Yanga Yaanza Kutega Mitego ya Kumnasa Marcel Koller, Aliyekuwa Kocha Ahly
Klabu ya Yanga SC inajiandaa kushuka dimbani leo jioni dhidi ya Namungo FC katika muendelezo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara raundi ya 27, lakini wakati huo huo, ndani ya vyumba vya maamuzi vya uongozi wa klabu hiyo, kuna harakati za kimya kimya zinazoendelea kuhusu mustakabali wa benchi la ufundi kwa msimu ujao.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa Yanga imeanza mazungumzo ya awali na wasimamizi wa aliyekuwa kocha wa Al Ahly ya Misri, Marcel Koller, raia wa Uswisi, kwa nia ya kumvutia aje kuinoa timu hiyo yenye makao yake makuu Jangwani, Dar es Salaam.
Hatua hii inakuja wakati tetesi zikizidi kuenea kuwa Yanga huenda ikaachana na kocha wake wa sasa, Miloud Hamdi, baada ya msimu huu kumalizika. Koller, ambaye amewahi kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili mfululizo akiwa na Al Ahly, ameachana na miamba hao wa Misri baada ya kushindwa kuifikisha timu hiyo fainali msimu huu.
Al Ahly ilitolewa katika hatua ya nusu fainali kwa mshangao na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, matokeo yaliyomuweka katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki wake waliomrushia makopo uwanjani mara baada ya kutolewa.
Licha ya kuwa alikuwa miongoni mwa makocha waliolipwa vizuri zaidi barani Afrika, Yanga haijaogopa kuchukua hatua ya kumfuata Koller. Vyanzo vya ndani ya klabu vinaeleza kuwa mradi wa maendeleo wa klabu hiyo umetumwa kwa wasimamizi wa Koller kwa ajili ya tathmini, huku uongozi ukisubiri majibu kuhusu uwezekano wa kufanya kazi na kocha huyo mwenye hadhi ya kimataifa.
Afisa mmoja wa juu wa Yanga alinukuliwa akisema:
“Inajulikana kwamba Koller alikuwa analipwa fedha nyingi, lakini ile ni Ahly na hii ni Yanga. Tumewapa mradi wetu wataupima na kufanya uamuzi, tunasubiri majibu yao.”
Kauli hiyo inaashiria dhamira ya dhati ya klabu ya Jangwani kuwa na benchi la ufundi lenye uzoefu na mafanikio makubwa barani Afrika. Malengo ya klabu hiyo kwa sasa ni kuwa na makocha waliowahi kufika hatua za juu kwenye mashindano ya CAF—nusu fainali, fainali au hata kutwaa ubingwa kabisa.
Mbali na Koller, Yanga pia inatajwa kuwa kwenye mazungumzo ya awali na Jose Riveiro, raia wa Ureno ambaye amehitimisha msimu akiwa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Riveiro aliiongoza Pirates hadi hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kabla ya kutolewa na Pyramids ya Misri. Taarifa kutoka Afrika Kusini zinaeleza kuwa tayari kocha huyo amewaaga mabosi wa klabu yake kwa ajili ya kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Hali hiyo imezua ushindani wa kimyakimya baina ya klabu kubwa Afrika, kwani taarifa zaidi zinaonesha kuwa Al Ahly nayo imeonesha nia ya kumrejesha Riveiro katika soka la Kiarabu. Waarabu hao wameanza mipango ya kumtafuta kocha mwingine mkubwa kutoka barani Ulaya baada ya kushindwa kumshawishi Rafa Benitez wa Hispania, ambaye alikataa ofa kubwa iliyowasilishwa kwake.
Wakati hayo yakiendelea, jioni ya leo Yanga itaendelea na kampeni yake ya kuwania taji la Ligi Kuu kwa kuvaana na Namungo kwenye Uwanja wa KMC Complex, ikiwa ni miongoni mwa mechi nne zinazopigwa leo kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Mechi nyingine ni kati ya JKT Tanzania dhidi ya Fountain Gate saa 8 mchana, KenGold dhidi ya Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Sokoine saa 10:00 jioni, na usiku Azam FC watamenyana na Dodoma Jiji FC.
Mapendekezo ya Mhariri:
- Simba Yaendelea Kugawa Dozi Kwa Kila Anayekutana Naye Ligi Kuu
- Kikosi cha Yanga Vs Namungo FC Leo 13/05/2025
- Matokeo ya Yanga Vs Namungo FC Leo 13/05/2025
- Yanga Vs Namungo FC Leo 13/05/2025 Saa Ngapi?
- Xabi Alonso Atangazwa Kuwa Kocha Mpya wa Real Madrid Hadi 2028
- Simba Sc vs KMC leo 11 May 2025 Saa Ngapi?
- Simba Yapewa Vitisho Vikali na KMC Kuelekea Mechi ya Kesho Mei 11, 2025
- Napoli Yajipanga Kumsajili Jack Grealish Kutoka Man City
- KENGOLD Yapanga Kuipeleka Simba Ruvuma Juni 18
- Simba SC Yakata Tiketi Ligi ya Mabingwa Afrika 2025-2026 Baada ya Kufikisha Pointi 66
Leave a Reply