululizo.
Pambano hilo pia litakuwa la kwanza kwa makocha Steve Barker wa Simba na Pedro Goncalves wa Yanga kukutana katika Dabi ya Kariakoo ya Ligi Kuu, baada ya wote kuingia mwishoni mwa mwaka jana.
Mapendekezo ya Mhariri:









Leave a Reply